Awapa `vidonge` mahasimu wanaofukuzia urais
Atoboa walivyoandaa bajeti bil.10/- za rushwa
Atoboa walivyoandaa bajeti bil.10/- za rushwa
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta
Amedai kuwa watu hao wamekula yamini ya nchi kuongozwa na mtu tajiri kupitia njia ya mkato.
Aidha, akasema kuna hatari wakati taifa
likielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani, na uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015, kuzuka kwa kundi la matajiri, ambao wengi wao ni
wakwepa kodi mashuhuri, watoroshaji wa madini ya nchi na watoroshaji wa
nyara na maliasili za nchi.
Akizungumza jana katika mahafali ya 17 ya
Shule ya Sekondari ndogo ya Agape inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la
kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Sitta alisema walafi
hao wa madaraka ni pamoja na baadhi ya viongozi waliojitajirisha kupitia
fursa za serikali kwa njia ya rushwa, mikataba mibovu, wauza madawa ya
kulevya na mawakala wa maovu.
Alisema kutokana na mwelekeo huo potofu,
amewataka wananchi wamruhusu kutumia hadhara hiyo kuzungumzia hatari
kubwa inayoikabili nchi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka
2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Katika mazingira haya inasikitisha kwamba
viongozi wengi hususani wenye uroho wa madaraka na mali wamejigeuza
kuwa wachekeshaji wa mfalme kwa kumuunga mkono, kujipendekeza na
kumsifia kiongozi wanayejua maovu yake kwa mategemeo ya kupewa fedha na
vyeo. Watu hao katika miaka miwili wamejipambanua kwa njia ya harambee
mbalimbali zinazotangazwa kwa mbwembwe na kelele katika baadhi ya
makanisa, misikiti na makundi mengine ya jamii,” alisisitiza.
Alisema kuwa hadi sasa, watu hao
wamechangia fedha zinazokadiriwa kufikia Shilingi bilioni saba huku
wakiwa wameshaandaa bajeti ya bilioni 10 kwa ajili ya rushwa ya uchaguzi
ambayo hawataki iitwe rushwa kwa sababu macho yao yamepofuka.
Alisema kuwa Watanzania hawahitaji shahada
ya siasa kubaini watu hao wakifanikiwa katika malengo yao. Alisema
uongozi utakaotokana na genge hilo hautaweza kuleta neema kwa Tanzania
kwa kuwa ngazi zote za uongozi katika himaya ya aina hiyo, zitajazwa na
watu wanaofanana katika maadili potofu.
“Masikini na wanyonge watabanwa mbavu
zaidi, matabaka ya wenye utajiri na masikini yatapanuka kiwango ambacho
hakitavumilika. Lakini pia ukusanyaji wa kodi na mapato mengine ya
serikali utadorora na kudidimiza huduma zote za jamii na kipato cha kila
Mtanzania… hatimaye misingi yetu ya umoja na usawa itabomoka na
kulitumbukiza taifa katika machafuko,” alisema.
Kuhusu hatma ya taifa kabla na baada ya
uchaguzi mkuu, Sitta alisema Watanzania wasipokuwa na mtazamo wa
kizalendo na wakasimama kwa dhati ya mioyo yao kupambana na kulikataa
jambo hilo, watawaachia watoto wao urithi ambao utatafuna vizazi hata
vizazi.
“Dhambi kubwa katika taifa lolote ni pale
mbele ya maovu, watu wema wanaamua kukaa kimya. Mimi na wewe tukiamua
hali hii ikome sasa, inawezekana na cha msingi ni kurudi nyuma na
kujipanga upya kupambana na hali hii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na
kijacho,” alisema.
Kuhusu suala la maamuzi magumu, Sitta
alisema tatizo jingine linalodhihirisha mgawanyiko wa kitabaka ni kiburi
cha baadhi ya viongozi ambao wanatamba kwamba hawawajibiki kwa vyombo
vya sheria kama wafanyavyo watu wa kawaida.
Sitta ambaye alikuwa mgeni rasmi katika
mahafali hayo yaliyoambatana na harambee ya kuchangia ujenzi wa chepo ya
Seminari hiyo, alichangia Sh. 5,750,000.
Awali akisoma risala ya wahitimu wa
seminari hiyo, Shaine Mapunda, alisema inakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwamo ukosefu wa zahanati ya shule ambayo husababisha
wanafunzi kukosa masomo kwa ajili ya kufuata matibabu hospitali ya
Marangu.
“Tunaomba kuongezewa vitabu vya michepuo
ya sanaa ili kuongeza ufaulu na ubora kwa wanafunzi wa michepuo ya
sanaa, uboreshaji wa viwanja vya michezo ufanyike kwa awamu ili kuzidi
kukuza na kuinua vipaji vya michezo mbalimbali,” alisema Shaine.
Mkuu wa Shule hiyo, Sista Elistaha Mlay,
alisema shule hiyo yenye mikondo ya kidato cha tano na cha sita yenye
jumla ya wanafunzi 548, inakabiliwa na tatizo la uhaba wa maji na umeme
hali inayosababisha kero kwa wanafunzi kujisomea. Jumla ya wanafunzi 108
wa kidato cha nne wamehitimu.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment