LATEST POSTS

Wednesday, April 3, 2013

DOKTA BOYA, AFISA WA SERIKALI ANAYEJISHUGHULISHA NA SHUGHULI ZA KILIMO


Dokta Lyebu Boya ni Afisa Mifugo katika Halmashauri ya Wilaya ya Urambo. Kutokana na kazi hiyo,Yapo majukumu ya kila siku ya kiofisi ambayo anapaswa kuyatekeleza kama Afisa Mifugo lakini, pamoja na majukumu hayo aliyonayo, Dokta Boya anajishughulisha na shughuli za kilimo pamoja na ufugaji baada ya masaa ya kazi na hasa katika siku za mwishoni mwa wiki.
 
Akiongea na Mwandishi wa Makala hii, Dokta Boya alisema kuwa, kilimo kipo kwenye damu yake na anaamini kwamba, kwake yeye, maana halisi ya kilimo, inajumuisha pamoja na masuala ya ufugaji Wanyama(Mifugo). Kwa maana hiyo, pamoja na kulima mazao ya Mpunga, Mahindi, Karanga, Viazi vitamu, Migomba vilevile anafuga Ng'ombe wa kienyeji ambao huwatumia kama Wanyamakazi na pia humpatia samadi na Maziwa.

 
         Moja ya mifugo ambayo inafugwa na Dokta Boya ni kuku

Dokta Boya aliendelea kusema kuwa, ameamua kujiingiza katika kilimo ili kuwa na uhakika wa chakula nyumbani kutokana na uzalishaji wake mwenyewe, kujiongezea kipato na kupunguza matumizi ya fedha inayotokana na mshahara ili aweze kufanya shughuli zingine kwa ajili ya maendeleo yake, kushiriki pamoja na Wakulima ili kujua changamoto mbalimbali ambazo wanazipata katika shughuli za kilimo na ufugaji ili iwe rahisi kuwapatia ushauri wa kitaalamu kuhusiana na masuala ya kilimo pale inapohitajika, kupata nafasi nzuri ya kujaribu baadhi ya teknolojia za kilimo na ufugaji kama vile mbinu bora za kilimo na ufugaji, mbegu bora, zana na madawa ya kilimo na mifugo.

 
Muhogo uking'olewa shambani kwa Dokta Boya

 
Kung'oa shina moja inatakiwa ule ushibe hasa maana si mchezo

 
Dokta akiwa kwenye tuta alilolima muhogo

 
Muhogo huo

 
Mmh!!
Dokta Boya ambaye amefanikiwa sana katika masuala ya kilimo na ufugaji kiasi cha kuivutia www.urambonews.blogspot.com kuamua kumtembelea shambani kwake na kuandika makala hii kwa faida ya Wakulima wa Urambo na Tanzania nzima kwa ujumla ili waweze kujifunza kupitia kwake alisema kuwa, siri kubwa ya mafanikio yake katika kilimo ni kufuata kanuni bora za kilimo kama vile kulima na kupanda mazao mapema, kutumia mbegu bora , kutumia mbolea kwa usahihi na kudhibiti wadudu waharibifu.
 
 
Bwawa la Dokta Boya

 

 
 
 
 
Samaki aliyevuliwa katika bwawa la Dokta
 
Vilevile amekuwa akifanya juhudi za ziada kwa kutumia muda wake wa ziada baada ya saa za kazi kusimamia na kufuatilia shughuli za kilimo, kujifunza kupitia kwa wakulima wengine na kuendeleza shughuli za kilimo kwa kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira.
Aidha, alisema alipata mafunzo na maelekezo ya kanuni kumi bora za kilimo na ufugaji. Vilevile, Halmashauri iliweza kumpatia usafiri wa kubeba Vifaranga vya Samaki kutoka Kata ya Ukondamoyo na Kata ya Ukondamoyo hadi kwenye bwawa lake.
"Kusema ukweli, kilimo kimeweza kuninufaisha kwani hadi sasa, mimi sinunui mchele, mahindi, karanga, viazi vitamu, mihogo, kuku wala samaki, nimeongeza eneo la shamba la kulima, ninatoa ushauri kwa Wakulima kwa ufanisi kuhusiana na kilimo na ufugaji, na kwa kujifunza kupitia kwangu, wakulima nane kutoka katika Kijiji ambacho ninafanyia shughuli zangu za kilimo, wameweza kuchimba mabwawa na kufuga samaki kwa nguvu zao wenyewe na pia, nimeweza kujenga nyumba ya kuishi". Alisema Dokta Boya.
Pamoja na mafanikio hayo aliyoyapata, Dokta Boya anakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile kuchoka kwa ardhi, kustawi kwa magugu aina ya  striga hasa kwenye zao la mahindi, wadudu waharibifu kama vile Lusomi na Viwavi jeshi, magonjwa ya Ng'ombe yaambukizwayo na Kupe na magonjwa ya minyoo, magonjwa ya kuku hususani mdondo na ndui ya kuku.
Vilevile, ipo changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa ambapo kuna wakati kunakuwepo na hali ya ukame na muda mwingine mvua kuanza kunyesha. Mabadiliko haya yanaathiri muda wa kuanza kulima na kupanda.

 
Shamba la Mpunga la Dokta

 
Dokta Boya akiwa kwenye shamba lake la Mpunga
Ili kukabiliana na changamoto hizo, Dokta Boya anatumia dawa za kuulia wadudu waharibifu mara tu dalili zinapojitokeza, huogesha ng'ombe kwa kutumia dawa za kuua kupe, inzi na mbung'o na kuwapa dawa za kuua minyoo, kuchanja kuku kwa kutumia dawa za matone ili kudhibiti ugonjwa wa mdondo na kutumia mbegu mbalimbali katika kilimo zinazostawi kwa muda mrefu na kuzaa sana wakati wa mvua nyingi na mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi wakati wa mvua.
Akihitimisha, maongezi yake na mwandishi wa Makala haya, Dokta Boya alishauri Wataalamu wa Kilimo na Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo waendelee kutoa ushauri kwa Wakulima na Wafugaji wa kuwataka watumie kanuni bora za kilimo, kuwepo na mashamba maalum kwa yatakayomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya na kusimamiwa na Idara ya Kilimo kwa ajili ya maonesho.
Aidha, kwa upande wa Wananchi, aliwataka wathamini na kufuata ushauri wa kitaalamu wanaopewa na wataalamu wa kilimo na mifugo, wajenge tabia ya kwenda kwa mtaalamu kuomba ushauri wa kitaalamu kuhusiana na kilimo na si kusubiri mtaalamu awafuate na pia, Wananchi wawe wanahudhuria vikao na mikutano ya kitaalamu inayoendeshwa kwenye maeneo yao ili kujua mambo mbalimbali yanayojiri kuhusiana na masuala ya kilimo na ufugaji kitu ambacho kitawasaidia kuweza kuibua miradi ya maendeleo ya kilimo na mifugo.

Imeandaliwa na:
Theresia Chacha
Urambo. 

0 comments: