Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Mosha Mahona ameuawa na
wananchi baada ya kuwachoma kwa kisu abiria watano waliokuwa kwenye
daladala linalofanya safari zake kati ya Posta na Ubungo Simu 2000.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema jana kuwa tukio
hilo lilitokea juzi saa moja usiku katika eneo la Magomeni Usalama na
Mahona aliuawa kwa kushambuliwa na wananchi baada ya kudhuru abiria
wenzake.
Kamanda Wambura alisema Mahona alikuwa ndani
ya daladala hilo lililokuwa likitokea Posta kwenda Kituo cha Simu 2000
ndipo alipotoa kisu hicho na kuwashambulia wenzake sehemu mbalimbali ya
miili yao.
“Mahona aliuawa na wananchi baada ya
kuwachoma kwa visu abiria watano ambao walipelekwa katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili kwa matibabu. Majeruhi hao wanaendelea vizuri,”
alisema Wambura.
Wambura alisema baada ya Mahona kufanya kitendo hicho walianza kumshambulia na kusababisha kifo chake.
Aliwataja abiria waliochomwa visu kuwa ni; Daudi Mwenera, Geogre Nomani, Bakari Andrew, Zawadi Mwaipopo na Eda Kiwege.
Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi ili kujua sababu ya marehemu huyo kufanya kitendo.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
Hilo ni tukio la kwanza la aina yake kwa abiria kuchoma visu wenzake.
0 comments:
Post a Comment