LATEST POSTS

Wednesday, January 15, 2014

Niliula mguu wa adui kulipiza kisasi


Huku hali ya taharuki ikiendelea kutanda kati ya jamii za waisilamu na wakristo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, BBC imegundua mambo ya kutisha yanayofanyika mjini Bangui, mji mkuu wa taifa hilo.
Wanaoyashuhudia baadhi ya mambo hayo wameambia BBC kuhusu kisa cha mwanamume mmoja anayejulikana kwa jina la utani kama "Mad Dog," kuwa alimkata mguu muisilamu mmoja baada ya kumuua akisaidiwa na umati wa watu na kuula.
Mwanamume aliyekifanya kitendo hicho ameambia BBC kuwa alifanya hivyo kama hatua ya kulipiza kisasi baada ya wapiganaji wa kiisilam kumuua mkewe aliyekuwa mja mzito na wifi yake pamoja na mwanawe.

Aidha mwanamume huyo kwa jina Ouandja Magloire alisema kuwa kila mtu ameghadbishwa na wapiganaji waisilamu na hakuna atakayewasamehe kwa walichokifanya.

Anasema alimuona mwathiriwa akiwa ameketi ndani ya basi moja. Alimtoa nje na kuanza kumshambulia na punde si punde akasaidiwa na umati uliokuwa unashuhudia kitendo hicho ambao pia ulimshambulia mwathiriwa huyo.

"Muisilamu! Muisilamu! Muisilamu!. Nilimdunga kisu kichwani na kummwagia petroli kisha kumteketeza. Baadaye nikaanza kuula mguu wake mmoja kwa Mkate hadi kwenye mfupa. Ndio maana watu wananiita Mad-dog," alisema Magloire.

'Nilifanya hivyo kwa sababu nina uchungu mwingi, wala sina sababu nyingine.''

Hali ilivyo kwa sasa katika taifa hilo hakuna hata mtu mmoja aliyejaribu kumnusuru mwathiriwa. Jamhuri ya Afrika ya Kati imekumbwa na ghasia za kidini tangu Machi mwaka 2013 ambapo wapiganaji wa kiisilamu walimsaidia aliyekuwa Rais Michel Djotodia kuingia mamlakani kwa njia ya mapinduzi.

Kisa hiki hata hivyo kimewashangaza wengi sana . Na hali hii ikijiri, Mamia ya wanajeshi wa serikali walioasi jeshi na kujiunga na wapiganaji wakristo katika vita vyao dhidi ya waisilamu,wameanza kurejea katika kambi zao za kijeshi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, wanajeshi hao wengi wao wakiwa wamevalia mavazi ya kiraia walitia saini makubaliano na wakuu wa jeshi kabla ya kurejea kambini. Ni kutokana na ombi la mkuu wa majeshi Ferdinand Bomboyeke, aliyewasihi kurejea kambini Jumatatu.

Chanzo: BBC SWAHILI

0 comments: