LATEST POSTS

Wednesday, July 16, 2014

‘Tunaumizwa na madai kwamba Ballali yupo hai’

Baadhi ya wanafamilia wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Ballali wamesema taarifa zilizozagaa kwamba ndugu yao huyo yupo hai hadi sasa, zinawaumiza na kuwakumbusha uchungu walioupata wakati wa kifo chake.
Wakizungumza na Mwandishi wa gazeti hili hapa nchini na Marekani, baadhi ya ndugu hao walisema hakuna shaka yoyote kwamba ndugu yao alifariki dunia na kwamba pengine suala linalowatatiza ni sababu za kifo chake pekee.Miaka sita tangu Ballali alipofariki dunia, kulikuwa na hoja nyingi kuhusu kifo chake hasa kutokana na ukweli kwamba, mbali na mazishi yake kufanywa kwa siri yakiwahusisha wanafamilia pekee, hata kaburi lake halikuwahi kuonekana pahali popote.
Hata hivyo, kati ya Jumamosi iliyopita mpaka jana, mara kadhaa gazeti hili lilichapisha picha za kaburi hilo ambazo zilipigwa na mwandishi aliyefika katika makaburi ya Gate of Heaven, eneo la Silver Spring, Maryland, Marekani ambako alizikwa Mei 23, 2008.
Paschal Ballali ambaye ni mdogo wa marehemu, alisema kutajwa kila mara kwa jina la kaka yao na madai kwamba bado anaishi ni mambo ambayo yanawaumiza kama wanafamilia kwani wao wanaamini kwamba ndugu yao alifariki dunia na alizikwa Marekani na kwamba jambo wasilolifahamu kama familia ni sababu za kifo chake.
“Tunaumia sana na hivi tunakaribia kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, tunahofu kwamba wanasiasa wanaweza kuamua kutumia jina lake kisiasa, wao hawafahamu madhara wanayosababisha kwetu maana wanaweza kutamka neno moja, sisi katika familia likatuumiza mwaka mzima,” alisema Paschal akiwa kijijini kwake Luganga, Mufindi mkoani Iringa na kuongeza:
“Kweli tunajisikia vibaya sana, maana mtu alifariki na akazikwa, halafu leo hii mnaambiwa mara yupo hai au amefichwa mahali fulani, kweli inaumiza sana, mimi naomba watuache maana tusingependa kuendelea kuishi katika hali hii.”
Ndugu mwingine wa Gavana huyo, Osward Ballali ambaye anaishi Dar es Salaam, alisema: “Wamwache kaka yetu apumzike na waiache familia yetu nayo ipumzike maana sisi tuna uhakika kwamba alifariki dunia, sasa hao wanaosema yuko hai pengine watusaidie kujua yuko wapi.”
Oswald alisema pamoja na kwamba yeye binafsi hakuhudhuria mazishi, lakini dada zake wawili walikuwapo na kushiriki katika mchakato mzima wa safari ya mwisho ya Ballali, hivyo yeye hana shaka kwamba kaka yake alifariki na siyo vinginevyo.
Akizungumza na Mwandishi wa gazeti hili, dada wa marehemu Ballali, Margaret Mpango anayeishi Kigoma alisema: “Tanzania imegeuka kuwa nchi ya uzushi, inakuwaje mtu anazusha tu kwamba Ballali yupo hai, kama kuna mtu anajua aliko basi amlete maana sisi tungefurahi kuwa naye.”
“Akili ya kawaida inakutuma mtu ujiulize kwamba mtu yuko hai, halafu eti anaishi Marekani, mke wake, watoto wake na sisi ndugu zake hatufahamu, hilo linawezekanaje? Mimi nasema watuache, yaliyosemwa kuhusu familia yetu yanatosha,” alisema Margaret na kuongeza: “Mnaposema yuko hai, mmemwona wapi? Huyo mwingine tunasikia eti amejitokeza kwenye twitter na amekuwa akiendelea kudai kwamba yeye ni Ballali yuko hai, kama ni kweli basi awasiliane na sisi ambao ni ndugu zake, lakini mimi nilishiriki mazishi na nilishuhudia mwili wa kaka yangu ukizikwa.”
Margaret mbali na kushiriki mazishi hayo, mumewe ambaye ni Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Kasulu, Kigoma, Dk Gerald Mpango alishirikiana na baadhi ya Makasisi wa Kanisa la Mtakatifu Stephen, lililopo Washington DC kuongoza ibada ya mazishi ya Ballali.

Chanzo: Mwananchi

0 comments: