Ndugu waandishi wa habari na ndugu Watanzania wenzangu.
Yamepita
majuma mawili tangu mchakato wa kuchagua mgombea urais wa Tanzania
kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ukamilike. Nimetumia muda huu
kutafakari kwa kina yaliyotokea Dodoma na hatima yangu katika siasa
nchini. Ninajua marafiki wengi na wananchi wenzangu wanaoniunga mkono
wamekuwa wakisubiri kwa hamu nitoe kauli.
Nilipokuwa
natangaza nia ya kugombea urais kule Arusha, nilieleza nia yangu ya
kuanza mchakamchaka wa maendeleo ya nchi yetu na kuondokana na umaskini.
Pamoja na yaliyotokea Dodoma, azma hii bado iko palepale.
Lakini
nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa
rehema aliyetupa sisi pumzi ya kuendelea kuwa wazima wa afya njema hadi
hivi sasa. Nawashukuru pia mke wangu Regina, wanangu, wanafamilia na
marafiki wote kwa mapenzi, msaada na uvumilivu wao wakati wa kipindi
hiki kigumu tunachopitia. Nawashukuru sana pia maelfu ya wanachama wa
CCM walionidhamini na mamilioni zaidi walioniunga mkono.
Katika
safari zangu za mikoani wakati wa kuomba udhamini, nilitiwa hamasa na
umati mkubwa wa watu waliojitokeza kuniunga mkono.Aidha, ninawashukuru
sana wana kamati wangu, makundi mbalimbali na mamilioni ya vijana
wakiwamo; “For You Movement”, “Friends of Lowassa” “Team Lowassa”, Umoja
wa Bodaboda na wengine wengi ambao walijitolea kwa hali na mali katika
Safari yetu ya Matumaini.
Nitakuwa sijahitimisha orodha
ya shukrani iwapo nitaacha kuwashukuru viongozi wa dini zote nchini
ambao waliungana na waumini wao wengi katika maombi na kwa kuniunga
mkono. Najua sote tumevunjika moyo kwa yaliyotokea Dodoma na mazingira
yaliyopelekea matokeo yale.
Kama ilivyokwishaelezwa,
mchakato wa kuteua wagombea uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa
maadili, uvunjaji wa Katiba na taratibu za uchaguzi za CCM.
Zaidi
ya hayo uchaguzi ulisimamiwa kwa upendeleo dhahiri na chuki
iliyokithiri dhidi yangu. Kikatiba, Kamati ya Maadili si chombo rasmi na
haina madaraka ya kuchuja na kupendekeza majina miongoni mwa wale
wanaoomba kugombea Urais kupitia CCM.
Kilichotokea
Dodoma ni kupora madaraka ya Kamati Kuu na kukiuka katiba ya CCM. Aidha,
Kamati Kuu na Halmashauri Kuu viliitishwa na kuburuzwa ili vitekeleze
azma ya watu binafsi pasipo kujali demokrasia, katiba, kanuni na
taratibu za uchaguzi ndani ya CCM. Niliwekewa mizengwe na kuzushiwa
majungu na uongo mwingi, kuhakikisha kuwa jina langu halifikishwi mbele
ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kujadiliwa licha ya ukweli usiopingika
kuwa nilikuwa mgombea anayeungwa mkono na wananchi na wanachama wengi wa
CCM kuliko wenzangu wote. Kibaya zaidi ni kile kitendo cha kuwanyima
wagombea wote 38 haki ya kujieleza mbele ya Kamati Kuu.
Ni
dhahiri kwamba njama dhidi yangu ndani ya CCM si jambo jipya.Kumekuwa
na mkakati wa siku nyingi wa kulichafua jina langu kwa uzushi na uongo
usio na kifani. Aidha, mmeshuhudia jinsi vijana kadhaa walivyotumika
kunikashifu na kunitukana na bila aibu na uongozi wa CCM na Serikali
kuwazawadia madaraka makubwa.
Kwa namna ya kipekee
napenda kuwapongeza na kuwashukuru wazee wetu akiwamo Mzee Kingunge
Ngombale Mwiru na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ikiwa ni pamoja na
waheshimiwa Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Alhaj Adam Kimbisa kwa
uadilifu na ushujaa wao mkubwa wa kuisimamia katiba ya CCM na misingi ya
haki na kukataa maamuzi batili ya Kamati ya Maadili na Kamati Kuu
kuhusu uteuzi wa wagombea.
