LATEST POSTS

Sunday, January 19, 2014

Rais Kikwete ateua makatibu tawala wapya



Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa makatibu tawala wapya wa mikoa mitano na kuhamisha wengine, huku akiwateua makatibu wa wizara wawili kuwa makatibu tawala wa mikoa.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue iliyotolewa jana usiku, ilieleza kuwa uteuzi na uhamisho huo ulianza jana.
Mhandisi Omari Chambo ambaye alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi anahamishiwa Mkoa wa Manyara kuwa Katibu Tawala wa Mkoa huo na Dk John Ndunguru aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi anahamishiwa Mkoa wa Kigoma kuwa Katibu Tawala wa mkoa huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, makatibu tawala wapya na mikoa yao katika mabano ni Wamoja Dickolangwa (Iringa), Abdallah Chikota (Lindi) na Symthies Pangisa (Rukwa).
Wengine ni Alfred Luanda (Mtwara) na Jackson Saitabau (Njombe).
Taarifa hiyo iliwataja waliohamishwa kuwa ni Beatha Swai aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani na sasa anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI; Sipora Liana ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI; Benedict Ole Kuyan ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga anahamishiwa Mkoa wa Mara na Salum Chima ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa anahamishiwa Mkoa wa Tanga.
Wengine waliohamishwa ni Mgeni Baruani ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe anahamishiwa Mkoa wa Pwani; Juma Iddi ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya anahamishiwa Jiji la Arusha.

Chanzo: Mwananchi

0 comments: