LATEST POSTS

Tuesday, February 25, 2014

TBS kuteketeza juisi za Smile Dar

Dar es Salaam. Shirika la Viwango Tanzania(TBS) linakusudia kuteketeza kinywaji chenye ladha ya matunda (juisi) kijulikanacho kwa jina la Smile, baada ya kubaini kuwa hakina viwango vinavyohitajika.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Ubora wa Bidhaa wa TBS, Ashura Katunzi alisema maofisa wa shirika hilo walipata taarifa kutoka kwa walaji kuhusu juisi hiyo inayotengenezwa na Kampuni ya A One Products and Bottlers Ltd, ambayo ni miongoni mwa kampuni tanzu za Mohamed Enterprises.
“Maofisa wa TBS walikwenda kufanya ukaguzi kwenye kiwanda eneo la Vingunguti, Dar es Salaam Januari 20 mwaka huu, na walichukua sampuli ya juisi mbili ya Smile na Pride zenye ladha ya machungwa kwa ajili ya kuzichunguza, kabla ya kubaini kutokuwa na viwango vinavyotakiwa,” alisema.
Alisema gharama za kuteketeza juisi hiyo zitatolewa na kampuni husika, kwa sababu TBS haipo tayari kuona bidhaa ambazo hazijakidhi kiwango cha ubora zinaendelea kusambazwa sokoni.
Mwenyekiti wa Kampuni ya Mohamed Enterprise, Gulam Dewji akizungumzia suala hilo, alisema walishakubaliana na TBS kutopelekwa sokoni juisi hiyo na walitoa cheti cha ubora wa kuendelea kuzalisha nyingine kwa kiwango kinachotakiwa.
“Nachofahamu ni kwamba kulikuwa na makubaliano na TBS kuhusu ubora wa juisi hizi, tulikubali kuzalisha nyingine badala ya hizi,” alisema Dewji.
“Njoo nikuonyeshe vyeti vya TBS, tayari wametupa maelekezo tuliyaelewa na cheti cha kuthibitisha ubora wa juisi hiyo tayari wametupatia,” alisema Dewij.
Akifafanua zaidi Ofisa Viwango wa TBS, Zena Issa alisema kwa kawaida kinywaji cha aina hiyo, kinapaswa kuwa na kiasi cha sukari 10, lakini yenyewe ilipopimwa ilikutwa na kiwango 2.5.
“Pamoja na kuwa kwenye hali hiyo, bado juisi hii siyo sumu kwa watumiaji, ila ilipaswa kuwa na kiwango kinachokubalika cha sukari kama taratibu za ubora zinavyoonyesha,” alisema.
Aliongeza: “Kwa kuwa bidhaa hii inatumika zaidi na watoto pengine na wagonjwa, ilipaswa kuwa na virutubisho vitarajiwa kwa mnywaji, siyo hii ambayo ni kama maji yaliyowekwa rangi na ladha tu basi,” alisema.
Mwanasheria wa shirika hilo, Baptista Bitao alipohojiwa ni adhabu gani wanazokusudia kuchukua dhidi ya kampuni hiyo, alijibu kwamba Sheria ya Viwango namba 2 ya mwaka 2009 inaeleza wazi hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.
“Kuna sheria husika kwa makosa kama haya ya kuzalisha bidhaa chini ya kiwango kinachohitajika,” alisema Bitao.

0 comments: