Ofisa Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), George Kashura
(kushoto) akimkabidhi Katibu Mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo, Samson
Mwigamba fomu za uteuzi wa mgombea urais na makamu wa rais kwa niaba ya
wagombea wa nafasi hizo kupitia chama hicho, Dar es Salaam jana.
Sintofahamu imetanda ndani ya Chama cha ACT – Wazalendo juu ya
hatima ya mgombea wa urais baada ya mgombea aliyependekezwa na
kuchukuliwa fomu ya kuomba uteuzi, Profesa Kitila Mkumbo kuikataa nafasi
hiyo.
Mapema jana saa 4.30 asubuhi, Katibu Mkuu wa
chama hicho, Samson Mwigamba alitinga katika Ofisi za Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu bila ya kuwa na Profesa Kitila na kueleza
kuwa mgombea wao huyo yupo safarini.
Mwigamba alisema
alikwenda kuchukua fomu hiyo kwa niaba ya chama na bila kusindikizwa na
viongozi wengine kwa kuwa walikuwa kwenye vikao vya ndani vilivyokuwa
vikiendelea.
Muda mfupi baada ya Mwigamba kuchukua fomu
hizo, Profesa Mkumbo aliandika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa
anawashukuru makada na Kamati Kuu ya chama hicho kumwamini na kumtaka
agombee urais lakini kwa sasa hayupo tayari.
Katika
ujumbe huo ambao baadaye alikiri kuuandika, Profesa Mkumbo alisema
Kamati Kuu ilituma ujumbe maalumu nyumbani kwake juzi kuzungumza na
familia na jamaa zake juu ya ombi hilo na kubainisha kuwa amekuwa
akitafakari uwezekano wa kugombea nafasi hiyo baada ya juhudi za
kutafuta mgombea kushindikana.
“Nimefanya mawasiliano
mapana katika familia, ndani ya chama, chuoni ninapofanyia kazi,
kanisani kwangu na kwa watu na taasisi mbalimbali ninazohusiana nazo.
“Baada
ya tafakari na mawasiliano mapana, nasikitika kusema kwamba sina
utayari na maandalizi ya maana ya kisaikolojia, kifamilia na kisiasa
kuniwezesha kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi huu,” alisema
Profesa Mkumbo.
Alisema anajua bayana amewaangusha
lakini anaamini kwamba wafuasi hao wataheshimu uamuzi wake, hivyo
hawataacha kuthamini mchango alioutoa katika chama hicho kwa sababu
amekataa kugombea urais.
Alishauri chama kiwaombe
wanachama wengine waandamizi kuchukua jukumu hilo, akiwamo Mwenyekiti,
Anna Mghwira, huku akiwataka makada wa ACT –Wazalendo kutomtuhumu kwa
lolote juu ya uamuzi wake.
Kukataa kwa Profesa Mkumbo
kunakipa kazi chama hicho kutafuta mbadala wa mgombea huyo ambaye ni
moja ya waasisi wa chama hicho chenye makao yake makuu, Kijitonyama
jijini hapa.
Hata hivyo, Mwigamba alipoulizwa mbadala
baada ya mgombea waliyemchukulia fomu kukataa, alisema hawadhani kuwa
Profesa Mkumbo atakataa na ikitokea hivyo watamtafuta kada mwingine
agombee.
“Mwigamba alisema mgombea mwenza aliyetarajiwa ni kada wa muda mrefu wa ACT – Wazalendo aitwaye Hawra Shamte.
Alipotakiwa
kueleza kwa kina iwapo jina la mgombea mwenza huyo ni linahusiana na
Mhariri wa gazeti hili, Hawra Shamte, Mwigamba alisema: “Siyo huyo na
kiufupi yeye (mgombe mwenza) na mgombea urais tutawatangaza baada ya
kikao cha dharura cha Kamati ya Uongozi kukamilika leo (jana) au kesho
(leo).”
Shamte alipoulizwa kuhusu mpango huo, alisema
hajui jambo hilo na kwamba jina hilo huenda halihusiani naye kwa kuwa
yeye si mwanachama wa chama chochote.
Makada wavamia ACT
Baada
ya taarifa ya Profesa Mkumbo kukataa kuzagaa, makada zaidi ya 200 wa
ACT – Wazalendo walitinga katika ofisi cha chama hicho wakiwa katika
maandamano wakishinikiza agombee.
Maandamano hayo
yalianzia jirani na Ofisi ya Tume ya Sayansi na Teknolojia Kijitonyama,
wilayani Kinondoni hadi katika ofisi za chama hicho zilizopo umbali wa
kilomita moja.
Waandamanaji hao wakiwa na bendera za
chama hicho walifika katika ofisi za chama hicho saa 6.10 mchana na
kutishia kuvunja mlango wa ofisi lakini walizuiwa na wenzao waliokuwa
ofisini.
Baada ya azma hiyo kushindwa, waliendelea
kuimba nyimbo mbalimbali za kumshinikiza Profesa Mkumbo kuwania urais
huku wakiwa na mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali ukiwamo “…Bora
ofisi ifungwe kama hatuwezi kusimamisha mgombea urais.”
Wengi
wa waandamanaji hao ambao ni vijana kati ya miaka 20 na 30 waliendelea
kuimba: “Zitto na Kitila turudishieni chama chetu kama mmeshindwa kuweka
mgombea urais. Kitila Mkumbo tumia busara na hekima wewe ni rais 2015.”
Katika
hali ya kushangaza, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Shaaban Mambo
aliingia katika ofisi hizo saa 6.30 mchana na kupokewa kwa shangwe na
vijana ambao waliimba huku wakisema, “karibu Profesa Kitila, Kitila,
Kitila.”
Baada ya Mambo kuingia ndani, ndipo baadhi ya vijana wakaanza kuwaeleza wenzao kuwa yule hakuwa Profesa Kitila.
Baadaye
ofisi za chama hicho ziligeuka ‘uwanja wa vita’ kwa vijana hao baada ya
kuanza kugombania maji na biskuti zilizokuwa zikitolewa katika ofisi
hiyo.
Mmoja wa wafuasi wa chama hicho aliyekuwa akigawa
vinywaji hivyo alishindwa kuhimili vurugu za vijana hao na kuamua
kuwarushia juu chupa za maji na biskuti.
0 comments:
Post a Comment