Mkuu
wa Takukuru Mkoa wa Singida, Joshua Msuya alisema kwenye taarifa yake
kwa umma na vyombo vya habari jana kuwa Mwigulu alianza kuhojiwa na
Takukuru Wilaya ya Iramba kuanzia juzi na hadi jana alikuwa bado
anaendelea kuhojiwa dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Hata
hivyo, Mwigulu alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo alisema Takukuru ilikuwa
imeandaa kikao cha usuluhishi miongoni mwa wagombea wa vyama vyote baada
ya kuwapo kwa malalamiko kutoka miongoni mwao.
“Kuna baadhi walilalamika hadi kususia kampeni lakini tumesuluhishwa na tunaendelea na kampeni,” alisema.
Hivi
karibuni wapinzani wa Mwigulu, David Jairo, Amon Gyuda na Juma Kilimba,
walipeleka malalamiko Takukuru kuwa Mwigulu amekuwa akitoa ahadi za
kuwapa wananchi wa jimbo lake pikipiki, baiskeli na kukarabati barabara
kwa fedha zake katika kipindi cha kampeni, kitendo ambacho ni kinyume na
sheria za uchaguzi.
Msuya aliwatahadharisha wagombea
wa udiwani na ubunge mkoani hapa kutojihusisha na vitendo vya rushwa
kwenye kampeni za kura za maoni na Uchaguzi mkuu.
Alisema
watakaobainika kukiuka sheria hiyo kwa kutoa rushwa ya fedha taslimu,
madawati, vifaa vya michezo au rushwa ya aina nyingine yoyote,
watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Takukuru Tanga yaonya
Uongozi
wa Takukuru Mkoa wa Tanga, umedhamiria kuwabana wagombea ubunge na
udiwani kutokana na malalamiko kwamba baadhi wamekuwa wakitoa rushwa.
Tayari
taasisi hiyo imeanza kuwahoji baadhi ya wagombea wanaotuhumiwa huku
ikifuatilia kwa siri michakato ya uchaguzi katika vyama vyote vya siasa
pamoja na kutoa elimu ya Sheria namba 6 ya Uchaguzi ya mwaka 2010.
Kamanda
wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Aidano Ndomba alisema jana kuwa wagombea
watambue kwamba taasisi hiyo ipo kazini na itawabana wote watakaobainika
kutoa au kupokea rushwa.
“Tumeanza kuchukua hatua ya
kuwahoji na kukusanya ushahidi kwa baadhi ya wagombea ambao
wamelalamikiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa,” alisema Ndomba na
kusisitiza kuwa maofisa wa Takukuru wanafuatilia kwa siri michakato
yote.
0 comments:
Post a Comment