Cha msingi kuzingatia ni
kuwa ili kuhitimisha njama za kunipora mimi na wagombea wengine haki
zetu za msingi za kusikilizwa, viongozi wachache walikuwa tayari kupanda
mbegu ya chuki na mfarakano ambao ni mfano mbaya kwa CCM na hata Taifa
letu. Watanzania walitarajia chama kinachoongoza nchi kiwe ni mfano wa
utawala wa sheria na kinara katika kutetea misingi ya haki na demokrasia
na siyo kuihujumu. Yaliyotokea Dodoma yameitia dosari nchi yetu.
Kwa
kifupi, ninaamini sikutendewa haki katika mchakato mzima wa kupendekeza
majina na kuteua mgombea wa urais kupitia CCM. Nilinyimwa haki yangu ya
msingi ya kusikilizwa na kuchaguliwa.
Kwa mantiki hii
nitakuwa mnafiki kama nitaendelea kujidanganya mimi mwenyewe na umma wa
Watanzania kwa kusema kuwa bado nina imani na CCM au kuwa CCM ni chama
kitakachowaletea ukombozi wa kweli wa kiuchumi, kisiasa na kijamii. CCM
niliyoiona Dodoma siyo tena kile chama nilichokulia na kilichonipa
malezi na maadili ya siasa yaliyojengwa kwenye misingi ya haki, usawa na
uadilifu.
Ni dhahiri kwamba CCM imepotoka na kupoteza
mwelekeo na sifa ya kuendelea kuiongoza Tanzania yetu. Mimi kama
Mtanzania aliye na uchungu na nchi yake nasema imetosha na SASA BASI!
Kama
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyosema, CCM siyo
baba yangu wala mama yangu na kwamba kama Watanzania hawapati mabadiliko
ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Sasa tuyatafute mabadiliko nje ya
CCM.
Hivyo basi, baada ya kutafakari kwa kina nimeamua
kuwa kuanzia leo ninaondoka CCM na kuitikia wito wa Ukawa kupitia Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuungana nao katika kuleta
mabadiliko ya kweli ya nchi yetu. Navishukuru vyama vyote vya siasa
chini ya Ukawa, yaani Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kwa mwaliko wao
na imani yao na kuthamini mchango ninaoweza kutoa kufanikisha azma ya
kuleta mabadiliko na maendeleo ya kweli ya Taifa letu. Waheshimiwa
Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba, Mheshimiwa James Mbatia na
Emmanuel Makaidi asanteni sana.
Ndugu zangu, sikuufanya
uamuzi huu kwa pupa, lakini unafika wakati wa kuchukua maamuzi hata
kama ni magumu kwa kuamini fika kuwa ni kwa masilahi ya Taifa letu.
Nimejiridhisha
kuwa ndani ya Ukawa Taifa letu linayo fursa ya pekee na ya kihistoria
kushinda Uchaguzi Mkuu ujao na ya kuleta mabadiliko ya msingi katika
nchi yetu. Kwa uamuzi na ushiriki wangu huu, ninaamini kwa dhati kuwa
tutaondoa uhodhi wa madaraka wa chama kimoja na kujenga demokrasia yenye
ushindani wa kweli kisiasa.
Namalizia kwa kutoa wito
kwa Watanzania wenye nia njema na nchi yetu na wanaotaka kujenga
demokrasia na kuleta mageuzi na maendeleo ya kweli, kujiunga nasi katika
safari hii mpya ya kuinusuru nchi yetu.
Safari ya
Matumaini inaendelea kupitia Ukawa lakini haitafanikiwa iwapo sote
hatutajiandisha kupiga kura. Natoa wito kwa wakazi wa Dar es salaam,
kutumia fursa iliyopo kujiandikisha kwa wingi.
Aidha,
nawakumbusha Watanzania kote nchini waliojiandikisha kutunza shahada zao
na kukumbushana kupiga kura ili ifikapo Oktoba mwaka huu tupate ushindi
wa kishindo.
Ndugu zangu Watanzania, tuungane pamoja kuuondoa umaskini na kuleta mabadiliko ya kweli.
NARUDIA CCM SIYO MAMA YANGU
0 comments:
Post a Comment