Mkazi wa Kijiji la Luganga, Wilaya ya Mufindi, Iringa,
alikozaliwa Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi
Ballali analazimika kutumia saa 32 kufika katika kaburi la kiongozi huyo
lililopo eneo la Silver Spring, Maryland nchini Marekani.
Ndugu wa Ballali (pichani) wanaweza kutaka kwenda
kuona kaburi la ndugu yao, kutokana na ukweli kwamba wengi wao
hawakuwahi kupata fursa ya kumzika Gavana huyo ambaye alikuwa kiongozi
wa juu kabisa wa taasisi kubwa inayosimamia masuala ya fedha na uchumi
wa nchi.
Mwandishi wa gazeti hili alisafiri kwa saa 24
kutoka Dar es Salaam hadi Washington, Marekani ambako alithibitisha pasi
na shaka kwamba Ballali alizikwa Mei 21, 2008 katika makaburi ya Gate
of Heaven, baada ya kufariki dunia akiwa nyumbani kwake Maryland, Mei
16, mwaka huo.
Safari hiyo ya siku kumi, ilianza Alhamisi Juni
26, 2014 hadi Jumapili, Julai 6. Mwandishi wa habari hizi aliligundua
kaburi hilo baada ya kwenda makaburi ya Gate of Heaven kwa siku tatu
mfululizo.
Siku ya kwanza, mwenyeji wa mwandishi ambaye jina
lake tunalihifadhi kwa sasa alimfikisha katika makaburi hayo, lakini
kaburi la Ballali halikuonekana na hata mwandishi alipokwenda siku ya
pili peke yake, kaburi hilo pia halikuonekana kwa kutokana na ukubwa wa
eneo hilo.
Siku ya tatu, Mwandishi wa Mwananchi alilazimika
kuomba msaada wa Ofisi ya Makaburi ya Gate of Heaven, ambayo ilimsadia
kuonyesha eneo lilipo kaburi hilo, hivyo kuwezesha kupata picha zake.
Kaburi lake liko katika msitari wa mwisho kabisa
na Ukanda wa Kijani wa miti iliyozunguka makaburi ya Gate of Heaven,
likiwa limeandikwa jina la kiongozi huyo, pamoja na maneno ya Kiingereza
yanayosomeka “When the heart weep for what it has lost, the soul
rejoices for what it has found”.
Maana ya maneno hayo ni kwamba “wakati moyo
ukiomboleza kwa kile kilichopotea, roho hufurahi kwa kile
kilichopatikana”. Kaburi hili limezungukwa na makaburi mengine kadhaa
ambayo si ya Watanzania, kwani kwa haraka kutokana na mazingira
yalivyokuwa, Mwandishi wa Mwananchi hakuweza kuona kaburi jingine lenye
majina yenye asili au kuwa na mwelekeo wa asili ya Tanzania.
Uthibitisho huu ni tofauti na hekaya za miaka
nenda rudi zilizogubika kifo cha kiongozi huyo, ambaye tangu alipoondoka
nchini kwenda Marekani Agosti 2007, hakuwahi kurejea na badala yake
zilisikika taarifa za kuugua kwake, kifo chake na baadaye mazishi yake
yaliyokuwa ya siri kubwa yakiwahusisha ndugu wa karibu pekee.
Kutokana na mazingira hayo, kumekuwapo na uvumi
kwamba Ballali hakufa na pengine amefichwa kusikojulikana, madai
yanayochagizwa na mtu aliyejitokeza katika mitandao wa kijamii ya
Twitter na facebook, akidai kwamba yeye ni Ballali na kwamba hajafa,
huku akisisitiza kuwa wakati ukiwadia ukweli utafahamika.
Mtu huyo asiyefahamika hadi sasa alianza
kujitokeza Twitter, Oktoba Mosi, 2012 pale aliposema “Nitakutana na Rais
Kikwete (Jakaya) na ujumbe wake wiki hii hapa Marekani”. Mtu huyo
alidai kwamba alikuja nchini Tanzania na kukaa karibu na Hoteli ya Hyatt
Kempinski Kilimanjaro na baadaye kuondoka ghafla kwa kile alichokiita
sababu za kiusalama.
Novemba 13 mwaka huo alituma ujumbe akisema:“In
Dar es Salaam, Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kempinski Kilimanjaro
Hotel. Feels good to be close to my former office, BoT,” akimaanisha
kwamba niko Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, najisikia vizuri kuwa
karibu na ofisi yangu ya zamani BoT.
Mtu huyo ambaye sasa tunaweza kuthibitisha kuwa ni feki amekuwa
akiendelea kutuma ujumbe akijitambulisha kwa jina hilo la Ballali.
Ballali alifariki dunia kama ilivyotagazwa, lakini
ilikuwaje akaenda safarini Washington, ugonjwa wake na hata kifo chake
kilikuwaje? Je ndugu zake wanasemaje, safari ya kwenda Marekani
ilikuwaje? Fuatilia mfululizo wa habari hii
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment