WALIMU
na wanafunzi wa shule za sekondari za Ibiri na Ilongalulu za mkoani
Tabora, wamefurahi baada ya kuwezeshwa kupata mafunzo kupitia mtandao
kutokana na ushirikiano wa Kampuni ya Airtel Tanzania na mradi wa
Millennium Village.
Shule hizo zimefaidika kupitia mradi wa Connect to Learn
unaowawezesha wakufunzi na wanafunzi waliopo nje ya nchi kuwasiliana na
kupata mafunzo kwa mtandao ambapo Airtel kupitia huduma yake ya intaneti
ya 3.5G inaziwezesha shule hizo kuunganishwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa Shule ya Sekondari
Lolangulu, Cleophas Bugombo, alisema wanashukuru kwa mpango huo wa
kibunifu unaowezesha kupata nyenzo za ziada za kufundishia.
Alisema kupitia mpango huo wanapata nafasi ya kuwaunganisha wanafunzi
wao na wanafunzi wengine kutoka maeneo mbalimbali ya ulimwengu kwa njia
ya Skype ambapo wanapata nafasi ya kujifunza na kupeana uzoefu.
“Hiki ni kitu muhimu katika kuongeza upeo wa kufahamu, kwani kuna
mambo mengi wanayoweza kuyaona ulimwenguni kuliko wanavyoona sasa kila
siku,” alisema.
Chiku Ramadhani, mwanafunzi wa Sekondari ya Ibigiri, alisema
anafurahi kuunganishwa na wanafunzi waliopo Marekani kupitia Skype na
kuweza kushirikiana na kusoma pamoja.
“Ni ajabu kuona teknolojia inavyotuwezesha sisi watoto wa vijijini
kuona mambo ya nje na kujifunza kutoka kwa mataifa mengine, nafurahia
sana na ni mengi mazuri ya kujifunza kupitia mtandao,” alisema.
Mkurugenzi wa Mradi wa Millennium Village, Dk. Gerson Nyadzi, alisema
kwa kuwekeza kwenye teknolojia ya 3.5G na kutoa huduma ya intaneti ya
vifurushi vya mwezi bila gharama yoyote, Airtel imewezesha mradi wa
Connect to Learn kuwaunganisha mamia ya wanafunzi kutoka shule zilizo na
uhaba wa vifaa zilizoko vijijini.
“Ni matumaini yetu kuwa teknolojia hii itakuwa chachu ya maendeleo na
kutoa mwanya kwa wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao,” alisema.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment