Na Imelda Mtema
WAKATI
mamilioni ya watoto duniani wanafurahi kutokana na wazazi wao kuwa na
uwezo wa kuwapeleka shule, sambamba na afya zao kuwa nzuri, hali ni
tofauti kabisa kwa mtoto Hamisi Hashimu, mkazi wa Yombo Buza jijini Dar
es Salaam ambaye kwa zaidi ya miaka sita sasa, yupo katika mateso
makubwa.
Hamis mwenye umri wa miaka 12, aliyezaliwa akiwa mzima wa afya,
alipata ulemavu ghafla wakati akicheza na watoto wenzake, lakini
jitihada za wazazi wake kumpeleka hospitali ya CCBRT ziligonga mwamba
baada ya maradhi yake ya kuvimba mguu kushindwa kutibika na hivyo
kulazimika kumrudisha nyumbani ambako hakwenda tena kutibiwa.
Akizungumza kwa uchungu, kijana huyo alisema anakumbuka siku moja
akiwa mdogo alikuwa anacheza na wenzake ndipo miguu yake ilipovunjika
kwa zaidi ya miaka sita sasa, mguu wake unaongezeka ukubwa kutokana na
kuvimba, kitu kinachomfanya ashindwe kabisa kutembea.
“Mimi mpaka sasa hivi naendelea kuteseka kwa sababu wazazi wangu
hawana uwezo kabisa wa kunisaidia kuhangaikia matibabu, kila siku mguu
unaendelea kuwa mkubwa,” alisema Hamis.
Lakini katika hali ya kusikitisha zaidi, licha ya ulemavu huo
unaompatia maumivu makubwa, bado Hamisi hulazimika kwenda Kariakoo kwa
ajili ya kuomba hela kwa wasamaria wema mwishoni mwa wiki ili aweze
kujikimu yeye na familia yao ambayo ni maskini.
“Huwa ninaenda shuleni kwa msaada wa kusukumwa kwenye baiskeli, siku
za Jumamosi na Jumapili ndiyo huelekea Kariakoo kwa ajili ya kuomba
msaada. Huu mguu ni mkubwa sana lakini kwa vile nina shida ndiyo maana
najikokota ili niweze kupata fedha ya kujikimu katika maisha yangu ya
kila siku,” alisema Hamisi.
Kama umeguswa na habari za mtoto huyu na unapenda kumsaidia, wasiliana na chumba chetu cha habari kupitia namba 0713612533.
SOURCE: GLOBAL PUBLISHERS
0 comments:
Post a Comment