LATEST POSTS

Tuesday, January 14, 2014

Geita. Mtoto mwenye umri wa miaka sita ameuawa kikatili, baada ya kudaiwa kupigwa na baba yake kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake.
Hatua hiyo inadaiwa kutokana na mtoto huyo kwenda kucheza kwenye majaluba ya mpunga.
Tukio hilo linakuja kukiwa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) na taasisi mbalimbli nchini zikiwa zimeunda muungano wa waandishi mikoani kuandaa na kuandika habari za kuelimisha umma dhidi ya ukatili huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo alisema mtoto huyo aliuawa Januari 11 saa 1:00 usiku katika Kijiji cha Kibumba, mkoani hapa.
“Mtoto huyo alikuwa anaishi na baba yake taarifa zinasema mtoto alikuwa na tabia ya kutoroka nyumbani kwenda sehemu za majaluba ya mpunga kucheza. Tabia hiyo ilionekana kumkera mzazi na kuamua kumpiga,” alisema Paul.
Pia, alisema baada ya baba yake kumuua mtoto huyo, aliamua kumzika kitendo hicho hakikiwafurahisha majirani ndipo walipotoa taarifa polisi.
“Baada ya majirani kutoa taarifa, polisi tuliuchukua mwili huo na kuupeleka Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa uchunguzi, ilibainika alikuwa na michubuko kwenye mwili wake,” alisema Paulo.
Kamanda Paul alisema mtuhumiwa alikamatwa na upelelezi unaendelea na utakapokamilika atafikishwa mahakamani.
Alisema matukio ya aina hiyo yameongezeka hivi karibuni, huku akitoa wito kwa jamii kushirikiana na polisi kukabiliana na vitendo hivyo.
Alisema vitendo hivyo havitakiwi kufumbiwa macho na kwamba, polisi bila ushirikiano haiwezi kufanikiwa.

Chanzo: Mwananchi

0 comments: