Mazungumzo kuhusu siasa na hasa Uchaguzi Mkuu, idadi ya watu
waliojitokeza kujiandikisha kupiga kura na idadi kubwa ya watu
wanaojitokeza kwenye mikutano ya hadhara ya wanasiasa ndiyo hali
iliyoenea kila kona ya nchi kwa sasa, kitu ambacho wachambuzi
waliohojiwa na gazeti hili wamekielezea kuwa ni kuongezeka kwa mwamko wa
wananchi katika masuala ya siasa.
Wachambuzi hao,
ambao waliohojiwa na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wameeleza kuwa
mwamko huo pia unatokana wananchi kutaka mabadiliko, uamuzi wa kada wa
CCM, Edward Lowassa kuhamia Chadema na umoja wa vyama vya upinzani
ambavyo vimeamua kuunganisha nguvu kwenye uchaguzi, kitu ambacho
kimewafanya wananchi waone kunaweza kuwa na ushindani wa kweli safari
hii.
Tangu mchakato wa uchaguzi uanze ndani ya vyama,
mazungumzo ya wananchi wa kawaida kwenye mikusanyiko mbalimbali kama
sokoni, maskani, kwenye vyombo vya usafiri na mitandao ya jamii imekuwa
ikitawaliwa na siasa na hasa baada ya CCM kuanza kutafuta mgombea wake
wa urais.
Ufuatiliaji huo wa habari za siasa
uliongezeka zaidi baada ya kumteua Dk John Pombe Magufuli kuwania urais
kwa tiketi ya chama hicho tawala na jina la Lowassa kutoingia tano bora,
kitu kilichomfanya atangaze kujivua uanachama na kuhamia Chadema.
Wanasiasa
hao wawili pia wamevuta maelfu ya watu kwenye mikutano yao ya
kutambulishwa kwa wanachama, kutangaza kuhama chama na kuchukua fomu za
kuwania urais, huku mbunge wa zamani wa Chadema, Zitto Kabwe akivuta
mamia ya watu kwenye mikutano yake ya kukitangaza chama kipya cha ACT
Wazalendo.
Idadi ya watu wanaotangaza kuhama chama
kimoja na kwenda kingine imekuwa ikiibua mijadala mara kwa mara, huku
bendera za vyama vikuu vya kisiasa—CCM, Chadema, CUF na NCCR
Mageuzi—zikipepea maeneo mengi.
Wakati mwaka 2010
waliojiandikisha kupiga kura mwaka 2010 walikuwa milioni 11.5, mwaka huu
idadi inaweza kuwa maradufu baada ya makisio ya watu waliotarajiwa
kujitokeza kujiandikisha kuwa milioni 24 huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) ikieleza kuwa imefikia idadi iliyotarajiwa au kupita malengo
kwenye baadhi ya mikoa.
Pamoja na ukweli kwamba kipindi
cha kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25 kinatakiwa
kitawaliwe na habari na mijadala ya kisiasa, wachambuzi wanazungumzia
mwamko wa mwaka huu kuwa ni mkubwa zaidi kulinganisha na chaguzi
zilizopita.
Kauli za wasomi
Akizungumza
na Mwananchi kuhusu hali hiyo ya siasa kushika nafasi kubwa katika
mijadala mbalimbali, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu Kishiriki
cha Ruaha (Ruco) alisema wananchi sasa wameamka na kutambua haki yao ya
kupigakura, na hivyo wanataka kuitumia kudai mabadiliko waliyoyakosa kwa
muda mrefu.
“Kuongezeka kwa umasikini, vijana kukosa
ajira, ufisadi na kuongezeka kwa rushwa kumewaamsha wananchi kwa kiasi
kikubwa na kuamka kwao kunatokana na kukua wa utandawazi,” alisema
Profesa Mpangala.
“Ukiongea na wananchi wengi,
wanakwambia kuwa wanataka mabadiliko. Wana matatizo mengi na wanaamini
kuwa wakichagua kiongozi mzuri anaweza kuondoa matatizo yanayowakabili.”
Hata
hivyo, Profesa Mpangala alisema tatizo lililopo ni wananchi kuamini
kuwa mtu mmoja ataweza kuwaletea mabadiliko na kusahau kuwa mabadiliko
watayaleta wenyewe, akieleza kuwa ili mabadiliko yatokee ni lazima
kubadilisha mfumo wa utawala.
“Wanatakiwa kutazama
mfumo maana chama kitakachoingia Ikulu kitaweza kuleta mabadiliko kama
mfumo wa utawala utakuwa mzuri. Chama kinaweza kuwa na mgombea mzuri,
lakini akashindwa kuleta kipya kwa sababu ya mfumo,” alisema.
Kauli
ya Profesa Mpangala juu ya Watanzania kutaka mabadiliko inaungwa mkono
na Richard Mbunda ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), ambaye alisema mwamko huo pia unatokana na ugumu wa maisha kwa
watu wengi.
“Ninatembea maeneo mbalimbali ya nchi yetu
na kuzungumza na watu. Nilichokibaini ni wananchi kuchoshwa na maisha
wanayoishi. Wanahoji wazi iweje maisha yao yawe duni na ya wengine yawe
ya juu. Watanzania sasa si watu wa kufuata upepo tu kama ilivyokuwa
miaka ya nyuma,” alisema Mbunda.
“Wanaona tatizo kubwa
tulilonalo ni la kimfumo na wanaamini kuwa wakichagua kiongozi wa aina
fulani hali yao ya maisha itabadilika.”
Alisema kitendo
cha Ukawa kumsimamisha Lowassa kimeibua changamoto mpya kwa sababu ni
mgombea anayekubalika na watu wengi na wengi wanaamini kuwa akiwa rais
ataweza kuwavusha.
“Hata Magufuli amefanya mengi ikiwa
ni pamoja na kujenga barabara nyingi na wananchi wanamfahamu. Wagombea
hawa wanaufanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa wa kihistoria,” alisema.
Dk
Benson Bana ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) naye
alimtaja Lowassa kama chachu inayowafanya Watanzania kujitokeza kwa
wingi kushiriki uchaguzi.
“Mabadiliko ni hali ya kutoka
katika hali uliyokuwa nayo kwenda katika hali nzuri zaidi. Watu
hawajaanza kuyataka mabadiliko leo, wamekuwa wakiyataka kila uchaguzi.
Wapo wanaomuonea huruma Lowassa na kuona kuwa dhamira yake ya kuhama CCM
kwenda Chadema ni ya kweli na kuna jambo anataka kulifanya,” alisema.
Alisema CCM imekaa madarakani kwa muda mrefu na kufikia hatua ya kujisahau, jambo ambalo linawafanya wananchi kutaka mabadiliko.
“Binadamu
siku zote hupenda mabadiliko. Hili suala la watoto wa viongozi nao
kupewa uongozi, wananchi wanaliona na linawaudhi na wanaona CCM kama
uwanja fulani hivi wa kubebana. Hawasemi tu ila wanayaona haya na
wanayatafakari,” alisema.
“Mfumo wa CCM kujiendesha
unatakiwa kutazamwa upya maana chama kineonekana kama cha (katibu mkuu
wa CCM, Abdulrahman) Kinana na (katibu wa itikadi na uenezi wa CCM),
Nape (Nnauye),” alisema na kusisitiza kuwa makamu mwenyekiti wa chama
hicho, Philip Mangula amebaki kushughulikia masuala ya nidhamu. Hivi
utapata kura kwa kushughulikia nidhamu?”
Alisema
wanachotakiwa kukifanya Watanzania ni kuzichambua sera za CCM na vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kama zinaweza kutatua
matatizo yanayowakabili, si kutazama sifa za mgombea mmoja mmoja.
“Wagombea
wote wanakuja na lugha za kuwasaidia machinga, waendesha bodaboda,
mamantilie na tatizo la ajira. Hizo ni lugha za kutafuta kura tu.
Wanachotakiwa kutueleza wagombea wote ni mkakati watakaoutumia kumaliza
matatozo hayo,” alisema.
Hoja za kuwapo mwamko pia
zilitolewa na mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala na mhadhiri wa
Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim.
“Watanzania
wanataka mabadiliko na wapo wanaodhani watayapata kupitia CCM na
wanaodhani watayapata nje ya CCM kutokana na kuyasubiri ndani ya chama
hicho tawala kwa muda mrefu,” alisema Salim.
Alisema
kitendo Lowassa kuhamia Ukawa kumeibua mihemko na ushindani mpya wa
kisiasa nchini, na kwamba hilo limekuwa moja ya sababu ya wananchi wengi
kujiandikisha.
“Ila si wote wanaojiandikisha
kupigakura watapiga kura kuchagua viongozi, wapo watakaotumia shahada
zao katika masuala yao binafsi,” alisema.
Profesa
Damiani Gabagambi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine(Sua) anaouona mwamko
huo kwa vijana waliozaliwa mwishoni mwa miaka ya tisini na mwanzoni mwa
miaka ya tisini, akisema wengi wanataka mabadiliko lakini hawajui
yataletwaje.
“Miaka ya nyuma wananchi walikuwa hawapigi
kura wakiamini kuwa nguvu ya upinzani ni ndogo, ila kitendo cha vyama
vinne kuungana na kusimamisha mgombea mmoja kimewazindua na sasa
wanauona ushindani wa kweli. Ila wapo waliojiandikisha ili wapate
shahada tu kwa matumizi mbalimbali,” alisema.
Katika
uchaguzi wa mwaka huu, watu saba wamejitokeza kuwania urais kumrithi
Rais Jakaya Kikwete ambaye amemaliza vipindi vyake viwili vya miaka
mitano kila kimoja.
Wakati CCM imemsimamisha Dk
Magufuli, vyama vinne vinavyounda Ukawa vimekubaliana kumsimamisha
Lowassa, hali inayofanya uchaguzi wa mwaka huu uonekane kuwa ni vita vya
kihistoria baina ya wawili hao.
Pia mwenyekiti wa DP,
Mchungaji Christopher Mtikila amechukua fomu za kugombea urais sambamba
na Chifu Lutayosa Yemba (ADC), Macmillan Lyimo (TLP), Hashimu Rungwe
(Chauma) na Fahami Dovutwa (UPDP).
Mgombea wa nane anatarajiwa kutoka chama kipya cha ACT Wazalendo.
chanzo: Mwananchi
chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment