Kinara, Selemani Shabani Ulatule.
WAKATI jeshi la
polisi nchini likiendelea kuwasaka watuhumiwa wa mauaji ya polisi na
kupora silaha katika Kituo cha Stakishari, Ilala jijini Dar, Uwazi
limefanikiwa kuipata picha ambayo inadaiwa ni ya mtuhumiwa kinara wa
tukio hilo aliyetajwa kwa jina la Seleman Shaban Ulatule.
ENEO LA TUKIO
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wanahabari
wetu walifika katika Kijiji cha Mandikongo, Mkuranga, Pwani na wakazi
wa maeneo ya jirani wakiwa katika hofu baada ya watuhumiwa hao waliokuwa
wakiishi jirani na kijiji hicho kutoweka.
NGOME YAO YATEKETEZWA
Wanahabari wetu walioambatana na afisa
mtendaji wa Kijiji cha Mandikongo, polisi na wanajeshi wa Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ), walishuhudia makazi ya watu hao yakiwa
yameteketezwa kwa moto na wananchi wenye hasira kali.
WANANCHI WAZUNGUMZA
Wakizungumzia tukio hilo, wakazi wa
kijiji hicho walisema majambazi hao waliokuwa wamejitenga na makazi ya
wanakijiji, walitoweka na familia zao baada ya kupata taarifa kuwa kuna
msako mkali unaofanywa na jeshi la polisi ambao ulifanikiwa kuwakamata
baadhi ya watuhumiwa, bunduki 15 za kivita na fedha zaidi ya shilingi
milioni 170.
Shimo ambamo zilifichwa millioni 170.
WALIVYOFICHA FEDHA
Wakizidi kuelezea tukio hilo, wakazi hao
waliwaonesha waandishi wetu shimo ambalo walilitumia kuhifadhia fedha
hizo ambapo juu yake waliweka kinyesi cha binadamu kilichokadiriwa kuwa
ni cha watu saba ikiwa ni alama yao ambayo pia itamfanya mtu akisogelea
eneo hilo alipitie mbali kwa kuona kinyaa.
“Tunaomba
vyombo vya usalama kuhakikisha watuhumiwa wote wanapatikana na silaha
nzito walizokimbia nazo maana wanaweza kuja kukivamia kijiji hiki na
kufanya unyama wa kutisha pindi vikosi vya usalama vitakapoondoka hapa,”
alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho aliyeomba hifadhi ya jina lake
gazetini.
MTENDAJI AZUNGUMZA
Afisa mtendaji wa kijiji hicho, Issa
Said Mchalaganga aliwataja watuhumiwa ambao walikuwa wakiongozwa na
kinara wao Seleman Shaban Ulatule ni pamoja na Said Mohamed Ulatule,
Ally Mohamed Ulatule, Hamis Mohamed Ulatule, Haji Seleman Ulatule na
Ally Said Ulatule.
“Hao wote walikimbia nyumba zao na baadaye kuharibiwa na wananchi kwa kuteketezwa kwa moto,” alisema Mchalaganga.
…Iliyokuwa ngome yao.
WALIOKAMATWA
“Katika msako wa vyombo vya usalama
walifanikiwa kumkamata Ramadhani Hamis Ulatule na mwenyekiti wa kijiji,
Ramadhani Mohamed Ulatule kwa ajili ya mahojiano na kwa kweli
tunampongeza Kamishna Suleiman Kova na vyombo vya usalama kwa kazi nzuri
ya kubaini kikundi hiki na kufanikiwa kupata baadhi ya silaha,” alisema
mtendaji huyo.
Baadhi ya nguo zao walizoziacha kwenye ngome hiyo.
MAISHA YAO KIJIJINI HAPO
Wananchi wa kijiji hicho waliliambia
Uwazi kuwa, watu hao ambao wanadaiwa kuwa majambazi kabla ya kubainika,
walikuwa wakiishi maisha ya usiri na wakifanya mafunzo ya kijeshi
porini.
WALIJITENGA NA SERIKALI
“Hawakupenda kushiriki na wanakijiji
katika shughuli za maendeleo, upigaji kura, uhesabuji wa watu hata
hospitali ya hapa walikuwa hawaji kupata huduma na haikujulikana
walikokuwa wakipatia matibabu,” alisema mwanakijiji mmoja.
Sehemu ya jiko.
YADAIWA KUNA ASKARI ALIYEKUWA AKIWATEMBELEA
Wananchi wa kijiji hicho walidai kuwa,
kulikuwa na askari mmoja wa Gereza la Dondwe lililopo karibu na kijiji
hicho ambaye alikuwa rafiki wa majambazi hao aliyekuwa akiwatembelea
mara kwa mara katika makazi yao.
“Huyo askari tulikuwa tunamuona akienda
huko porini mara kwa mara sasa tangu tukio litokee hajaonekana,
tunaiomba serikali imfuatilie,” alisema mkazi mwingine wa kijiji hicho.
WALIKATAA KUHESABIWA
Afisa mtendaji wa kijiji hicho
aliwaeleza waandishi wetu kuwa walimtilia shaka kiongozi wa ukoo wa
Ulatule, Seleman Shaban ambaye aliwahi kuandikiwa barua na mkuu wa
Wilaya ya Mkuranga yenye kumbukumbu namba AB/226/290/1/40 ya Agosti 31,
mwaka 2012 (nakala tunayo) ikimhoji kwa nini aliwakataza watu wa eneo
lake kuhesabiwa kwenye sensa.
“Hapo ndipo tulipotilia shaka haswa
baada ya tukio hili kutokea. Seleman alikuwa hataki kabisa kujihusisha
na shughuli za serikali. Hata wakati wa zoezi la sensa aliwakataza watu
wa eneo lake kuhesabiwa,” alisema mtendaji huyo.
WALIISHI NA RAIA WA KIGENI
Uchunguzi unaonesha kwamba watu hao
hawakupenda wananchi kutembelea wala kukatisha katika makazi yao na
kulikuwa na nyumba nyingine jirani ambazo zinadaiwa walikuwa wakiishi
watu wasio Watanzania.
SABABU YA KUVAMIA VITUO VYA POLISI NI NINI?
Inadaiwa kuwa kuna majambazi wana mpango
wa kuanzisha kikosi kikubwa kama jeshi la kupambana na dola ambayo
imewashikilia wafuasi wao katika magereza mbalimbali nchini.
Imeelezwa kwamba, utaratibu huo ulikwepo
tangu zamani na walikuwa wakipata silaha za kivita kutoka kwa wakimbizi
wa nchi jirani lakini hali hiyo ikadhibitiwa na serikali kukawa hakuna
silaha inayoingia nchini kinyume na taratibu.
WABADILI MBINU
Inasemekana kwamba baada ya kuwa na
uhaba wa silaha wakawa wanawavamia polisi katika vituo, mabenki na
popote pale wanapofanyia doria wakiwa na silaha kisha kuwapora.
Uchunguzi mwingine unaonesha kwamba
walioua katika Kituo cha Polisi Stakishari ni baadhi ya kikosi chao na
baada ya kufanya mauaji walipitia Barabara ya Nyerere na kuingia Banana
kuelekea Kitunda, Msongola, Mbande kisha kuingia katika pori la Kijiji
cha Mandikongo.
KAMISHNA KOVA ANENA
Kamishna Kova alipoulizwa kuhusu mzee
Ulatule na sakata zima la kambi hiyo ya watu hao waliotoroka alisema,
suala hilo atalizungumzia Ijumaa kwa sababu ndiyo siku aliyopanga
kuzungumza na waandishi wa habari.
“Siku hiyo ndiyo niliyopanga kuzungumza na waandishi wa habari hivyo uje na swali hilo nitalijibu,” alisema.
TUJIKUMBUSHE
Julai 12, mwaka huu watu wanaokadiriwa
16 walifanya uvamizi katika Kituo cha Polisi Stakishari na kuua polisi
wanne na raia watatu kisha kupora silaha zaidi ya 24 ambapo Kamanda wa
Kanda Maalum ya Kipolisi Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, SACP Lucas Mkondya waliapa
kuwakamata watuhumiwa hao na silaha walizoiba.
Msako wa polisi katika ngome hiyo
iliyokuwa jirani na Kijiji cha Mandikongo, polisi walifanikiwa kupata
bunduki 15 ambazo baadhi ni zile zilizoporwa katika Kituo cha
Stakishari.
Chanzo: Global Publishers
0 comments:
Post a Comment