Moshi/Kahama. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli amesema anawaachia
Watanzania waamue mkweli kati ya kamati yake na Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Kauli hiyo ya Lembeli inafuatia taarifa ya gazeti
moja la kila siku (Siyo Mwananchi), iliyomnukuu Nyalandu akisema ripoti
ya Operesheni Tokomeza Ujangili iliyowang’oa mawaziri wanne ilikuwa ya
uongo.
Nyalandu anadaiwa kutoa kauli hiyo alipozungumza
na viongozi wa taaluma mbalimbali na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa
Dodoma na Manyara kuhusu mgogoro wa mipaka kati wanavijiji na Hifadhi
ya Tarangire.
Pia, mgogoro huo unahusisha Pori la Akiba Nkungunero na vijiji vya jirani.
Nyalandu alikaririwa akisema kutokana na taarifa
hiyo kueleza wapo watu waliobakwa wakati siyo kweli. Tanzania imeonekana
kushuka kwa kiwango kikubwa katika utawala bora kutokana na ukiukwaji
haki za binadamu.
Hata hivyo, Lembeli alipoulizwa na gazeti hili
jana kuhusiana na kauli hiyo alijibu: “Sijaisoma hiyo habari ila
nimeisikia tu, kama ni kweli ametoa kauli hiyo (Nyalandu) basi ni
hatari.”
Lembeli alisema anawaachia Watanzania kupima mkweli kati yake, kamati yake na Waziri Nyalandu katika jambo hilo.
“Kwa sasa niko kijijini kwangu huku jimboni, lakini nitafafanua zaidi nitakaporejea Dar es Salaam,” alisema.
Ripoti hiyo ya kamati ndogo ya uchunguzi
iliyoongozwa na Lembeli ndiyo iliyosababisha mawaziri wanne kuwajibika,
kutokana na kuibuliwa kwa vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za
binadamu. Mawaziri waliong’olewa ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk
Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Dk Mathato David na Maliasili na Utalii, Balozi Khamis
Kagasheki alijiuzulu kabla.
Atangaza ubabe
Lembeli alikazia kwa kusema hawezi kuishi kwa
kuhofia vitisho vya maisha, kwa madai ya taarifa yake ya Operesheni
Tokomeza Ujangili iliyosababisha kung’olewa kwa mawaziri wanne.
Akihutubia mkutano wa hadhara Kata ya Igunda, Lembeli alisema haogopi vitisho hivyo na ataendelea kutetea masihali ya umma.
Awali, Diwani wa kata hiyo, Tabu Katoto wakati akimkaribisha, alimpa pole mbunge huyo kwa kazi ngumu na lawama aliyoifanya mwaka jana kwa faida ya taifa, hali ambayo Lembeli alisema inampa wakati mgumu kutokana na watu wenye akili ndogo kumpa vitisho vya maisha yake.
Chanzo: Mwananchi
Awali, Diwani wa kata hiyo, Tabu Katoto wakati akimkaribisha, alimpa pole mbunge huyo kwa kazi ngumu na lawama aliyoifanya mwaka jana kwa faida ya taifa, hali ambayo Lembeli alisema inampa wakati mgumu kutokana na watu wenye akili ndogo kumpa vitisho vya maisha yake.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment