Dk. Joseph Chilongani aliyepigwa akiwa amezimia.
Job Ndugai.
Dodoma. Kampeni za wagombea ubunge wa Jimbo la Kongwa juzi zilikumbwa na tafrani baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kudaiwa kumchapa fimbo na baadaye kumpiga ngumi mgombea mwenzake aliyeanguka na kuzirai.
Mgombea huyo, Dk Joseph
Chilongani, ambaye hivi sasa amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Kongwa,
alipata kipigo hicho juzi saa 10.20 jioni wakati walipokuwa kwenye
mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Ugogoni wilayani Kongwa.
Kwa
kawaida, wagombea ubunge wa CCM hupelekwa pamoja na chama hicho kwenye
mikutano ya kampeni ya kila kata ambako hujieleza kwa wanachama kabla ya
siku ya kupigiwa kura.
Mpambe wa Dk Chilongani,
Shaaban Chihimba alimwambia mwandishi wetu kuwa Ndugai alimshambulia
mpinzani wake kutokana na kukasirika baada ya mgombea mwingine, Simon
Katunga kujinadi kwa kuponda utendaji wa mbunge wa sasa wa Kongwa.
“Mgombea
huyo alisema fedha zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya miradi ya
maendeleo katika halmashauri yetu zimekuwa zikiliwa hivyo akichaguliwa
atahakikisha fedha hizo zinatumika kwa mambo yaliyokusudiwa,” alidai
Chihimba.
Alisema kuwa kauli hiyo ilionekana kumkera
Ndugai, hali iliyomfanya kusimama na kutaka kwenda kumpiga mgombea
huyo, lakini viongozi wa CCM walimzuia.
“Akiwa anataka
kuketi, alimuona Dk Chilongali akirekodi tukio hilo kwa kutumia simu ya
mkononi, ndipo alipomwendea na kumpiga ngumi za usoni na fimbo kwenye
tumbo hali iliyosababisha kuanguka chini na kuzirai,” alidai.
Video
ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii, inamuonyesha Ndugai akiwa
ameshikilia fimbo mkononi huku akisema “embu na wewe usinipige,
unanipiga makamera ya nini?”
Chihimba alidai kuwa baada
ya mgombea huyo kuanguka, mkutano huo ulivurugika na wagombea wengine
wakishirikiana na baadhi ya wanachama walimchukua Dk Chilongani na
kumpeleka kabla ya kupelekwa hospitali.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema jana jioni kuwa Dk
Chilongani alifika Kituo cha Polisi Kongwa na kutoa taarifa za
kushambuliwa kichwani na tumboni kwa fimbo.
“Uchunguzi
wa tukio hilo unaendelea kwa kuwahoji watu waliokuwapo na mara baada ya
upelelezi kukamilika jalada litapelekwa kwa wakili wa Serikali kwa ajili
ya utekelezaji wa hatua stahiki za kisheria,” alisema.
Alipoulizwa
kuhusu tukio hilo, Ndugai alijibu kupitia ujumbe mfupi wa simu akisema:
“Ni kweli kumetokea mtafaruku, lakini hakuna aliyepigwa ngumi. Na
katika maisha yangu sijawahi kumpiga mtu ngumi.”
Mganga mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dk Festo Mapunda alikiri kupokewa kwa mgombea huyo juzi jioni lakini alikataa kuzungumza zaidi.
Kaimu
Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Peter Minja alikiri kutokea kwa tukio
hilo lakini akasema si kwa ukubwa huo. “Leo asubuhi (jana), tutakuwa na
kikao cha kulijadili na baadaye tutatoa taarifa... tunaendelea na
kampeni,” alisema Minja.
Hata hivyo, Minja alikataa kuthibitisha iwapo ni kweli mgombea huyo alipigwa au kukanusha kwa madai kuwa hakuwepo eneo la tukio.
“Tulishamuita
mgombea huyo na kumuonya kuhusu kujinadi kwa kukipaka matope chama na
halmashauri kwa sababu Halmashauri ya Kongwa imepata cheti safi cha
(Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali - CAG), lakini hakusikia
aliendelea.
“Tumepata taarifa ya maneno, lakini
tunasubiri ya maandishi, taarifa ya polisi na hospitali kwa kuwa
utaratibu wa chama unasema kila mwenye malalamiko awasilishe katika
vikao husika.”
Minja alisema alikwenda jana hospitalini kumuona mgonjwa huyo, lakini hakuweza kuzungumza naye.
Hata hivyo, alisema jana polisi waliwahoji baadhi ya viongozi, wanachama na wagombea kuhusu tukio hilo.
Alisema tukio hilo limesababisha mchakato wa kampeni za kura za maoni kusimama hadi leo.
“Tulikuwa
tumebakiza kata mbili za Sejeli na Kongwa Mjini ambazo zimesalia kwa
watia nia kupiga kampeni na hizi tutamalizia kesho,” alisema.
0 comments:
Post a Comment