Kisanduku cheusi cha sauti cha ndege ya MH370 ya Malaysia
Airlines iliyopotea kwa zaidi ya majuma matatu, kimeshukiwa kuwa chini
ya maji, kwa sasa zoezi la kuitafuta ndege hio limehamia chini ya maji
baada ya meli moja ya Uchina inayoshiriki kwenye zoezi hilo kubaini
ishara ya sauti ambayo huenda ikawa imetoka kwenye kisanduku cheusi cha
ndege hiyo.
Kufuatia taarifa hizo, tayari uchunguzi umeanza kuhusu eneo
ambako sauti hizo zilibainika ingawa ni sehemu tofauti kabisa na ile ya
awali ambayo ilionekana kwenye picha za Sattelite za nchi ya Australia
na China.
Kitengo maalumu kinachoratibu zoezi la utafutaji wa mabaki ya ndege
hiyo, kimesema kuwa licha ya dalili nzuri za kubaini sauti hizi, bado
hawajapata uhakika wa asilimia mia moja iwapo kile kilichogundulika
huenda kikawa ni kisanduku cheusi cha mawasilaino ya ndege hiyo.
Mkuu wa operesheni za Australia kwenye utafutaji wa ndege hiyo, Angus
Houston, amesema taarifa hizi zilizotolewa sasa zinaendelea kuchunguzwa
kwa umakini mkubwa.
Iwapo kisanduku hicho cha sauti hakitapatikana ndani ya siku mbili
zijazo huenda ikawa ngumu zaidi kukipata kwa siku zijazo kwa kuwa siku
30 zimetimia kwa kisanduku hicho kupoteza nguvu yake.
0 comments:
Post a Comment