Tanzania na Afrika zina mashujaa wengi. Baadhi yao
hawatajulikana kwa sababu habari zao hazikutangazwa. Walitenda mema
wakaondoka zao. Wengine tunao humu mitaani na vijijini, wanafanya mazuri
kimya kimya.
Shaaban Robert alizaliwa mwanzoni mwa karne ya 20
akafariki Juni 1962, muda mfupi baada ya Tanganyika kupata uhuru, akiwa
na miaka 53 tu.
Kazi zake zilitumika kukuza Kiswahili. Nikiwa
shule ya msingi, tulikariri mashairi yake; hadi leo sijasahau Utenzi wa
Haki. Ubeti wa 50 unazungumzia tabia:
“Usishiriki uongo.
Ijara upate hongo.
Mtu mwongo ni msungo.
Masuto mengi hupewa.”
Kikubwa ndani ya maandishi lukuki ya marehemu
Shaaban Robert ni lugha na ujumbe. Miaka zaidi ya 75 tangu alipoandika
kazi zake, bado inakuhitaji uchimbe sana ili kujua maana ya
anachokisema, jambo linalokusaidia msomaji kujenga umahiri na msamiati
wa Kiswahili .
Hapo juu ijara ni malipo, mshahara au kipato.
‘Msungo’ ni mtu asiyepewa malezi ya kutosha, kimila. Aliandika pia
makala akiwa mwanasafu wa Gazeti la Mambo Leo, kisha akatoa mkusanyiko
wa ‘Maisha Yangu Baada ya Miaka Hamsini’-Kitabu hiki kiliandikiwa
utangulizi na aliyekuwa Waziri wa Elimu mwaka 1966, S. Eliufoo.
Mwaka 1991 Mkuki na Nyota chini ya mchapishaji
mkongwe Walter Bgoya, ilitoa vitabu hivi tena. Tuna bahati sana kuwa na
Walter Bgoya. Kazi anayoifanya kuendeleza vitabu, inafaa kuigwa na
kufuatwa hasa na wafanyabiashara na viongozi wetu.
Ingawa Shaaban Robert anaelezea mambo yake ya
binafsi- ndoa, wanawe na kazi, kitabu kinatathmini umaana wa kuishi,
wajibu wetu katika jamii na masuala ya mapenzi kwa kina.
Mathalan, shuhudia binti yake alipofaulu darasa la
nne kwenda la tano. Enzi hizo za ukoloni (kisa kilitokea 1945), haikuwa
kawaida wanawake kusoma. Hivyo baba mtu anaomba ahamishwe kazi toka
Mpwapwa kurudi Tanga kulikokuwa na shule.
Anasema, “Mtoto yeyote anyimwaye makusudi ya kusoma, kuandika na
hesabu ana haki ya kuwalaumu wazazi wake katika maisha yake
atakapojiona kuwa amefungiwa milango yote ya kusitawi baadaye.”
Mbali na kumwongelea binti, anamsifia mama yake
ambaye hakupata elimu lakini akahakikisha yeye Shaaban anasoma. “Deni
lake kwangu la wema alionitendea halilipiki kabisa.”
Mbali ya elimu anazungumzia ubaguzi wa rangi,
unyanyasaji kazini na wajibu wa mwandishi. Huu ulikuwa wakati wa vita
vikuu vya dunia. Anasema alikuwa mtu pekee, Afrika Mashariki,
aliyeandika mashairi kupinga wauaji wa Kinazi chini ya Dikteta Adolf
Hitler. Alipoulizwa vipi anafanya “kazi ya bure,” Akasisitiza haikuwa
bure.
“Nilikuwa nikiandika habari ya tukio kubwa
lililotokea katika dunia wakati wa karne ya maisha yangu.” Anazungumzia
pia suala hilo hilo la kuwajibika kipindi Mwalimu Nyerere na TANU
wakipigania uhuru wa nchi. Ilikuwa hatari hata kwenda mikutanoni. Lakini
marehemu alihudhuria. Alipenda msimamo wa Nyerere na TANU. Anasema watu
wa madhehebu na kabila mbalimbali waliungana “chini ya mtu huyu”. Yaani
Nyerere.
Siyo ajabu akaunganisha jina lake la Kiislamu
(Shaaban) na Kikristo (Roberts), kuunga mkono kauli ya umoja Tanzania.
Leo wangapi wenye msimamo wa aina hii? Shaaban Robert alijali
yaliyoendelea, si tu kitaaluma (kuandika) au kisiasa, bali akiwa na
wenzake, kazini.
“Mapatano na amani kati ya watu yalikuwa ni mambo
mawili ambayo niliyapenda na niliyoyafikiri kuwa ni muhimu katika
maisha. Ndege wa manyoya hupatana katika kiota chao kidogo; ni aibu
kubwa wanadamu hukosana katika nafasi pana.”
Shaaban Robert ni mmoja wa mashujaa wakubwa sana
Afrika na ukweli hatujamheshimu ipasavyo. Ndiyo. Zipo barabara na shule
zinazotumia jina lake. Lakini je, tumehifadhi na kuzitangazaje kazi
zake? Je, kweli sisi tunaheshimu mashujaa? Je, kwa nini mashujaa ni watu
muhimu? Tuangalie mifano miwili.
Takriban wanasiasa wote duniani hufuata kanuni
zilizoandikwa na mwandishi wa Kiitaliano, Nicollo Machiavelli,
aliyefariki mwaka 1527 akiwa na miaka 58. Aliandika ‘The Prince’ (Mwana
wa Mfalme), kinachotoa mwongozo wa namna ya kuwatawala na kuwaongoza
watu. Swali kuu linaloulizwa ni je, kiongozi anatakiwa apendwe au
aogopwe? Machiavelli anadai yote mawili ; ila bora kuogopwa kuliko
kupendwa, ili kutimiza malengo. Kimetafsiriwa takriban lugha zote kubwa
duniani. Nadharia za Machiavelli zinafuatwa na wanasiasa na vile vile
kampuni kubwa kama Google, Facebook, wanamuziki wa Rap, 50 Cent na
marehemu Tupac aliyekitungia kitabu wimbo.
Ingawa ‘The Prince’ ilichapwa 1532 (miaka mitatu
baada ya mwandishi kufariki) leo ukienda alikozaliwa, Florence, bado
nyumba aliyoishi hata nakala ya kitabu alichoandika mwanzo kwa mkono
imehifadhiwa. Miaka mingapi imepita? Piga hesabu msomaji. Lazima ulipie
fedha kuingia ndani. Fedha inakwenda’api? Kwa familia yake na Idara ya
Utamaduni. Mbali na maandishi, utatembezwa katika mashamba ya mizaituni,
kunywa mvinyo maarufu, misitu mizuri na kuelezwa historia ya Italia
miaka 500 iliyopita. Sasa fikiria hilo lingefanywa kuhusu Shaaban
Robert- kama sehemu ya utalii na hazina kitaifa! Mwingine. Nimewahi
kuingia jumba aliloishi mchoraji maarufu Van Gogh wa Uholanzi aliyejiua
mwaka 1890 akiwa mwenda wazimu na umri wa miaka 37.
Leo ukifika mjini Amsterdam kuna jumba la
makumbusho, mgahawa na mambo kibao yanayolipiwa fedha kutukuza kazi zake
zinazopendwa ulimwengu mzima. Van Gogh ni fahari ya Waholanzi.
Majuma matatu yaliyopita kampuni mpya ya “New Deal
Africa” chini ya uongozi wa mwanahabari Ayoub Mzee na mwenzake Enzy
Larusai ilifanya tafrija ya kuwapa Watanzania mbalimbali wakazi wa
Ughaibuni tuzo. Kati yao walikuwa Aseri Kitanga (anayeleta kompyuta kwa
watoto Afrika), Dk Hamza Hassan na Mariam Kilumanga, kiongozi wa Chama
cha Wanawake Uingereza.
Amina Waziri, mjukuu wake Shaaban Robert alipokea
“Tanzania Achievement Award 2013,” kwa niaba ya babu- kwa kuendeleza
elimu na lugha. Hii siyo zawadi za kwanza. Akiwa hai, Ustaadh alipewa
tuzo ya MBE (Member of British Empire) na Margaret Wrong Memorial Prize
na Waingereza waliomheshimu sana.
Chanzo: Mwananchi
Mjukuu mwingine Aisha, alinieleza namna babu yake alivyokuwa
muda mfupi kabla ya mauti. Mrefu, mcheshi, mtanashati, aliyependa sana
watoto, vitabu na mpangilio wa vitu. “Aliweka chupa zake za wino kando
ya vitabu, si unajua enzi hizo kalamu zilikuwa za kuchovya? Sasa ole
wako uumwage ule wino!”
Wajukuu hawa wawili wanasema babu yao alipenda sana watu na familia yake. Haya jamani, tujivunie na kuwapamba mashujaa wetu.
0 comments:
Post a Comment