Miaka ya hivi karibuni kulikuwa na gumzo kubwa hapa nchini na
hata nje ya nchi juu ya tiba ya kimaajabu maarufu kama ‘kikombe cha
babu.’
Tiba hiyo ya kikombe ilikuwa ikitolewa na
Mchungaji Ambilikile Mwasapile kijijini Samunge Wilaya ya Loliondo.
Taarifa za tiba hii zilienea kwa haraka nchi nzima hali iliyowafanya
wananchi wengi kila kona kuelekeza macho, masikio na mioyo yao kwenye
tiba hii.
Kutokana na uvumi wa maajabu ya kikombe cha Babu, baadhi ya watu walidiriki hata kuwatorosha wagonjwa wao hospitalini.
Wengine wakaacha matibabu na dozi walizopangiwa
hospitali kwa magonjwa mbalimbali, yakiwemo yale sugu na kuamua
kukimbilia kikombe cha babu kwa imani, kina uwezo zaidi.
Pia, ikumbukwe kwamba kikombe hakikuwa na tiba
sahihi kwani hata Serikali kupitia Wizara ya Afya na taasisi zake
zilishindwa kutoa uthibitisho wa kisayansi juu ya ukweli wa tiba ile.
Hivi sasa kumeibuka tiba ya ‘mayai ya kwale’ ambayo inavuma kila kona na
imekuwa gumzo kila mahali. Tiba hii ni ya kimaajabu kwani uvumi uliopo
ni kwamba mayai ya kwale yana uwezo wa kutibu magonjwa yote sugu.
Kasi ya kushauri wagonjwa na hata wasio wagonjwa
kutumia mayai haya badala ya kwenda hospitali kwa uchunguzi wa afya zao
inaongezeka na maelekezo yanayopatikana mitaani juu ya kutumia tiba hii
ni ya ajabu na yanatofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine.
Nilishuhudia mtu mmoja akimwelekeza mgonjwa kuwa alipaswa kuyapasua
mayai na kuyapondaponda pamoja na magamba yake na kisha ayanywe katika
hali ya ubichi. Mwingine aliambiwa ayapasue na kisha ayakoroge pamoja na
asali au maziwa kisha anywe, wengine wanaelekezwa kuyachemsha kama
mayai ya kawaida na kisha kula kiini cha ndani. Uvumi huu unaenea kwa
kasi mitaani.
Kutokana na kuvuma kwa tiba hii, mayai haya hivi
sasa yanaonekana kusakwa kila mahali na yanauzwa kati ya Sh15,000 hadi
20,000 kwa trei.
Uvumi wa tiba hii hauna tofauti na ule uliozuka
nchini juu tiba maarufu kama ‘kikombe cha Babu’. Watu wengi walikatisha
matibabu kwenye hospitali mbalimbali na kuamua kwenda Kijiji cha Samunge
kwenda kupata kikombe cha babu na kufanya kuwe na misururu mirefu ya
watu waliokesha usiku na mchana. Hii ilizusha adha kubwa hasa kutokana
na kutokuwepo na maandalizi ya vyoo hivyo watu kujisaidia ovyo
vichakani.
Adha ya safari ndefu na kukaa kwenye foleni kwa
zaidi ya siku tatu, kulifanya wenye afya mbaya kushindwa kuhimili na
hata kupoteza maisha.
Katika mazingira haya ya kuibuka tiba za
ajabuajabu ambazo hazijathibitishwa kitaalamu, ni vyema Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii ikatoa ufafanuzi.
Isisubiri hadi watu wapoteze maisha halafu ndiyo
ianze kuja na maelekezo tena yanayopingana na yale ambayo jamii
inaamini. Kuchelewa kunafanya wengi wapoteze fedha na hata kuacha tiba
sahihi na kukimbilia kitu ambacho kinavumishwa tu.
Serikali haipaswi kukaa kimya wakati watu wakiendelea kutibiana kwa vitu ambavyo havijathibitishwa kitaalamu.
Kama Serikali ingechukua hatua mapema, watu wasingepoteza maisha kupitia kikombe cha babu.
Uvumi huu wa tiba ya mayai ya kwale hauna tofauti na Kikombe cha Babu.
Katika ulimwengu huu wa utandawazi na soko huria,
ni kawaida kusikia mambo mapya yakiibuka kila kukicha, lakini kama mambo
hayo yanagusa afya zetu, hatuna budi kuwa makini na waangalifu zaidi.
0 comments:
Post a Comment