Kamishna wa Dawa za Kulevya, Alfred Nzowa.
Maofisa uhamiaji wa Uwanja wa Ndege wa Mumbai, India wamemkamata
Mtanzania, Fatma Chambo Basil akiwa na kilo 74 za dawa za kulevya aina
ya methaqualone alizokuwa akizisafirisha kuleta nchini.
Kwa
mujibu wa tovuti ya Gazeti la Indian Post, kiasi hicho cha dawa za
kulevya ni kikubwa kuliko vyote vilivyowahi kukamatwa katika uwanja huo
wa ndege.
Kamishna wa Uhamiaji wa Mumbai, Milind
Lanjewar alisema Chambo alikamatwa jana kwa kukiuka Sheria ya Kuzuia
Usafirishwaji wa Dawa za Kulevya ya India.
Kamishna Lanjewar alisema Chambo alikamatwa akiwa anaelekea Dar es Salaam kwa kutumia ndege ya shirika la Qatar.
“Alikamatwa
baada ya upekuzi na uchunguzi wa kina kwenye mizigo yake, uchunguzi huo
ulisaidia kugundua dawa hizo aina ya methaqualone,” Lanjewar alisema.
Akizungumzia
kukamatwa kwa Chambo, Kamishna wa Dawa za Kulevya, Alfred Nzowa alisema
hana taarifa kuhusu tukio hilo lakini akaahidi kufuatilia jinsi
alivyoondoka nchini na kupeleleza taarifa zake zote ikiwamo anakoishi,
hati yake ya kusafiria na nyendo zake.
“Huo ni mzigo
mkubwa, ni kiasi kikubwa cha dawa za kulevya. Sisi huwa tunawaonya kila
siku kuhusu kubeba dawa za kulevya na sasa wanakamatwa nchi nyingine,”
alisema.
Kadhalika, Nzowa alisema imezuka tabia kwa
Watanzania kuvuka na kwenda India kununua dawa za kulevya aina ya
ephedrine na methaqualone na kisha kuzileta nchini kabla ya kuzipeleka
Afrika Kusini.
Alisema dawa hizo zinalimwa na
kuzalishwa India kwa ajili ya matumizi ya tiba lakini watu wamekuwa
wakizitumia vibaya kama dawa za kulevya.
Akizungumzia
hali ya dawa za kulevya nchini, Nzowa alisema juhudi zinafanywa na
kitengo chake kuhakikisha nguli wa biashara hiyo wanakamatwa ili
kuumaliza kabisa mtandao huo.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment