Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Abubakari Khamis Bakari, pamoja
na abiria 17 wamenusurika kifo, baada ya ndege ya shirika la ndege la
‘Zan air’ waliyokuwa wanasafiria kupata matatizo ya breki na kusererekea
vichakani.
Ndege hiyo iliyokuwa na marubani wawili, iliserereka wakati inatua
katika Uwanja wa Ndege wa Karume kisiwani Pemba ikitokea Unguja juzi
jioni.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kusini Pemba, Swalehe Mohamed Swaleh,
akizungumzia ajali hiyo alisema ilitokea baada ya ndege hiyo kuwasili
Pemba ikitokea Unguja.
Alieleza kuwa ilikwenda kwa kasi kama kawaida ikitarajiwa kuwa ingepunguza mwendo lakini ilishindwa kufanya hivyo.
“Ni kweli ndege hiyo ya ‘Zan Air’ ilipata hitilafu na kuingia
majanini lakini abiria wote waliokuwamo na marubani wawili, walitoka
salama,’’alifafanua.
Alisema polisi imeliimarisha ulinzi wa ndege na abiria hao na haikuruhusiwa watu wasiohusika kuzengea eneo hilo.
Baadhi ya mashuhuda walioishuhudia ndege hiyo walisema ilikwenda
kwa kasi kubwa kama gari zinazofukuzana na kumfanya muongoza ndege
uwanjani hapo kukaa pembeni akishangazwa na kilichotokea.
Walisema baada ya kuiona ikiwa haipunguzi mwendo kasi kama inavyotakiwa, ghafla iliingia majanini na kuacha barabara ya ndege.
Mkuu wa kikosi cha zima moto na uokozi kisiwani Pemba Shaban Zidi
Heri Juma, alishuhudia ndege hiyo ikikimbia kwa kasi kubwa ambapo gari
la zima moto liliifuata kwa haraka hadi iliposimama kichakani.
Meneja wa uwanja huo, Rajabu Ali Mussa, alisema tukio hilo
lilitokea saa 10:30 jioni jana na kwamba ilipata hitilafu baada ya
uchunguzi wa awali kuonyesha matatizo ya breki.
Alifafanua kuwa wataalamu watachunguza ili kujua chanzo cha hitilafu kwenye breki.
Chanzo: Nipashe Jumapili
0 comments:
Post a Comment