Wakazi wa viunga vya Donetsk wakitazama masalia ya ndege ya Malaysian
Airlines iliyoanguka.
Ndege ya Shirika la Malasyia ilitunguliwa mashariki mwa
Ukraine na wanajeshi wanaoiunga mkono Russia na kuua watu 295 waliokuwa
ndani, ofisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ukraine alisema.
Ndege hiyo ‘Malaysia Airlines’ ilikuwa ikisafiri
kutoka Amsterdam kwenda Kuala Lumpur na ilikuwa juu umbali wa futi
33,000 kutoka usawa wa bahari wakati ikitunguliwa.
Ikizidisha hali ya wasiwasi katika mzozo baina ya
Mashariki na Magharibi ukihusisha Kiev na Moscow, ofisa huyo alilaumu
“magaidi” kuwa walitumia kombora la kutokea ardhini kutekeleza
shambulizi hilo na waziri mkuu wa Ukraine alizungumzia kutunguliwa kwa
ndege hiyo kuwa ni “janga”.
Mwandishi wa Reuters aliona mabaki ya ndege hiyo
yakiungua pamoja na miili ya watu ikiwa ardhini kwenye kijiji cha
Grabovo, karibu kilomita 40 kutoka mpaka wa Russia katika eneo ambalo
waasi wanaoiunga mkono Russia wamekuwa wakifanya shughuli zao na wamedai
kutungua ndege nyingine.
Ndege hiyo, Boeing 777 ilidondoka karibu na jiji
la Donetsk, sehemu ambayo ni ngome ya waasi hao, ofisa huyo wa Wizara ya
Mambo ya Ndani, Anton Gerashchenko alisema kwenye ukurasa wake wa
facebook, akiongeza kuwa ndege hiyo ilitunguliwa na kombora aina ya Buk
na watu aliowaita kuwa “magaidi” – neno ambalo serikali ya Ukraine
hutumia kumaanisha wanajeshi wanaotaka kuunganisha nchi ya Ukraine na
Russia.
Watu waliokuwamo kwenye ndege hiyo ni abiria 280 na wafanyakazi 15.
Shirika la Ndege la Malaysia lilisema kwenye
ukurasa wa Twitter kwamba ilipoteza mawasiliano na ndege hiyo namba
MH-17 kutokea Amsterdam. “Sehemu ya mwisho iliyojulikana ilikuwa kwenye
anga ya Ukraine,” ilisema taarifa ya shirika hilo.
Msemaji wa ikulu ya Marekani, Josh Earnest alisema
ofisi hiyo ina taarifa ya ajali hiyo lakini “hakuwa tayari kuthibitisha
“ taarifa zaidi.
Rais Barack Obama ameshataarifiwa na ameagiza timu yake ya usalama wa taifa kuwa karibu na mamlaka za Ukraine, alisema Earnest.
Obama alipuuza swali lililoulizwa kwa kupaza sauti
kuhusu taarifa hizo wakati akiwa njiani kutoka ofisini kwake kwenda
ofisi ya jeshi.
Kutunguliwa kwa ndege hiyo kumekuja miezi minne
baada ya ndege nyingine ya Malaysia, M370 ilipopoteza mawasiliano katika
muda wa chini ya saa moja baada ya kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kuala Lumpur na kupotea hadi sasa.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment