LATEST POSTS

Sunday, March 23, 2014

HALMASHAURI YA WILAYA YA URAMBO YATUNGA SHERIA KALI KUDHIBITI UTORO SHULENI

Wazazi kutozwa faini 300,000/-

KATIKA kukabiliana na utoro, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Urambo limepitisha sheria kali kuwabana wazazi na walezi walioshindwa kuwapeleka watoto shuleni.
Iwapo sheria hiyo iliyopitishwa mwishoni mwa wiki itatekelezwa kama ilivyo, adhabu ya kosa la utoro au kuzuiwa watoto kwenda shule ni faini ya sh. 300,000.
Uamuzi wa kupitisha sheria hiyo ndogo ulifikiwa baada ya mjadala wa kina kuhusu nini kifanyike ili kudhibiti utoro wa wanafunzi uliokithiri katika shule za msingi na sekondari wilayani humo.
Kwa kauli moja madiwani walipitisha adhabu ya faini ya sh. 300,000 ama kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa pamoja.
Lengo la adhabu hiyo imeelezwa ni kuwabana wazazi na walezi wasiwazuie watoto kwenda shule na kuwadhibiti wanafunzi watoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Richard Ruyango, alisema sheria hiyo ni muhimu kwa kuwa itasaidia kudhibiti utoro.
Alisema pia itasaidia kuinua kiwango cha elimu na kuongeza ufaulu wa wanafunzi kwa kuwa mahudhurio darasani yataongezeka tofauti na awali.
“Huu ndiyo mwarobaini kwa wazazi waliokuwa wanakwepa kuwapeleka watoto shule kwa visingizio mbalimbali, ikiwemo umasikini, huku wakiwatorosha na kuwapeleka katika kilimo cha tumbaku au kuchunga ng’ombe,” alisema.
Baadhi ya wazazi wamekiri kukithiri utoro kutokana na watoto kupelekwa katika kilimo cha tumbaku, jambo linalochangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu na elimu kuporomoka wilayani humo.
Hata hivyo, licha ya kupongeza kupitishwa sheria hiyo, baadhi ya wazazi ambao wengi ni wakulima na wafugaji, wameomba ipunguzwe makali kwa kuwa itawaumiza.
Ruyango alisema sheria hiyo imetungwa na kupitishwa na madiwani baada ya wananchi kushirikishwa kutoa maoni kuhusu nini kifanyike ili kudhibiti utoro.
Alisema wazazi wasiopenda sheria hiyo itumike ndio ambao wamekuwa wakiwazuia au kutowapeleka watoto shuleni.
 
 Chanzo:uhuru online

0 comments: