Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya
Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya,
amefunguka na kusema tuhuma zinazomhusisha na kumbaka na kumuambukiza
virusi vya Ukimwi msichana mwenye umri wa miaka 14, zimeasisiwa na
baadhi ya wapinzani wake wa ndani na nje ya chama chake (CCM) wenye
uwezo mdogo kisiasa.
Amesema nia ya wapinzani wake hao, ambao
hakuwataja, ni kumchafua na kudhoofisha juhudi na utendaji wake wa kila
siku, ili aonekane hafai katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Profesa Kapuya, ambaye amewahi kushika
wadhifa wa uwaziri katika wizara mbalimbali katika utawala wa serikali
za awamu ya tatu na nne, alisema hayo kupitia tamko alilolisambaza kwa
umma jana juu ya kile alichokiita uzushi unaoenezwa dhidi yake kuhusiana
na tuhuma hizo.
Alitoa tamko hilo siku moja baada ya
wakili wake, Yasin Memba, kumtetea, ikiwa ni pamoja na kutishia
kulishtaki mahakamani gazeti moja la Kiswahili litolewalo kila siku
(siyo NIPASHE) endapo halitamwomba radhi mteja wake huyo, kwa kuchapisha
tuhuma hizo bila kumpa nafasi ya kujitetea.
Profesa Kapuya alisema tuhuma hizo
zilizuka wakati akiwa jimboni akiendelea na shughuli za utekelezaji wa
ilani ya CCM, zikiwa hazina kichwa wala miguu kutokana na kutokuwa na
ukweli wowote.
“…Tuhuma kadhaa zilizoelekezwa dhidi yangu
zimeasisiwa na wanasiasa wenzangu wa ndani na nje ya chama changu ili
kudhoofisha juhudi na utendaji wangu wa kila siku,” alisema Profesa
Kapuya.
Profesa Kapuya alisema amekuwa akiitumikia
nchi kwa kipindi kirefu katika nyanja na sekta mbalimbali, kuanzia
darasani mpaka kwenye siasa.
“Kwa tamko hili, ninapenda kuwaambia kuwa
nimefedheheshwa sana na uwezo mdogo wa kisiasa unaofanywa na hawa watu
kwa kuwa dhamira yao haitatimia,” alisema Profesa Kapuya.
Alisema taarifa hizo ni za kutungwa zenye
lengo la kumdhalilisha na kumuondolea heshima yake aliyojijengea kwenye
jamii kwa kipindi kirefu.
“Waswahili wanasema dawa ya mjinga ni
kumpuuza. Na hili linajidhihirisha zaidi kwa habari hii kuandikwa na
chombo kimoja tu cha habari kinachotumiwa na chama kimoja cha siasa na
baadhi ya wanasiasa wa chama changu wasiokitakia heri chama chetu,”
alisema Profesa Kapuya.
“Chombo hiki cha habari kiliwahi kuripoti
mwaka jana kuwa kuna mitambo imeingizwa nchini inayoweza kuandika ujumbe
na kisha kuufanya uonekane umetoka kwenye namba fulani. Kwa kipindi
kile sikuwaelewa.”
“Lakini sasa ninawaelewa na nimewaona kuwa
wako sahihi na wao ndiyo waliouingiza mtambo huu na sasa wameamua
kuutumia dhidi yangu kwa kutengeneza meseji na kuzihusianisha na mimi.
Ninaamini ukweli utawaumbua muda si mrefu.”
Alisema ameijenga heshima na familia yake
kwa jamii kwa kipindi kirefu, hivyo hawezi kuruhusu kuharibiwa na
kupotezwa na watu wachache tena kwa muda mfupi.
“Hivyo, basi nimechukua hatua za kisheria
kuhakikisha heshima yangu inaendelea kulindwa na utu wangu
unaheshimiwa,” alisema Profesa Kapuya na kuongeza:
“Nimemwagiza mwanasheria wangu afungue
kesi na tayari amewashitaki watu wote wanaohusika kwenye mpango huu na
tayari wameshapokea taarifa ya kuitwa mahakamani. Nitaendelea
kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote watakaoendelea kutaka
kujipatia umaarufu ama wa kisiasa au wowote ule kwa kutumia jina langu.”
Alishauri yeyote mwenye kuona jambo hilo
lina ukweli alipeleke kwenye vyombo husika ili lishughulikiwe kwa
mujibu wa sheria na siyo kutumia vyombo vya habari kuchafuana.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment