Marehemu Muhammad Khamis Bhallo
Mwimbaji maarufu wa taarabu nchini Kenya Muhammad Khamis Bhallo amefariki dunia katika mji wa Mombasa nchini Kenya .
Marehemu Bhallo ambae amefia nyumbani kwake
akiwa na umri wa zaidi miaka sitini, kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa
na tatizo la moyo hali ambayo ilimlazimu kwenda nchini India mara
kadhaa kwa ajili ya matibabu.
Bhallo kwa zaidi ya miongo mitano
alikuwa akitunga mashairi na vile vile kuimba nyimbo za mahadhi ya
taarab na kujizolea sifa na wafuasi sio tu mjini Mombasa nchini Kenya,
bali pia hata nje ya mipaka ya Kenya zikiwemo nchi nyengine za Afrika
Mashariki na kati na hata nchi za Ulaya.
Mashabiki wake wengi walivutiwa zaidi na umahiri wake wa kutumia lafudhi ya Kiswahili cha Kimvita na kiamu.
Waliokuwa wakifuatilia kazi za Bhallo,
watakumbuka jinsi mziki wake ulivyonoga katika miaka ya themanini na
tisini pindi alipokuwa akilumbana na mpinzani wake Maulidi Juma na Bi
Shakillah kutoka Tanzania.
Akitoka katika jamii yenye mapenzi makubwa ya
filamu na nyimbo za kihindi, Bhallo aliweza kuzikonga nyoyo za wengi kwa
kutafsiri baadhi ya nyimbo za kihindi na kuziimba kwa lugha ya
Kiswahili.
Hata hivyo, kuzorota kwa hali yake ya afya
katika miaka ya hivi karibuni kutokana na tatizo la moyo, kulimtoa
kabisa katika ulingo wa muziki na kusababisha kuzagaa kwa uvumi kwamba
Bhallo alikwisha kufa siku nyingi, taarifa ambazo hazikuwa za ukweli
kwani Bhallo amefariki dunia Jumapili na kuzikwa siku hiyo hiyo huko
mjini Mombasa.
0 comments:
Post a Comment