Sophia Manguye akisaini mara baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo.
Mwanamke aliyepambana na jambazi na kufanikiwa kumnyang’anya bunduki
aina ya SMG, Sophia Manguye (46), amepewa zawadi ya Sh 500,000 na
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Tarime/Rorya, Gemini Mushy.
Mwanamke huyo ambaye aliomba Serikali kumpa silaha ili kujilinda,
alisema kuwa hajaridhika na zawadi hiyo kwa kuwa kama asingemmudu
jambazi huyo watu wengi wangepoteza maisha.
Hata hivyo, Mushy alimwomba Manguye kupokea kiasi hicho japokuwa ni kidogo kwa kuwa ni zawadi kutoka ofisi yake.
Sophia Manguye akihojiwa na wanahabari.
Tukio hilo lilitokea Februari 9, saa 2.42 usiku, baada ya watu watatu
kufika dukani kwake, mmoja wao akiwa na bunduki kisha kumwamuru atoe
fedha alizokuwa nazo.
Manguye alisema alichukua Sh80,000 alizokuwa nazo na kumkabidhi
jambazi huyo, lakini hakuridhika na kumlazimisha aongeze kiasi kingine.
“Nilipandwa hasira nikanyanyuka wakati jambazi anainama kuangalia
kwenye kiboksi cha fedha, nikamkamata kifuani na kung’ang’ania mkanda wa
bunduki, akaanza kunivuta kwenda nje, nami nikamvutia ndani, lakini
alifanikiwa kunitoa nje akaniangusha chini, lakini sikuachia mkanda wa
bunduki,” alisema Manguye na kuongeza:
“Aliposikia
wananchi wameanza kupiga yowe akaniachia na kutoa mkanda wa silaha
begani, akakimbia na kuniachia bunduki. Wakati huo huo jambazi mwingine
alikuwa amekamatwa kwenye duka la Zaituni Magasi, wananchi walipofika
wakaanza kumshambulia, wakati huo taarifa ilikuwa tayari imetolewa Kituo
cha Polisi Sirari, wakafika kumchukua,” alisema.
Hii
ni mara ya pili kwa Manguya kuvamiwa na majambazi wenye silaha, ambapo
mwaka 2014 alivamiwa dukani kwake na majambazi waliokuwa na bunduki,
lakini alifanikiwa kumpiga kwa kigoda aliyekuwa na bunduki na alianguka
chini.
Magasi alisema wakati wa tukio hilo, alikuwa amevamiwa na majambazi waliokuwa na bunduki, mapanga na nondo.
“Wakati anatoka mvunguni mdogo wangu alimkamata kwa nyuma na kummudu
huku akipiga kelele, watu wakafika wakaanza kumpiga hadi akazimia,
polisi walipofika wakamwokoa kwani kidogo wamuue,”alisema.
Source:Global Publishers
0 comments:
Post a Comment