Jehova Wanyanyi
Wahenga walisema; “duniani kuna mambo.” Jamaa mmoja aliyejiita
‘mungu’ huko nchini Kenya, Jehova Wanyanyi amefariki duniani na kuacha
wake 35 na watoto zaidi ya 95.
Wanyonyi alizaliwa mwaka 1924 magharibi mwa Kenya, karibu na Mlima Elgon ambako anatambuliwa kama Mlima Sayuni.
Wanafamilia
na waumini wa kiongozi huyo wa dini aliyoianzisha na kuiongoza,
wanasisitiza kuwa ‘mungu’ wao bado yupo hai, ingawa uongozi wa Serikali
ya kijiji alichokuwa akiishi unasema Wanyanyi alifariki dunia Julai 18
mwaka huu.
Taarifa za kufariki dunia kwa Wanyanyi
zilianza kusambaa tangu Julai mwaka huu, lakini ndugu zake walikuwa
wakisisitiza kuwa mungu wao hajafa na kwamba hakuna mwenye mamlaka ya
kuhoji mahali alipo.
Baadhi ya viongozi katika eneo
alilokuwa akiishi Wanyonyi wanasema kuwa ‘mungu’ huyo alifariki dunia
akiwa njiani kupelekwa katika Hospitali ya Kitale baada ya kuzidiwa.
“Wanafamilia
walikuja kwangu kuomba kibali cha mazishi, baada ya aliyejiita Jehova
Wanyonyi kushikwa na ugonjwa akiwa njiani kwenda Cherangany Nursing Home
Kitale mjini,” alisema Chifu Kipsomba Daniel Busienei alipozungumza na
gazeti la The Standard la Kenya.
Chifu Busienei alisema
wanafamilia walikwendea kumwomba kibali ya mazishi ili waende hospitali
wakachukue mwili wa Wanyonyi kwa kuwa wasingekabidhiwa maiti hiyo bila
ya kuwa na kibali hicho.
“Nilimwambia msaidizi wangu awape kibali, waende wakampumzishe Wanyonyi,” alisema Chied Busienei.
Msaidizi
wa chifu, Paul Bett anathibitisha kuwa alitoa kibali kwa familia hiyo
Julai 19, siku moja baada ya uvumi kuenea kuwa Wanyonyi amefariki dunia.
“Alifariki
dunia Julai 18, akiwa njiani kuelekea hospitali na kijana wake ndiye
aliyekuja kuomba kibali siku iliyofuata,” alisema Bett.
Wiki
mbili zilizopita vyombo vya habari vilizuiliwa kuingia katika makazi ya
Wanyanyi yaliyopo katika Kijiji cha Chemororoch, Jimbo la Soy kwa
maelezo kwamba ‘mungu’ wao alikuwa mzima wa afya.
Waandishi
hao walifika katika eneo hilo baada ya kupata taarifa kuwa Wanyonyi
amefariki dunia. Baadhi ya wanafamilia wakiwamo watoto na wake zao,
walisema kuwa mungu wao mwenye enzi alikuwa salama.
Awali,
ilielezwa kuwa Jehova amelazwa katika Hospitali ya Cherangany kabla ya
kusafirishwa kwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Moi huko Eldoret.
Hata
hivyo, utata wa kifo hicho uliongezeka baada ya waandishi wa habari
kushindwa kuliona jina la ‘mungu’ huyo katika orodha ya majina ya watu
waliokuwa wamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Utata
wa kifo cha mungu huyo aliyekuwa kiongozi wa huduma ya Lost Israelites
of Kenya, yenye wafuasi wengi katika mpaka wa majimbo ya Uasin Gishu na
Kakamega, ulichochewa na maoni tofauti yaliyokuwa yakitolewa na watu
mbalimbali.
Msemaji wa familia ya kiongozi huyo, Eliab
Masinde aliendelea kukanusha kuwa mauti imemchukua mungu wao, licha ya
uongozi kuthibitisha kifo hicho.
Masinde alisema:
“Jehova ni mzima, ingawa hali yake si nzuri sana, amelazwa katika moja
ya hospitali jijini Nairobi akipatiwa matibabu kwa usimamizi wa watoto
wake wawili.”
“Alikuwa na maumivu ya mgongo kwa muda
mrefu, lakini alipelekwa hospitali na watoto wake huko Nairobi. Mungu
huwa hafi, kama angekuwa amekufa, tungeshapata taarifa,” alisema
Masinde.
Msemaji huyo wa familia ambaye pia ni
mwangalizi wa madhabahu wa huduma hiyo, alisema majirani wa Wanyonyi
waliomwona alipokuwa akipelekwa hospitali ndio walioeneza uvumi wa kifo
chake.
Mkazi mmoja wa kijijini hapo, ambaye hakutaka
kutaja jina kwa kuihofia familia ya mungu huyo, alisema kiongozi huyo
alifariki ingawa wanafamilia wanaficha suala hilo.
“Jehova
alikuwa ana maumivu ya mgongo kwa muda mrefu, alikuwa anatembelea kiti
cha magurudumu kabla hajatoweka. Alikuwa ni mzee na tunachokijua,
familia inatawa kumweka mrithi wake kwa siri,” alisema.
Anaongeza kuwa Jehova ana wafuasi wengine nchini Uganda na kwamba inawezekana mwili wake umepelekwa huko kwa ajili ya mazishi.
Tangu
taarifa za kifo hicho kutolewa, waumini wengi wamekuwa wakifika
nyumbani kwa kiongozi wanayemtaja kuwa ni ‘mungu aliye hai’ kumwombea
ili apate nafuu haraka.
Baadhi ya wananchi wamekuwa na maoni tofauti kuhusu kifo hicho, huku wengine wakisema haiwezekani mungu kufariki dunia.
John
Paul alisema kupitia mtandao kuwa: “Inakuwaje mungu akafa au kuugua?
Kama kweli alikuwa mungu, hakupaswa hata kuugua, achilia mbali kifo.”
Wanavyoabudu
Waumini
wa Wanyanyi, husujudu mbele yake na kuomba wanachotaka. Mwandishi wa
BBC, Muliro Terewa aliingia katika kanisa hilo na kumsikia muumini
akisali:
“Mungu mkuu, uliyekuwepo, upo na utakuwepo
Jehova. Wewe ndiye aliyezungumzwa kwenye Biblia katika Kitabu cha Isaya
11. Tunakuheshimu kwa sababu kama ulivyosema mwisho umekaribia, tunaomba
utuongoze kwenda mbinguni.”
Akihojiwa na BBC, Wanyonyi
alisema:”Mimi ni masikini nina watoto 95 wa kuwalisha. Waangalie watoto
hawa, hawajala kitu chochote asubuhi hii, nahitaji dola 13 (Sh26, 000)
niwanunulie mikate.”
‘Mungu’ huyo alisema aliingia kwenye mwili wa mwanadamu miaka mingi iliyopita kama ilivyoandikwa katika vitabu vitakatifu.
Aliongeza:
“Jehova nilimtuma mwana wangu kuwaokoa watu wake lakini wanakataa,
hivyo nimeamua kuja mwenyewe labda watu wanaweza kuacha uovu wao.”
Alihadharisha kuwa kama hawatakubali na kubadilika, ataagiza moto kutoka
mbinguni uwachome, lakini wanaoamini kuwa yeye ni mungu hawataungua.
Waumini
wa Wanyanyi wanasema wameshuhudia ‘mungu’ wao akifanya miujiza, ukiwamo
ule wa mume na mke waliokuwa wakiugua Ukimwi kupona kabisa.
Hata
hivyo, wakati waumini wake wakipaza sauti kuwa Wanyonyi ni ‘mungu’,
baadhi ya watu walitishia kumuua iwapo wangemtia mikononi mwao.
“Wanyonyi ni nabii wa uongo. Ni miongoni mwa manabii wa uongo waliosemwa kwenye Biblia,” alisema Mchungaji Julius Makona.
Patrick
Busolo alisema: “Wanyanyi siyo Mungu, anajikusanyia mali tu kwa kutumia
imani aliyowajengea waumini wake. Anawalazimisha watu wamfanyie kazi
ili aweze kuishi vizuri.”
Wanyanyi alisema kuwa aliuteremsha Ukimwi duniani kama adhabu kwa wanadamu wanaodharau amri za Mungu.
Wakati
ikithibitika kuwa ‘mungu’ Wanyanyi amefariki dunia, kazi iliyobaki ni
kwa waumini wake kumteua kiongozi mwingine atakayesimamia mamia ya
waumini wa dhehebu hilo.
Pia, itakumbukwa kwamba,
‘mungu’ huyo alikuwa akisisitiza kwamba hakuna Mungu mwingine isipokuwa
yeye pekee aliyeumba vitu vyote. Kiongozi ajaye atasema ametoka wapi?
Bila shaka jibu wanalo waumini wa The Lost Israelites, wanaoomboleza kifo cha ‘mungu’ wao.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment