Mpango wa biashara ni roho ya biashara, kwani ndiyo unaoonyesha
dira ya biashara husika. Katika biashara tunasema bila kuwa na
mipangilio inayoeleweka, hakuna mafanikio yatakayoonekana.
Mpango wa biashara ni maelezo ya kina yaliyo
katika maandishi (na wakati mwingine kichwani mwa mtu) yanayoelezea
biashara ya mtu au kampuni fulani.
Maelezo hayo yanahusu bidhaa au huduma za biashara
husika, mbinu za uzalishaji, mbinu za kupata masoko, rasirimali watu,
muundo wa taasisi, mahitaji ya kifedha ikiwa ni pamoja na vyanzo vyake
na matumizi yake.
Mpango wa biashara unaelezea historia ya biashara
kwa maana ya wakati uliopita, wakati uliopo na ujao ambayo ndiyo lengo
kuu la biashara.
Pamoja na ukweli kuwa kuna mpango wa biashara
ambao hauko katika maandishi na ambao hutumiwa na wajasiriamali wadogo
walio wengi, katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia mpango wa
biashara ulio katika maandishi ndiyo unaokubalika zaidi kwani unaweza
kushikika na kufuatwa kikamilifu kama mwenye mpango husika atauandaa kwa
nia hasa ya kuendeleza biashara yake na wala si tu kwa ajili ya kupata
pesa kutoka vyombo vya fedha.
Mpango wa biashara ulio katika maandishi umekuwa
ukisisitizwa katika mafunzo mbalimbali yaliyo rasmi kwani unaweza
kutumika kuendeshea biashara hata kama mwenye biashara husika hayupo au
baada ya kifo cha mmiliki wa biashara au pindi mwenye biasahara apatapo
matatizo ya akili.
Kwa kuwa biashara ni maisha ya mjasiriamali na
mjasiriamali ni mtu wa mfano katika jamii kutokana na mchango wake
katika jamii na taifa kwa ujumla, mpango wa biashara hauna budi kuwa
bora ili kutoa picha halisi ya biashara na mmiliki wake.
Mpango mzuri wa biashara una sifa zifuatazo:
uliofikiriwa kwa umakini na wenye kutoa picha halisi ya biashara husika,
wenye kuelezea ubora na dira ya biashara husika, wenye kuelezea vizuri
tahadhari zinazohusiana na biashara husika, wenye kubainisha vizuri
vielelezo zinavyoonesha uwezekano wa kufanyika biashara husika, na wenye
mambo ya kuvutia kivitendo na yenye kuwasisimua/kuvutia wawekezaji
Mpango wa biashara una faida mbalimbali kwa
biashara husika na kwa mwenye biashara. Baadhi ya faida za mpango wa
biashara ni kama ifuatavyo: unaonyesha tathimini ya uchunguzi wa
uwezekano au uhalisia wa wazo jipya la biashara kimalengo na kiuchambuzi
pasipo kutawaliwa na hisia za mtu binafsi kwa kuonyesha uwepo wa masoko
na kiasi kinachotarajiwa kuuzwa katika masoko husika, uwezo wa
menejimenti katika kuendesha biashara, na kama biashara inaweza
kujiendesha kwa faida.
Mpango wa biashara unadokeza namna ya kuendesha
biashara kwa mafanikio zaidi kwa kubainisha fursa na kuepukana na
makosa, kuendeleza uzalishaji, usimamizi na mipango ya masoko, kutengeza
bajeti na makadirio ya upatikanaji wa fedha.
Mpango wa biashara unanadi au unelezea wazo la
biashara kwa watu wengine na hivyo kutumika kama msingi wa fedha mradi
kwa kubaini kiasi na aina ya mtaji unaohitajika, kukadiria faida na
marejesho ya uwekezaji, na kubashiri uingia wa pesa taslimu, uwezo wa
kulipia huduma na hulipaji deni.
Mjasiriamali mdogo anatakiwa kutambua kuwa mpango
mzuri wa biashara na utekelezaji wa mpango huo ndiyo njia pekee
inayoweza kusaidia biashara yake.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment