Zanzibar. Mtu mmoja kati ya wannewaliolipukiwa na mabomu, Unguja Ukuu Mkoa wa Kusini Unguja, amefariki dunia na kuzikwa jana Visiwani Zanzibar. Marehemu aliyetajwa kwa jina la Juma Abdallah Juma (32), alifariki dunia kutokana na majeraha makubwa aliyopata sehemu mbalimbali mwilini.
Katibu wa Hospitali ya Mnazi Moja, HassanMakame alisema marehemu alifariki juzi jioni wakati akipatiwa matibabu kwenye hospitali hiyo.
Alisema majeruhi, Pandu Haji Pandu aliyekatika mguu amehamishiwa katika Chumba Maalumu (ICU) kutokana na majeraha makubwa aliyopata.
Majeruhi mwingine ni Shaaban Khamis Ibrahim ambaye anaendelea kupatiwa matibabu ikiwa ni pamoja na kutolewa kitu kigumu sehemu ya kiunoni kilichosababishwa na mlipuko huo.
Makame alisema majeruhi Simai Hussein Hassan alipatiwa matibabu na kuruhusiwa baada ya hali yake kuimarika.
Akizungumza na gazeti hili katika wodi ya upasuaji wa mifupa Hospitali ya Mnazi Mmoja, majeruhi Shaaban Khamis Ibrahim, alisema mkasa huo ulimpata wakati alipokwenda karibu na karakana ya uchongaji vyuma baada ya pikipiki yake kupata matatizo.
“Baada ya kazi zangu za uvuvi, niligundua pikipiki yangu ina matatizo, nikaenda gereji kuifanyia matengenezo na nilipofika jirani na wachonga vyuma, nikasikia mlipuko na kitu kizito kilikuja kunipiga kiunoni,” alisema majeruhi huyo.
Alisema madaktari walimtoa chembechembe za mabaki ya vitu mwilini, ingawa anatakiwa kufanyiwa vipimo zaidi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame alisema mtu mmoja anashikiliwa na polisi kuhusiana na matukio ya milipuko yaliojitokeza katika maeneo matatu Zanzibar.
Askofu wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, Michael Hafidh alisema vyombo vya dola vinatakiwa kuwaeleza wananchi mhusika wa vitendo vya hujuma dhidi ya makanisa Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment