Watuhumiwa wa mtandao wa ugaidi nchini wakiwa chini ya ulinzi katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana walipofikishwa
kusomewa mashtaka. Picha na Salim Shao.
Watu 17 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwamo za
kujihusisha na matukio ya ugaidi nchini na katika nchi jirani ya Kenya.
Pia, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya
kula njama za kuwaingiza watu nchini kushiriki katika vitendo ya ugaidi,
kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo hivyo.
Washtakiwa hao ni pamoja na Jihad Swalehe, ambaye
alisomewa mashtaka peke yake ya kula njama za kusaidia na kuwezesha
kufanyika vitendo vya kigaidi.
Washtakiwa wengine ambao pia walisomewa mashtaka
ya kula njama za kuingiza watu nchini na kushiriki vitendo vya ugaidi ni
Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed na Mohamed Yusuph.
Wengine ni Abdallah Hassan, Hussein Ally, Juma
Juma, Said Ally, Hamis Salum, Said Salum, Abubakari Mngodo, Salum Salum,
Salum Amour, Alawi Amir, Rashid Nyange na Amir Juma.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana
mchana chini ya ulinzi mkali wa polisi na kisha walipandishwa kizimbani
na kusomewa mashtaka hayo na jopo la mawakili wa serikali lililoongozwa
na wakili mwandamizi, Prosper Mwangamila. Mawaklili wengine ni George
Barasa, Mwanaamina Kombakono na Brenda Nick.
Kati ya waliopandishwa kizimbani, washtakiwa 16 ni wakazi wa Zanzibar na wengine wakazi wa Dar es Salaam.
Wakili Barasa alidai kuwa kati ya Januari, 2013 na
Juni, 2014 katika maeneo tofauti nchini washtakiwa hao walikula njama
ya kutenda kosa kinyume cha Sheria ya Ugaidi ya mwaka 2002, kwa
kuwaingiza watu ili wafanye makosa ya ugaidi.
Katika shtaka la pili, Barasa alidai kuwa katika
kipindi hicho na maeneo tofauti nchini, kwa pamoja walikubaliana
kuwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary ili kushiriki kutenda makosa
ya ugaidi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Hellen
Liwa anayesikiliza kesi hiyo aliwaeleza kuwa hawapaswi kujibu chochote
kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa
litasikilizwa na Mahakama Kuu.
Wakili Mwangamila alisema kuwa upelelezi wa kesi
hiyo bado haujakamilika na akaomba kesi hiyo itajwe tena mahakamani hapo
Jumatano ijayo, akisema kuwa wanatarajia kuwa na maombi maalumu.
Hakimu Liwa alikubaliana na ombi hilo la upande wa
mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Jumatano ijayo. Pia aliamuru
washtakiwa kurudishwa rumande.
Baada ya washtakiwa hao kumaliza kusomewa mashtaka, alipandishwa kizimbani Swalehe na kusomewa mashtaka na wakili Brenda.
Wakili Brenda alidai kuwa katika tarehe tofauti
kati ya Machi 21, 2013 na Juni 2, 2014, eneo lisilofahamika mkoani Dar
es Salaam, mshtakiwa alikula njama na watu wengine ambao hawajafikishwa
mahakamani, kutenda kosa la kusaidia kutenda vitendo vya ugaidi.
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho, mshtakiwa kwa
kujua na kwa kutumia mawasiliano ya facebook aliwasiliana na Nero
Saraiva na watu wengine kwa ajili ya kupata malighafi, fedha na ujuzi
kwa nia ya kuweka mabomu sehemu tofauti nchini Kenya ili kusababisha
majeraha na hofu kwa Wakenya.
Mshtakiwa huyo pia hakutakiwa kujibu chochote na
upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi haujakamilika. Hivyo upande
wa mashtaka uliomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa
kwa kesi hiyo..
Hakimu Liwa aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 31, 2014 itakapotajwa.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo mchana
wakiwa ndani ya mabasi mawili yaliyokuwa yakisindikizwa na magari
mawili ya Kikosi cha Kuzuia na Kutuliza Ghasia (FFU) na mengine watatu
yaliyokuwa na askari wakiwa wamevalia kiraia.
Baada ya kusomewa mashtaka, washtakiwa
waliondolewa mahakamani hapo kwa kutumia basi ndogo la magereza
wakisindikizwa na magari manne ya FFU.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment