Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa
Wakati kukiwa na taarifa zinazosambaa mtandaoni zikimuhusisha Dk
Willibrod Slaa na akaunti ambayo imekuwa ikitoa msimamo wake wa
kujitenga na shughuli za siasa pamoja na Ukawa, katibu huyo mkuu wa
Chadema amekanusha taarifa hizo akisema hajawahi kuwa na akaunti ya
twitter.
Hii ni mara ya pili kwa Dk Slaa kuzungumza na
gazeti hili, lakini akikatakaa kufafanua mambo mbalimbali yanayohusu
sakata lake na Chadema, akiahidi kuwa kufanya hivyo baadaye, huku
akiweka bayana kuwa hajawahi kuwa na akaunti ya twitter.
Dk
Slaa, aliyekuwa anatajwa kuwa mgombea urais wa Chadema, hajaonekana
hadharani katika matukio makubwa ya kichama tangu Chadema na Ukawa
walipomkaribisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kumteua kuwa
mgombea urais anayeungwa mkono na vyama vinne vinavyounda umoja huo.
Mara
ya mwisho kuonekana kwenye shughuli za chama hicho ni katika kikao cha
Kamati Kuu wakati Lowassa alikaribishwa kufanya majadiliano na kujibu
hoja za wajumbe.
Lakini baada ya hapo Dk Slaa
hakuonekana wakati wa kutambulishwa kwa Lowassa kwa waandishi wa habari,
tukio la kuchukua na kurudisha fomu za urais ndani ya chama na tukio la
juzi la kuchukua fomu za urais kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Wakati
hayo yakiendelea, kuna akaunti ya twitter yenye jina la “Dr Willibrord
Slaa” ambayo imekuwa ikitoa kauli mfululizo zikiwa na ujumbe mbalimbali
unaoendana na mazingira aliyomo sasa mwanasiasa huyo.
Agosti 10, kulitumwa ujumbe zaidi mara 10, mmojawapo ukijaribu kuwaaminisha watu kuwa hiyo ni akaunti halisi ya Dk Slaa.
“Ndugu
zangu Watanzania, hii ni akaunti yangu rasmi, bila shaka yoyote na
naomba ninachoandika hapa kifikishwe kwa Watanzania popote walipo,”
unasema ujumbe huo.
Taarifa nyingine zilizotumwa kwenye
akaunti hiyo ya twitter ni pamoja na ile iliyoeleza kuwa Dk Slaa
ameomba ulinzi kutoka nchi na mashirika ya kimataifa na atazungumza
kupitia runinga na redio pindi atakapopata ulinzi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Slaa alisema hajawahi kutuma taarifa yoyote kwenye mitandao ya kijamii.
“Sijawahi ku-operate (kuendesha) kitu chochote kwenye akaunti ya twitter, sina akaunti kama hiyo,” alisema Dk Slaa.
Mbali
na kukanusha kumiliki na kuendesha akaunti hiyo, Dk Slaa alirudia kauli
yake ya wiki iliyopita kuwa atatoa msimamo wake muda muafaka
utakapofika, baada ya kuulizwa swali kuhusu hatma yake ndani ya Chadema
na kisiasa kwa ujumla.
“Subira yavuta heri, sasa ili
uipate hiyo heri unatakiwa kuvumilia. Kwa hiyo wakati ukifika
nitazungumza tu na Watanzania,” alisema.
Alipoulizwa ni
wapi alipo kwa sasa, alisema yupo Dar es Salaam anapumzika, lakini
akasisitiza kuwa ipo siku ataweka wazi mustakabali wake kisiasa.
Dk
Slaa alisema yeye na mke wake Josephine Mushumbusi wanatarajia kusafiri
kwenda nje ya nchi katika siku chache zijazo, ingawa hakuweka wazi nchi
anayotarajia kuitembelea, lakini akasema atarejea baada ya wiki moja.
0 comments:
Post a Comment