MAKACHERO wa Jeshi la Polisi Zanzibar, wamefanikiwa kumtia mbaroni
mmoja wa washukiwa wa matukio ya tindikali visiwani hapa, Alawi
Mohammed Silima (25), mkazi wa Fuoni Melinne, nje kidogo ya mji wa
Zanzibar.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar,
Inspekta Mohammed Mhina, mtuhumiwa anahusishwa na tukio la kummwagia
tindikali Sheha wa Shehia ya Tomondo mjini Zanzibar, Mohammed Omar
Saidi Kidevu kabla ya kutoweka.
Inspekta Mhina alisema mtuhumiwa huyo ambaye kwa muda mrefu alikuwa
akisakwa na polisi kuhusu tukio hilo, alikamatwa juzi usiku akiwa
mafichoni katika eneo la Fuoni, baada ya taarifa za kiintelijensia
kubaini kuwepo kwake.
Alisema bado makachero hao wanaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo kwa
lengo la kuubaini mtandao mzima wa matukio mbalimbali, yakiwemo ya
tindikali yaliyotokea siku za nyuma visiwani hapa.
Alibainisha kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na taarifa
za siri za raia wema, ambapo Jeshi la Polisi lilikuwa likiendelea na
upelelezi wa chini kwa chini wa kumbaini mtuhumiwa na mahali
alipojificha.
Baadhi ya wananchi wa Zanzibar, wamepongeza kukamatwa kwa mtuhumiwa
huyo na kuliomba Jeshi la Polisi kuendelea na juhudi zake za kuwasaka
watuhumiwa wengine wanaohusika katika matukio mengine kama hayo siku za
nyuma visiwani hapa.
Tukio la kumwagiwa tindikali kwa sheha huyo, lilitokea majira ya saa
2:45 usiku Mei 22 mwaka jana, wakati alipokuwa akirudi nyumbani akitoka
kuchota maji nyumba jirani. Alijeruhiwa vibaya mgongoni, kifuani,
sikio na jicho la upande wa kulia.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment