LEO ni siku ya 100 tangu Rais John Magufuli alipoingia Ikulu ya
Magogoni, Dar es Salaam, na tangu alipotoa hotuba yake siku ya kuapishwa
na ile ya uzinduzi wa Bunge la 11, ameishi katika maneno yake kwa
kutenda kile anachokisema.
Miongoni mwa mambo aliyoahidi ni kupambana na rushwa pamoja janga la
dawa za kulevya, akisema dawa za kulevya zimeathiri vijana wengi, hivyo
akaahidi kushughulikia mtandao huo na wakubwa wanaohusika. Kwa upande wa
rushwa, Rais Magufuli aliahidi kupambana na ufisadi na rushwa na katika
kutekeleza hilo, alisema ataunda mahakama maalumu ya kushughulikia wezi
wakubwa yaani mafisadi. Pia aliahidi kuwashughulikia wafanyakazi
wazembe ili Serikali yake isiendelee kulea watu wanaolipwa mishahara tu
wakati hawafanyi kazi yoyote.
Katika kubana matumizi ya serikali, aliahidi kudhibiti warsha ambazo
hazina umuhimu katika Serikali wala kuongeza ufanisi kwa wafanyakazi.
Aliahidi pia kudhibiti safari za nje, ambazo zimekuwa zikigharimu
Serikali fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika katika shughuli
mbalimbali za kimaendeleo. Rais Magufuli pia alisema Serikali yake
itaongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato, ukizingatia kuwa kodi ni
kitu muhimu na ni lazima zikusanywe.
Aliahidi kufufua viwanda viliyobinafsishwa, ambavyo baadhi alidai
vimegeuzwa mazizi ya mbuzi wakati waliopewa kwa madhumuni ya
kuviendeleza. Aliahidi pia kushughulika na kero zinazolalamikiwa
kutendwa na polisi, hospitali, mizani, Mahakama, maliasili na vilio vya
wachimbaji. “Inabidi haya yote niyataje ili nijue tunaanzia wapi na
tunakwenda wapi, nisipoyataja nitakuwa mnafiki,” alisema Rais Magufuli
wakati akizindua Bunge la 11 mjini Dodoma.
Tayari Rais Magufuli ametenda yale ambayo aliyaahidi kwa Watanzania.
Amebana matumizi ya serikali kwa kudhibiti safari zisizo na tija,
matumizi yasiyo ya lazima, ameshughulikia watumishi wazembe,
ameshughulikia mafisadi ndani ya serikali na kutoa elimu ya bure.
Alivyoanza kazi Mara tu baada ya kuingia ofisini, alimuapisha
Mwanasheria Mkuu, George Masaju aliyemteua muda mfupi tu baada ya
kuapishwa.
Kesho yake, Rais alifanya ziara ya kushtukiza katika Wizara ya Fedha
ambako aliagiza maofisa wa wizara hiyo, kuhakikisha wanaongeza kasi ya
ukusanyaji mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hususan kwa
wafanyabiashara wakubwa bila kuogopa. Akataa mchapalo wa Bunge Rais
alionekana tofauti na viongozi wengine waliomtangulia baada ya kuifanya
sherehe ya kuzindua Bunge kutokuwa ya kifahari na hivyo akaokoa Sh
milioni 251, ambazo aliagiza zikanunue vitanda Hospitali ya Taifa
Muhimbili.
Jumla ya vitanda 300, magodoro 300, viti maalumu vya wagonjwa 30,
vitanda vya kubeba wagonjwa 30 na mashuka 1,695. Afuta gwaride la Uhuru
Rais Magufuli pia alifuta gwaride la Siku ya Uhuru, badala yake akaamuru
siku hiyo iadhimishwe na wananchi wote kwa kufanya usafi maeneo
yanayowazunguka ili kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu.
Wananchi waliitikia agizo hilo kwa wingi na kufanya usafi mkubwa.
Fedha Sh bilioni nne zilizopaswa kutumika kugharimia shamrashamra za
Siku ya Uhuru, ambazo zingefanyika tarehe 9 Desemba 2015, Rais aliamuru
zitumike kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar
es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3, kwa kuongeza njia mbili za
barabara za lami.
Ujenzi wa barabara hiyo tayari umeanza. Majipu yalivyotumbuliwa Rais
alianza kazi ya kutumbua majipu siku yake ya nne akiwa ofisini, alifanya
ziara ya ghafla katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambako
alijionea huduma zilizozorota hospitalini hapo na hivyo akalazimika
kuivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)
pamoja na kumuondoa madarakani Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo,
Dk Hussein Kidanto.
Mamlaka ya Mapato Baadaye Waziri MKuu Kassim Majaliwa alifanya ziara
katika Bandari ya Dar es Salaam, ambako aligundua upotevu wa makontena
329. Hatua iliyosababisha Rais kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA,
Rished Bade na kumteua Dk Phillip Mpango kukaimu nafasi hiyo. Kabla ya
Bade, Majaliwa alishatangaza kuwasimamisha kazi Kamishna wa Forodha,
Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya.
Wengine ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(Tehama), Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari na Mkuu wa Kitengo cha Bandari
Kavu, Eliachi Mrema. Majaliwa pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka
hiyo, wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani, ambao ni
Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni, lakini baadaye
akabadilisha uamuzi wake na kuamuru watumishi hao nao wasimamishwe kazi.
Upotevu huo wa makontena pia ulisababisha TRA kuwasimamisha kazi
watumishi wake 35 na kampuni 43 za uwakala wa forodha, zilisimamishwa
kwa tuhuma za kuhusika kutorosha makontena hayo. Uchukuzi, Bandari na
Reli Baada ya kubainika matumizi ya Sh bilioni 13 za Kampuni ya Reli
(TRL) kutumika kiholela, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Katibu Mkuu
wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka kwa ajili ya kupisha
uchunguzi dhidi ya matumizi mabaya ya fedha hizo.
Pia Rais siku hiyo aliivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), iliyokuwa chini ya Profesa Joseph
Msambichaka kutokana na kubainika madudu mengi bandarini hapo. Rais pia
alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadh Massawe. Takukuru
Katika kutimiza ahadi yake ya kupambana na ufisadi, Rais Magufuli pia
alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti
Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea.
Alimteua Naibu Mkurugenzi Valentino Mlowola kukaimu nafasi hiyo.
RAHCO Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania
(RAHCO), Benhadard Tito naye alisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa
kina kutokana na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi, uliobainika
katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa Reli ya Kati. Licha ya
kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Rahco, Rais Magufuli pia
aliivunja Bodi ya Rahco.
Vitambulisho vya Taifa Kutokana na malalamiko ya kusuasua kwa utoaji
wa vitambulisho vya Taifa, Rais pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na
kuwasimamisha kazi maofisa wengine wanne wa taasisi hiyo.
Maofisa wanne wa NIDA waliosimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa
namna Sh bilioni 180 zilivyotumiwa na mamlaka hiyo wakati wananchi
waliopatiwa vitambulisho vya taifa na mamlaka hiyo ni wachache ni
Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande,
Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na George Ntalima ambaye ni Ofisa
Usafirishaji.
Mabalozi Rais pia aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja
mabalozi wawili, ambao mikataba yao iliisha. Mabalozi hao ni Batilda
Buriani aliyeko Tokyo nchini Japan na Dk James Msekela aliyeko Rome,
Italia. Rais alimrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London,
Uingereza, Peter Kallaghe.
Balozi huyo anarejea wizarani ambako atapangiwa kazi nyingine.
Uhamiaji Madai ya kukithiri kwa rushwa katika Idara ya Uhamiaji pia
kulimfanya Rais Magufuli kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Uhamiaji,
Sylvester Ambokile na Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia Utawala na
Fedha, Piniel Mgonja ili kupisha uchunguzi katika idara hiyo nyeti
nchini.
Elimu bure yaanza Katika siku zake 100 akiwa Ikulu, Rais Magufuli
ametenga Sh bilioni 137 kwa ajili ya kugharimia utoaji wa elimu ya bure
kuanzia Januari hadi Juni mwakani. Elimu bure inatolewa kuanzia shule ya
awali hadi kidato cha nne
0 comments:
Post a Comment