Margaret Mpango akizungumza na mwandishi wa gazeti la Mwananchi, nyumbani kwake mkoani Kigoma.
Margaret Ballali ambaye ni dada mdogo wa aliyewahi kuwa Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Ballali ameeleza jinsi
alivyojitahidi kumuwahi kaka yake kabla ya kukutwa na mauti, lakini
alishindwa na badala yake akaambulia kutoa heshima za mwisho na
kushiriki mazishi.
Margaret alisema alikwenda Marekani kutokana na
wito alioupokea Mei 12, 2008, saa 11:00 jioni kutoka kwa wifi yake (mke
wa Ballali, Anna Muganda), akimtaka afanye haraka kwenda nchini humo
kwani hali ya kaka yake (Ballali) haikuwa nzuri na kwamba alikuwa
akihitaji kuzungumza naye.
“Taarifa hiyo ilinishtua sana maana wifi
aliniambia nifanye nifanyavyo kutafuta ndege mapema kadri inavyowezekana
ili niende, maana hali ya kaka ilikuwa mbaya, kwa hiyo nilijipanga na
kwa sababu Mzee (Askofu Dk Gerald Mpango) alikuwa huko kwa shughuli za
kikazi, nilimwarifu ili ikiwezekana tukutane (Washington) DC,” alisema
Margaret ambaye ni mke wa Askofu Mpango wa Kanisa la Anglikana.
Alisema kutokana na kwamba alikuwa Kigoma wakati
huo, ilimchukua siku tatu kuanza safari, hivyo alisafiri kwa ndege ya
Swiss Air, Mei 15, 2008 na kutua Uwanja wa JF Kennedy, New York Marekani
Mei 16, saa 4:00 asubuhi, siku ambayo Ballali alifariki dunia.
“Nikiwa njiani na hata baada ya kutuas JFK,
nilikuwa nawasiliana na wifi. Alionekana kama mtu aliyekata tamaa na
alikuwa akiniuliza niko wapi kila wakati, nilikuwa nikisubiri ndege hapo
kwa saa kama mbili. Bahati mbaya ni kwamba baada ya kucheck inn
(kuidhinishwa kusafiri na kuingia sehemu ya kusubiria ndege), gurudumu
lake moja lilipasuka,” alisema.
“Hili jambo halikuwa la kawaida kwasababu ilibidi
sasa tushuke na tusubiri tena kwa saa kama mbili ili tubadilishiwe
ndege, na wakati nikiwa bado uwanjani hapo JFK, ilikuwa kama saa 8:00
mchana, nilipata simu kutoka kwa wifi akiniambia ‘Mage we have lost
Daudi’ (Margaret, tumempoteza Daudi (Ballali).”
Alisema hakuwa na cha kufanya zaidi ya kuendelea
na taratibu za safari na kwamba alipowasili Washington muda wa jioni
alikwenda moja kwa moja kwenye nyumba ya kuhifadhia maiti ya Vo Funeral
Home ambako aliwakuta wanafamilia, akiwamo Mama Muganda, watoto wa
Marehemu Rahel na Octavio pamoja na wauguzi wawili na madaktari wakiwa
wamezunguka kitanda cha marehemu, kabla ya mwili wake kuhifadhiwa.
Alisema baada ya hapo walirejea nyumbani na kuanza
kupanga taratibu za mazishi, ambayo yalifanyika Mei 23, 2008 katika
makaburi ya Gate of Heaven eneo la Silver Spring, Maryland, Marekani,
huku mumewe, Dk Mpango akiwa miongoni mwa walioongoza ibada ya maziko ya
kiongozi huyo.
Umahututi wake
Baadhi ya ndugu wa Ballali wanasema kubadilika
ghafla na kuwa mahututi kuliwashtua kutokana na kutokuwapo kwa taarifa
za mapema kuhusu ugonjwa wake.
Wanasema Ballali aliondoka Agosti 2007 kwenda
Marekani akiwa mzima na hawakuwa na taarifa zozote kwamba ni mgonjwa,
lakini walishtushwa na taarifa za kuugua kwake ghafla kiasi cha kuambiwa
kwamba alikuwa mahututi.
Ballali alilazwa katika Hospitali ya
Massachusetts, Boston mwishoni mwa Agosti 2007, wakati alipokwenda kwa
ajili ya uchunguzi wa afya yake na tangu wakati huo afya yake
haikuimarika hadi alipofariki dunia, Mei 16, 2008 akiwa nyumbani kwake
Washington DC.
Kabla ya kifo chake, alilazwa kwa mara ya katika Hospitali ya
Chuo Kikuu cha Georgetown lakini alirejeshwa nyumbani baada ya madaktari
wa hospitali hiyo kumwambia kwamba asingeweza kupona. Alifariki wiki
mbili baadaye.
Margaret, kwa upande wake, alisema awali
walishtushwa na taarifa kwamba Ballali yu mahututi na kwamba ilikuwa
vigumu kuamini kwa sababu kabla ya hapo hawakuwa na taarifa zozote za
ugonjwa wake.
“Mimi nilipata taarifa kwamba kaka (Ballali)
amekwenda Boston kwa ajili ya medical checkup (uchunguzi wa afya),
lakini ghafla niliarifiwa amelazwa na muda mfupi tukapewa taarifa
nyingine kwamba yuko mahututi, kweli nilishtuka,” alisema Margaret.
Kwa upande wake, Pascal, ambaye ni mdogo wa
Ballali alimwambia mwandishi wa Mwananchi nyumbani kwake katika Kijiji
cha Luganga wilayani Mufindi, Iringa akisema: “Taarifa za kuumwa kwake
zilitushtua, maana nilikutana naye siku chache kabla ya safari yake ya
kwenda Marekani na wakati huo alikuwa ametoka Dodoma, kwa jinsi
nilivyomwona hakuwa mgonjwa.”
Ballali aliondoka nchini wakati kesi za wizi wa
takriban Sh122 bilioni kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA)
zikiwa zimeshamiri. Ballali alitajwa kwenye kashfa hiyo kwa kuidhinisha
fedha kinyume na taratibu. Kuondoka kwake kulizua maswali yake, hali
kadhalika kuumwa na mazingira ya kifo chake ambayo yamefanya watu wengi
wahoji.
ameachwa maswali mengi.
“Tulipokaa muda si mrefu tulipata tena taarifa
kwamba kaka ni mgonjwa sana na yupo mahututi. Hapo wasiwasi wetu ulizidi
maana kama unavyotuona huku ni mbali, hivyo taarifa kutufikia zilikuwa
ni kidogo sana, kila tulipojaribu kufuatilia hatukupata taarifa
zinazotosheleza”.
0 comments:
Post a Comment