Kaburi la aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Daudi Ballali
lililopo katika makaburi ya Gate of Heaven nchini Marekani. Gharama ya
kumzika mtu katika eneo hilo ni Sh7.9 milioni. Picha na Neville Meena
Eneo alilozikwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT),
Daudi Ballali katika makaburi ya Gate of Heaven, Maryland nchini
Marekani liliigharimu familia yake kiasi cha Dola 4,810 za Kimarekani
(sawa na zaidi ya Sh8 milioni).
Ballali aliyefariki dunia Mei 16, 2008 nyumbani
kwake Washington DC, alizikwa katika eneo namba 6, ploti ya 241, safu
namba 17 katika makaburi hayo yaliyopo katika anwani ya 13801, Georgia
Avenue Silva Spring, MD 20906.
Safu hiyo namba 17 aliyozikwa Ballali imepewa jina la Jesus in the Temple, ikimaanisha ‘Yesu Hekaluni’.
Gavana huyo wa zamani aliondoka nchini kwenda
Marekani kikazi, akiacha mjadala mkubwa juu ya wizi wa fedha kutoka
kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa), huku jina lake
likitajwa kuwa alihusika kuidhinisha fedha hizo kwa makampuni 22 kinyume
cha taratibu.
Aliachishwa kazi baada ya ukaguzi wa kampuni ya
Ernst and Young kubaini ufisadi mkubwa kwenye taasisi hiyo kuu ya fedha
nchini. Muda mfupi baadaye Ballali alifariki, kifo ambacho kilizua
mjadala kutokana na mazingira yake.
Kwa mujibu wa ramani, ambayo gazeti hili liliipata
kutoka ofisi iliyopo kwenye makaburi hayo, aina ya kaburi la Balalli
inaangukia katika eneo yalipo makaburi yenye mnara ambayo yanagharimu
kiasi hicho cha fedha.
Pia aina hiyo ya eneo inaruhusu kuwapo kwa
makaburi pacha iwapo mmiliki wa eneo husika atahitaji, lakini kwa
gharama ambazo ni maradufu. Hata hivyo haikufahamika mara moja iwapo
familia ya Ballali imechukua sehemu ya pili.
Idadi kubwa ya Wamarekani wanamiliki maeneo ambayo
tayari wameyaandaa kwa ajili ya maziko baada ya kufariki dunia na
maeneo hayo hulipiwa ada kila mwaka kwa gharama ambayo huzingatia
matunzo na eneo yalipo makaburi hayo.
Mtanzania Safari Ohumai ambaye ni mkazi wa
Greenbelt, nje kidogo ya Washington aliiambia Mwananchi nyumbani kwake
kuwa: “Kufa hapa Marekani ni gharama kubwa. Lazima ulipie eneo ambalo
umeliandaa kwa ajili ya maziko yako utakapofariki dunia”.
Taratibu za mazishi
Mazishi ya Ballali yalikuwa ya faragha kwani mwili
wake haukuonyeshwa hadharani, hivyo Watanzania wengi wanaoishi katika
miji ya Washington DC, Maryland na Virginia (DMV), hawakuweza kushiriki.
Familia ya Gavana iliyopo Marekani na Tanzania,
kwa nyakati tofauti ilimwambia mwanandishi wa Mwananchi kwamba usiri wa
taratibu za mazishi, ulikuwa ni utekelezaji wa matakwa ya Ballali ambaye
kabla ya kifo chake aliagiza maiti yake isionyeshwe hadharani isipokuwa
kwa ndugu wa karibu pekee.
Baadhi ya Watanzania ambao wameishi katika miji hiyo kwa miaka
kati ya 15 na 20, walionekana ama kutomfahamu kabisa Ballali au
kutofahamu alikokuwa akiishi, kifo na mazishi yake, tofauti na hapa
nchini.
Ballali alifariki dunia akiwa nyumbani kwake
Washington DC, Mei 16, 2008 baada ya kuugua kwa miezi kumi na baadaye
kuzikwa Mei 23, tukio lililowahusisha ndugu wa karibu.
Usiri uliogubika kifo na mchakato wa mazishi yake
ndiyo chachu ya kuwapo kwa hisia kwamba kiongozi huyo hakufa, bali
alifichwa sehemu mojawapo ya Marekani kutokana na kile kinachodaiwa
kwamba alikuwa na siri nyingi kuhusu kashfa ya fedha zilizochotwa kwenye
Akaunti ya Epa.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika
(Voa), Mwamoyo Hamza alisema: “Siyo rahisi kwa wana DMV wengi wa sasa
kumfahamu Ballali, kwa sababu mbalimbali, lakini kubwa ni kwamba yeye
alifika hapa (Marekani) siku nyingi sana.”
“Kwa mfano huu umoja wa sasa wa Watanzania
wanaoishi DMV, Ballali hakuwa mwanachama, kwa hiyo naweza kusema
alifahamika zaidi kwa wenzake wenye umri sawa na yeye waliokwenda
Marekani miaka ya 60,” alisema Mwamoyo.
Kuhusu uamuzi huo, Mwamoyo alisema nchini Marekani
msiba ni suala linalohusu familia zaidi na kwamba haikuwa ajabu kama
familia ya Ballali iliamua kuomboleza kifamilia.
“Hapa ndiyo utamaduni wao, mazishi au masuala ya
misiba huwa ni ya kifamilia kwa hiyo haikuwa ajabu kwa familia ya
Ballali kufanya taratibu zao kwa jinsi walivyoona inafaa,” alisema
Mwamoyo ambaye pia alibainisha kuwa Voa walifuatilia taarifa za kifo
chake na walizitangaza katika taarifa zao.
Watanzania wengine
Mtanzania Harriet Shangarai anayeishi Maryland kwa
zaidi ya miaka kumi sasa, alisema hamfahamu Ballali na wala hajawahi
kusikia taarifa zake. “Huyo ndiyo nani? Mie simfahamu kwa kweli,”alisema
Harriett alipozungumza na Mwananchi, eneo la Silver Spring.
Mtanzania mwigine, Abou Shatri, ambaye pia ni
mkazi wa Maryland ambaye pamoja na kusihi nchini Marekani takriban miaka
20, hakuwahi kusikia taarifa zozote zinazomuhusu Ballali na wala
hamfahamu.
“Ndugu yangu nisikudanganye, huyo mtu mimi
simfahamu kabisa kwani huyo ndo nani?” alihoji Shatri na alipoelezwa
kwamba alikuwa Gavana wa BoT ambaye pia aliishi Maryland na baadaye
Washington, alisema hamfahamu kabisa.
Mbelwa Bandiwo, ambaye pia ni mkazi wa eneo la
DMV, alisema anamfahamu Ballali lakini hakufuatilia msiba wake kwa
sababu mazishi yalikuwa ni ya kifamilia.
“Hilo ni jambo la kawaida hapa Marekani. Mara nyingi mazishi ama
shughuli za misiba huwa ni ya kifamilia zaidi na marafiki wa karibu.
Kwa hiyo ndiyo maana Watanzania wengi wa maeneo haya watakwambia kwamba
hawakushiriki kwenye huo msiba,” alisema Bandiwo.
“Lakini jambo jingine ni kwamba huu ni utamaduni
tuliouzoea kwa hiyo ni jambo la kawaida kwamba katika familia nyingine
hata makaburini huwa hawaendi kabisa kuzika, badala yake kazi hiyo
hufanywa na kampuni zilizosajiliwa kwa ajili hiyo na baadaye labda
Jumamosi au Jumapili ndipo familia huenda kuona mahali alipozikwa ndugu
yao na kuweka maua”.
Itaendelea.....
Chanzo: Mwananchi
Itaendelea.....
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment