Zanzibar. Kazi ya kutafuta mabaki ya miili ya
raia wawili wa Ufaransa waliouwawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga na
kutupwa katika kisima huko Matemwe katika Mkoa wa Kaskazini,
imekamilika, imefahamika.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Unguja, Pembe Juma Khamis, alisema kazi ya kufukuwa kisima
hicho ilikamilika saa 9:00 alasiri ya juzi.
Alisema kazi hiyo ilifanywa kwa ushirikiano wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi ,Polisi na wananchi wa shehiya hiyo.
Khamis alisema kwa sababu ya mazingira magumu
katika kuvunja zege, ili kufika kina kikubwa cha kisima hicho, wataalamu
wa uokoaji waliamua kutumia trekta la kuchimbia vifusi kuchimba na
kufanikiwa kupata mabaki ya mifupa. Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa,
mabaki hayo ni pamoja na fuvu moja na hivyo kufanya idadi ya mafuvu
yaliyopatikana kuwa mawili. Alitaja mabaki mengi kuwa ni mifupa ya miguu
na mbavu.
“Kazi ya kutafuta mabaki ya miili imekamilika
baada ya waokoaji kutumia kijiko cha kuchimbia vifusi. Tunashukuru kazi
hiyo imemalizika salama na na kinachofuatia sasa ni uchunguzi wa kijinai
unaofanywa na polisi”, alisema mkuu huyo wa mkoa.
Kuhusu kiini cha mauaji hayo, alisema anayepaswa
kuzungumzia ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar,
Yussuf Ilembo.
Alipoulizwa kuhusu maendeleo ya uchunguzi wa tukio
hilo mkurugenzi huyo alisema msemaji ni Kamishana wa Polisi Zanzibar,
Hamdani Khamis Omar.
Kwa upande wake, Kamishna Hamdani alisema hakuwa katika mazingira mazuri ya kutoa taarifa kuhusu kukamilika kwa kazi hiyo.
Raia wawili wa Ufaransa Francios Chererobert
Daniel ambaye aliwahi kuwa mtumishi wa ngazi ya juu katika Serikali ya
Ufaransa na mkewe Brigette Mary waliuawa na kufukiwa kisimani kwa
kutumia zege.
Tayari watu watatu wanashikiliwa na polisi kwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Tukio hilo limekuja miezi kadhaa baada ya raia wawili ya Uingereza kumwagiwa tindikali mjini Unguja mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment