Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amesema endapo itatokea
kwa namna yoyote akafa, mhusika mkuu wa kifo chake itakuwa “Serikali ya
CCM” na ameagiza kuwa kamwe wasifike kwenye msiba wake wala kutoa
rambirambi.
Wakati Kafulila akitoa tuhuma hizo nzito mkoani
Kigoma, Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema) kimemtaka Rais
Jakaya Kikwete kutangaza zabuni kwa ajili ya kupata kampuni ya kimataifa
kwa ajili ya kukagua akaunti ya escrow iliyofunguliwa kwa ajili ya
kuhifadhi fedha kusubiri kumalizika kwa mgogoro ulio mahakamani baina ya
Shirika la Umeme (Tanesco) na kampuni binafsi ya kufua nishati hiyo ya
IPTL.
Kauli ya Kafulila inatokana na mbunge huyo wa
tiketi ya NCCR-Mageuzi kudai kutishiwa maisha na Mwanasheria Mkuu Jaji
Federick Werema. Jaji Werema anadaiwa kutoa vitisho hivyo baada ya
Kafulila kumtaja ndani ya Bunge kama mmoja wa wahusika katika kashfa ya
wizi wa Sh200 bilioni kutoka katika akaunti hiyo ya Tegeta Escrow
iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania.
Akihutubia mkutano wa hadhara kwa nyakati tofauti
katika Uwanja wa Mwanga Center na Cine Atlas mjini Kigoma, Kafulila
alisema amejitolea maisha yake kupigania rasilimali za taifa ambazo
zinachotwa na genge la watu wachache kwa masilahi yao binafsi na
kuwaacha Watanzania wengi wakiishi katika lindi la umaskini na huduma
mbovu za kijamii.
“Mbunge wenu (Kafulila) nilisema ndani ya Bunge
kwamba Sh200 bilioni zimeibwa katika akaunti ya escrow na waliozichota
wapo na wanajulikana, lakini Serikali haitaki kuwachukulia hatua. Mbaya
zaidi hata Spika wa Bunge (Anne Makinda) amekataa kuunda Kamati teule ya
Bunge ili ichunguze kashfa hiyo,” alisema Kafulila.
“Matokeo yake nimeanza kutishiwa maisha yangu na
Serikali imekaa kimya licha ya kuliwasilisha jambo hilo kwenye vyombo
vya dola. Naomba nichukue nafasi hii kutoa tamko kwamba wakati wowote
nikifa, mhusika mkuu wa kifo changu ni Serikali ya CCM na kamwe sitaki
wafike kwenye mazishi na hata msiba wangu.”
Pia, alimlaumu Mkuu wa Polisi (IGP), Ernest Mangu
kwa kukalia kimya jambo hilo, akisema amepoteza imani na jeshi hilo kwa
vile linaonekana kumuogopa Jaji Werema kwa kushindwa hata kumuhoji.
“Nilipeleka malalamiko yangu kwa IGP, lakini hadi
hivi leo (jana) ninapoongea hapa hajawahi hata kuitwa polisi atoe
maelezo. Hili ni janga kwa utawala wa kisheria nchini. Jambo la
kushangaza zaidi ni kuwa tulitarajia mtu mwenye hadhi ya jaji awe mtii
na mtekelezaji wa sheria za nchi, lakini inapofikia jaji kutishia
kuniua, hapo ujue mfumo wa sheria ni legelege na hauna nguvu kwa baadhi
ya watu.”
Wakati wa Bunge la Bajeti, Kafulila alisema fedha
hizo zilipitishiwa kwenye benki moja na kuchukuliwa zikiwa taslimu,
tofauti na sheria za benki na kuwatuhumu vigogo wa Serikali kuhusika na
akiomba Bunge liunde kamati huru kuchunguza tuhuma hizo.
Wakati Bunge hilo likiendelea, Jaji Werema
alitumia neno “tumbili” kumhusisha na Kafulila na ndipo mbunge huyo wa
Kigoma alipomwita mwizi na kusababisha tafrani ambayo iliepushwa na
wabunge wengine waliomzuia Jaji Werema asimkaribie Kafulila.
Inataarifiwa kuwa akaunti hiyo ilikuwa na takriban
Dola 250 milioni za Marekani, lakini baada ya kikao cha pamoja kati ya
Kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP), Tanesco na Wizara ya
Nishati ilikubaliwa kuwa Dola 122 milioni kati ya hizo zitolewe kutoka
akaunti hiyo na kulipwa PAP ambayo ni mmiliki mpya wa IPTL.
Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutoa tenda kwa kampuni za
ukaguzi wa hesabu za kimataifa ili kufanya uchunguzi. “Serikali iache
bla bla, itoe tamko kwa fedha hizo zaidi ya Sh400 bilioni. Wanasema siyo
fedha za serikali, wakati nyaraka zote hizi nilizonazo zinaonyesha kuwa
ni za serikali.
Huu ni ufisadi tu kama ulivyokuwa wa EPA,” alisema akirejea kashfa kashfa nyingine ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni iliyokuwa Benki Kuu.
Huu ni ufisadi tu kama ulivyokuwa wa EPA,” alisema akirejea kashfa kashfa nyingine ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni iliyokuwa Benki Kuu.
Katika kashfa hiyo, kampuni 22 zilichota fedha kinyume na utaratibu.
“Rais Kikwete aitishe tenda kwa kampuni za ukaguzi
wa hesabu za kimataifa ili tujue ukweli. Hizo fedha ni zetu, ni kodi ya
wananchi.”
Alionyesha kushangazwa na kitendo cha Kampuni ya
IPTL kumshtaki Kafulila wakati suala lenyewe bado lilikuwa mikononi mwa
Bunge, ambalo limeiagiza Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za
Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
ilichunguze.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment