HUKU Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikijipanga kuweka
safu mpya ya uongozi kitaifa ifikapo Agosti 31, imebainika kuwa
mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya chama hicho chini ya
Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa.
Kwamba viongozi hao ni mwiba mkali kwa wapinzani wa chama hicho, hasa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015, ndiyo maana
wamekuwa wakisakamwa kila mara katika wiki za hivi karibuni, Tanzania
Daima Jumatano limedokezwa.
CHADEMA ndicho chama pekee cha upinzani nchini ambacho tangu kurejea
kwa mfumo wa vyama vingi kinazidi kuimarika hatua kwa hatua kila wakati
licha ya kuwapo taarifa za CCM kujaribu kukisambaratisha kwa kutumia
vyombo vya dola, na wasaliti wa ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, jitihada hizo za CCM zimekuwa zinagonga mwamba kwa sababu ya uthabiti wa uongozi wa sasa wa CHADEMA.
Tangu kuanzishwa mwaka 1992, CHADEMA imeongozwa na wenyeviti watatu;
Edwin Mtei, Bob Makani na Mbowe ambaye alishika wadhifa huo mwaka 2004
na kufanikiwa kukipa chama hicho haiba na sura mpya, na kukieneza katika
kila kona ya nchi akishirikiana na Dk. Slaa na viongozi wengine.
Rekodi za CHADEMA zinaonyesha kuwa katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa
mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, kiliunga mkono mgombea urais wa
NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema, lakini kilipata viti vinne vya ubunge na
madiwani 42. NCCR – Mageuzi ilipata wabunge 27.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, CHADEMA kiliunga mkono mgombea
urais wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, lakini kikapata wabunge watano na
madiwani 75.
Kasi ya CHADEMA ilizidi kuongezeka katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2005, ambapo kwa mara ya kwanza kiliweka mgombea urais, Freeman Mbowe,
kikapata msisimko mkubwa kitaifa na kupata wabunge 11 na madiwani 103.
Kitisho kwa CCM ulikuwa uchaguzi mkuu wa 2010, ambapo Dk. Slaa
aligombea urais na kukiwezesha chama hicho kupata wabunge 49 na madiwani
467.
Chama hicho kina wenyeviti katika vijiji, mitaa na vitongoji vingi
nchi nzima huku pia kikiwa na mameya na wenyeviti katika halmashauri na
majiji mbalimbali.
Ni dhahiri kasi ya CHADEMA inazorotesha uhai wa CCM.
Na kama CCM ilivyofanikiwa kusambaratisha vyama vingine vya upinzani
kama NCCR-Mageuzi, CUF na TLP, imeendelea kutumia mbinu hizo hizo dhidi
ya CHADEMA, lakini zimegonga mwamba.
CHADEMA kimepitia kwenye dhoruba ya propaganda za udini, ukabila,
ugaidi na sasa mkakati umehamia kwenye usaliti wa kupandikiziwa mamluki
ndani ya chama ili kuwachafua Mbowe na Dk. Slaa waachie ngazi.
Tukio la karibuni lilikuwa la kutimuliwa kwa viongozi kadhaa wa chama
hicho waliobainika kutumiwa na CCM kusambaza nyaraka za mapinduzi ya
viongozi kupitia mitandao ya kijamii, mkakati ambao nao umeshindikana.
Na katika kutegua kitendawili cha uchaguzi mkuu wa chama hicho, ambao
baadhi ya wasaliti walikuwa wakidai viongozi walivunja katiba kwa
kujiongezea muda, Katibu Mkuu, Dk. Slaa ameweka bayana ratiba nzima.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Dk. Slaa alisema
uchanguzi wa taifa wa kumchagua mwenyekiti na makamu wake wa Bara na
Visiwani utafanyika Agosti 31.
Uchaguzi huo ambao wanachama wengi wameonyesha nia ya kumtaka Mbowe
agombee tena nafasi hiyo, utakwenda sambamba na chaguzi nyingine za
ngazi mbalimbali katika chama.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, baada ya kukamilisha chaguzi ndani ya chama
kuanzia ngazi za chini, sasa wanaelekea katika uchaguzi mkuu.
Alisema katika ngazi ya vitongoji wamepata viongozi 196,000 kati ya
256,000 na wataendelea kuchagua viongozi hadi idadi itakapotimia, na
kwamba ngazi ya matawi tayari wana viongozi 16,000 kwa awamu ya kwanza.
Dk. Slaa alisema katika awamu ya pili uchaguzi utaanza Agosti 3 hadi
8, na kuendelea katika ngazi ya majimbo pamoja na mikoa ukifuatiwa na
mkutano wa siku saba.
Alisema kuwa Agosti 27, utafanyika uchaguzi wa viongozi wa Baraza la
Vijana (Bavicha) na Baraza la Wazee, ambapo Agosti 28 ni uchaguzi wa
Baraza la Wanawake (Bawacha) huku Agosti 29 ni uchaguzi wa Kamati Kuu ya
kwanza.
Agosti 30, Baraza Kuu jipya litakutana ambalo litawezesha Mkutano Mkuu wa Agosti 31 pamoja na kuwapata mwenyekiti na makamu.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, Septemba mosi, Baraza Kuu litakutana kuchagua
katibu mkuu na manaibu wawili, na Septemba 2 ni Mkutano wa Kamati Kuu.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment