Home »
» CCM KALIUA WAPINGANA NA AGIZO LA RCC.
MWENYEKITI wa jumuiya ya wazazi ya chama mapinduzi (CCM),wilaya ya
Kaliua mkoa wa Tabora Hassan Aleale amepingana na maagizo ya kamati ya
ushauri ya mkoa (RCC) kuhusiana na wilaya hiyo kuhamia mkoa wa Katavi.
Kauli hiyo aliitoa kwenye mutano wa hadhara uliotishwa na CCM wilaya
na kufanyika katika viwanja vya Msufini.
Akihutubia wananchi Aleale alisema anashangazwa na baadhi ya madiwani
wa kata 12 ambao wamebadili msimamo na kukataa wilaya hiyo kuhamia
mkoa wa Katavi wakati awali walikubaliana.
Aleale alisema kata 6 ndizo zina msimamo wa wilaya ya Kaliua kuhamia
mkoa wa Katavi lakini anashangazwa na hatua ya madiwani wa kata 12
ambao wana ajenda ya siri katika hilo.
"Awali kuna ujumbe ambao ulikwenda mkoa wa Katavi na kuna mambo ambayo
walijifunza na kukubaliana.....lakini leo hii kwa sababu zao binafsi
wamebadili msimamo."aliongeza.
Alisema wapo watu ambao kwa maslahi yao binafsi wamepandikiza maneno
kuwa mbunge Profesa Kapuya anawalazimisha kuhamia mkoa wa Katavi
wakati wao walishakubali kwenye vikao halali.
Aleale aliongeza kuwa wapo viongozi wilaya ya Kaliua walikwenda mkoa
wa Katavi na kuna kura zilipigwa ikaonekana wengi wanataka kuhamia
mkoa wa Katavi lakini kutokana na kurubuniwa wakabadili misimamo.
Anafafanua kuwa siku zote viongozi ambao huwa hawasemi ukweli itafikia
siku watawajibishwa kwa ajili ya maslahi ya wananchi.
Kuhusu Ulyankulu kuwa wilaya mwenyekiti huyo alifafanua kuwa maneno
yanayosemwa na watu kuwa profesa Juma Kapuya hataki Ulyankulu iwe
wilaya siyo kweli na kwamba ni uzushi mtupu.
Alisema eneo la Ulyankulu kwa asilimia 92 ni eneo la hifadhi hivyo
kuanzisha wilaya bila kubadili baadhi ya maeneo kutoka hifadhi kuwa
makazi ya watu lazima yazingatie utalaamu.
Alisema wananchi wamepata wilaya ya Kaliua hivi karibuni na wilaya hii
imetokana na wilaya ya Urambo ambayo ilianzishwa mwaka 1975.
Alifafanua kuwa wilaya inayotakiwa na kudaiwa kupigwa vita na Kapuya
ni lazima itokane na wilaya ya Kaliua na mchakato wake ni lazima
kwanza mchakato wa kubadili matumizi ya maeneo ya hifadhi,kuongeza
kata na vijiji kuomba jimbo na ndipo wilaya inaweza kuanzishwa.
Alisema msimamo wa CCM wilaya ya Kaliua ni kuhamia Katavi na
kuanzishwa wilaya ya Ulyankulu kufuate taratibu za kisheria.
Alisema kuendelea kumzulia Kapuya maneno ya uongo kila kukicha,siyo
sahihi kwani Kapuya amefanya mengi mazuri wilayani hapa na siku zote
mafanikio yoyote yanakuja na changamoto zake.
Alisema tufikie mahali tuone haya tumuache mzee wa watu Kapuya afanye
kazi za maendeleo na kwamba ataitisha mkutano mwingine ili kuweka wazi
viongozi wa CCM wakiwemo madiwani waliotafuna fedha za wakulima kama
mmoja aliyekula sh milioni 240 na hajakamatwa.
Chanzo: Tabora yetu
0 comments:
Post a Comment