MAUAJI ya kikatili
dhidi ya wanawake wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga yamezidi kupamba
moto kufuatia tukio la kuuawa mama na mwanaye walioshambuliwa kwa
kukatwakatwa mapanga huko katika Kijiji cha Ngokolo Kata ya Bukomela
usiku wa kuamkia juzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist
Mangala aliwataja wanawake waliouawa kuwa ni Mhulu Nh'ambo (50) na
mwanaye Helena Charles (30), walioshambuliwa kwa kukatwakatwa mapanga na
watu wasiojulikana mnamo saa moja usiku walipokuwa wakiandaa chakula
cha usiku nyumbani kwao.
Kamanda Mangala alisema, siku hiyo ya tukio
wakati mama huyo akiwa na mwanaye wakiandaa chakula cha usiku ghafla
walivamiwa na kundi la watu wasiojulikana ambao waliwashambulia kwa
kuwakatakata mapanga sehemu za kichwani na mgongoni hali iliyosababisha
wapoteze maisha papo hapo kutokana na kuvuja damu nyingi.
Hata
hivyo, alisema chanzo cha mauaji hayo mpaka sasa hakijafahamika na
tayari polisi inamshikilia mtuhumiwa mmoja ambaye jina lake
limehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi na juhudi za kuwasaka watuhumiwa
wengine zinaendelea ili waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani
kujibu shtaka la mauaji.
Kamanda Mangala ametoa wito kwa raia wema
kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi ama ofisi za watendaji wa
vijiji na kata pale watakapomuona mtu au watu wanaowatilia shaka ili
waweze kukamatwa na kuchunguzwa iwapo walihusika na mauaji hayo.
Hivi
karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya alikiri kuwepo na
wimbi kubwa la mauaji dhidi ya wanawake na kusema mauaji yanayofanyika
hivi sasa ni tofauti na yale ya awali ambapo waliokuwa wakiuawa ni
wanawake vikongwe wenye umri wa kuanzia miaka 60.
Alisema, hivi sasa
takwimu zinaonesha wanawake wanaouawa ni pamoja na wale wenye umri wa
kati ya miaka 50 hadi 20 ikiwemo wanaochinjwa na waume au wenzi wao wa
kiume kutokana na kinachodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Mpesya
aliyekuwa akihojiwa na mwandishi wa habari aliyekuwa akifanya utafiti wa
vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo mauaji ya vikongwe katika
wilaya hiyo ulioandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA)
alisema, takwimu zinaonesha hivi sasa ndani ya mwezi mmoja hutokea
mauaji ya wanawake wasiopungua watatu.
Alisema, ugomvi wa kuwania
mali ikiwemo mirathi na masuala ya kugombea ardhi ni moja ya chanzo cha
mauaji hayo ambapo hata hivyo katika kipindi cha Novemba, mwaka jana
wanawake watatu waliouawa kwa kuchinjwa akiwemo mwanafunzi wa kidato cha
nne chanzo kilikuwa ni wivu wa kimapenzi.
0 comments:
Post a Comment