Wananchi wa Unguja wakimshangilia mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,
Edward Lowassa alipokuwa akiwahutubia katika mkutano wa hadhara
yuliofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti, Zanzibar jana.
Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
vimetangaza mgawanyo wa majimbo 253 kati ya 265 ya ubunge huku 12
yaliyokuwa kwenye mvutano yakibaki kiporo.
Katika
mgawanyo huo uliotangazwa kwa wanahabari jana, Chadema kimepata majimbo
138, sawa na asilimia 73 ya majimbo yote huku CUF ikichukua 99, NCCR –
Mageuzi 14 na NLD matatu.
Hiyo ni pamoja na kujumlisha majimbo 51 ya Zanzibar ambayo yote yalikwenda kwa CUF isipokuwa moja lililoachwa kwa Chadema.
Mgawanyo
huo ambao umechapishwa katika ukurasa wa 36 wa gazeti hili, umetangazwa
wakati mgombea urais wa Ukawa akihutubia mkutano wake wa nne wa
kujitambulisha kwa wananchi katika Uwanja wa Demokrasia, Kibandamaiti,
Zanzibar; baada ya kufanya hivyo katika mikoa ya Mbeya, Arusha na
Mwanza.
Majimbo hayo yalitangazwa na wawakilishi wa
makatibu wakuu wa umoja, John Mnyika (Chadema), Nderakindo Kessy (NCCR –
Mageuzi), Shaweji Mketo (CUF) na Masudi Makujunga (NLD) waliokutana
katika Ofisi za Makao Makuu ya za NCCR – Mageuzi.
Miongoni
mwa majimbo ambayo hayajagawanywa ni, Segerea, Kigamboni, Mbarali,
Geita Vijijini, Gairo, Mtwara, Mpwapwa na Geita Mjini, Mwanga na
Serengeti ambalo Katibu Mkuu wa NCCR – Mageuzi, Mosena Nyambabe jana
alichukua fomu kuliwania.
Taswira ya mgawanyo
Chadema
ambacho katika uchaguzi uliopita kilipata majimbo 24 dhidi ya manne ya
NCCR-Mageuzi na mawili ya CUF Bara, kimeachiwa majimbo karibu yote
katika mikoa ya Mara, Shinyanga, Geita, Njombe, Rukwa, Arusha, Manyara,
Singida, Katavi huku Cuf ikibeba mkoa wote wa Lindi na NCCR-Mageuzi
ikibeba ngome ya Kigoma.
Katika mgawanyo huo, NLD
ambayo haikuwa na jimbo hata moja imeachiwa majimbo matatu tu ya
Lulindi, Masasi na Ndanda mkoani Mtwara.
Katika mkutano
huo, Kessy alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya majadiliano ya muda
mrefu, kuhusu kuachiana majimbo ya ubunge kwa vyama vinavyounda Ukawa.
Mnyika
alisema katika uchukuaji wa fomu za Tume ya Uchaguzi, hatatambuliwa
mgombea kutoka vyama hivyo, nje ya makubaliano yaliyofikiwa na Ukawa.
Akizungumzia mvutano wa baadhi ya majimbo, mfano Segerea, Mnyika alisema wananchi wanatakiwa kuvuta subira.
Vigezo
Mketo
alitaja vigezo sita vilivyotumika katika mgawanyo huo kwa chama husika
kuwa ni matokeo ya Uchaguzi wa Serikali Mitaa, matokeo ya Uchaguzi Mkuu
wa 2010, kukubalika kwa mgombea, hali ya kisiasa ndani ya jimbo na
mtandao wa chama husika.
“Taarifa hii ni rasmi kutoka
CUF kwani kila chama kilitoa mapendekezo ya majimbo ndani ya vikao vya
Ukawa na yalijadiliwa kupima vigezo hivyo kwa hivyo tunaomba viongozi
wote waheshimu uamuzi uliofikiwa,” alisema Mketo.
Agosti
2014, viongozi wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa walisaini makubaliano
(MoU) ya kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na
urais wa Muungano na Rais wa Zanzibar.
Lowassa Zanzibar
Wakati
huohuo, mgombea urais kupitia Chadema na Ukawa, Edward Lowassa jana
alitambulishwa Zanzibar na kusema umefika wakati wa kuikomboa nchi dhidi
ya mfumo kandamizi wa CCM.
Alisema jukumu la awali ni kuiondoa CCM madarakani na kutoa nafasi kwa rais kupitia Ukawa ili kuikwamua Tanzania kimaendeleo.
“Mkituchagua
mimi na Maalim Seif (mgombea urais wa Zanzibar) mtaiona Tanzania
inakwenda kasi ya ajabu, haijawahi kutokea. Hatuwezi kushindwa na
Rwanda! Hatuwezi kuachwa na Malawi! Hatuwezi kushindwa na Kenya na
Uganda! Tupeni nafasi tuikwamue nchi yetu kutokana na ufukara na
umaskini,” alisema.
Kama ilivyokuwa katika mikoa ya
Mbeya, Arusha na Mwanza, Lowassa alionya kuhusu mwenendo aliouita wa
hujuma na ubadhirifu wa CCM hasa katika uchaguzi, akisisitiza kuwa
hakuna msaada wowote wa kukinusuru chama hicho kikongwe kwa sasa
kisiondoke madarakani kwa kuwa muda wake umekwisha.
“Ninawasihi
ndugu zangu wale mliobaki CCM njooni haraka muungane nasi kuikomboa
nchi hii, wakati ni huu, hakuna namna ya kuzuia wimbi hili la umma
katika safari hii ambayo inaelekea katika ushindi wa kihistoria na
mwisho wa utawala wa CCM,” aliongeza.
Lowassa aliweka
msisitizo juu ya azma ya kusimamia kikamilifu mapendekezo ya Katiba kwa
mujibu wa maoni ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Jaji
Joseph Warioba.
“Hatuhitaji kusimama na batili ambayo
haikuwa chaguo wala mapendekezo ya wananchi walio wengi, tutalinda
masilahi ya Zanzibar katika Muungano kama nchi kamili yenye heshima
yake,” alisema Lowassa.
Alisema iwapo atachaguliwa, Serikali yake itahakikisha haki za masheikh waliopo kizuizini zinapatikana haraka iwezekanavyo.
Mgombea
mwenza, Juma Duni Haji alisema upepo mkali wa mabadiliko na nguvu
isiyozuilika ya Ukawa dhidi ya CCM ni ujumbe tosha kwamba mwisho wa
chama hicho umewadia.
“Someni yaliyojiri Urusi,
Ukraine, Misri na kila pembe ya mabadiliko duniani, muangalie ni wapi
dola iliposhinda nguvu za umma,” alihoji Duni ambaye hivi karibuni
alijivua uanachama wa CUF, alikokuwa Makamu Mwenyekiti na pia kujiuzulu
uwaziri katika Baraza la Mawaziri Zanzibar.
Maalim Seif
Akizungumza
katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad
alimtahadharisha Rais Jakaya Kikwete juu ya matumizi mabaya ya vyombo
vya dola.
“Ndugu yangu, rafiki yangu kipenzi, Rais
Kikwete nakuomba umechukua nchi kwa amani ondoka kwa amani,” alisema
huku akilaumu tabia ya watu aliowaita “Janjaweed”, waliodaiwa kumpora
Abdi Seif Hamad fomu ya kugombea Ubunge kupitia CUF katika Jimbo la
Shaurimoyo jana.
Abdi ni miongoni mwa watu waliohama CCM siku za karibuni na kujiunga CUF kwa matarajio ya kuungwa mkono na Ukawa.
Mamia
ya mashabiki jamii wa Kimasai walimiminika katika Uwanja wa Ndege wa
Abeid Amani Karume kumlaki Lowassa na katika hali ambayo haikuzoeleka,
walionekana kupiga saluti wakiwa wamejipanga barabarani wakati msafara
wa viongozi wa Ukawa ukipita Barabara ya Kiembe Samaki, Mwanakwerekwe
kuelekea Kibandamaiti.
Wamasai hao walimiminika kwa
wingi uwanjani hapo na kupata fursa ya kuburudisha umati wa watu kwa
wimbo wa Kimasai wenye maana ya ‘tunampenda Lowassa’.
Freeman Mbowe
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe alisema safari ya Ukawa ni ndefu, imepitia
majaribu mengi lakini bado umoja huo uko imara hivyo wananchi hawana
budi kujitokeza kwa wingi kuunga mkono umoja huo kuelekea ukombozi wa
pili wa Tanzania.
“Ndugu zangu tumetoka mbali
tutasimama imara kuhakikisha safari yetu inafikia tunakohitaji katika
mafanikio na ushindi na hatimaye kushika uongozi wa nchi,” alisema.
James Mbatia
Mwenyekiti
wa NCCR, Mageuzi, James Mbatia alisema: “Tumeshawaagiza mawakili wetu
kurekodi kila tukio kila udhalimu na kila uonevu, tunamuomba Bensouda
(Fatou, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa) kufutilia namna
zote za uvunjaji wa haki na ifikapo Novemba tunampeleka yeyote ICC.”
Khamis Mgeja
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja aliwahamasisha
Wana-CCM kujiunga na Ukawa na kumpigia kura Lowassa, wakielewa kwamba
hatima ya chama hicho kikongwe imewadia.
Wengine wachukua fomu za uraisi
Wakati
mkutano wa Ukawa ukiendelea, wagombea wengine wa urais Zanzibar
walijitokeza jana katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)
kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo.
Waliojitokeza ni
Juma Ali Khatib wa Tadea na Said Soud Said wa Chama cha Wakulima (AFP).
Khatib ni Katibu Mkuu wa Tadea na Soud ni mwenyekiti wa AFP.
Imeandikwa na Kelvin Matandiko, Borrice Bwire (Dar) na Hussein Ali (Zanzibar).
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment