DIWANI wa Kata ya Masagalu, Wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, Bw. Mohamed Makengwa, ametoa kauli ambayo ilipingwa vikali na madiwani wenzake baada ya kuishauri Serikali iache kutumia fedha nyingi kuwagharamia watu wazima walioathirika na ugonjwa wa Ukimwi akidai watu hao wamejitakia wenyewe.
Alisema Serikali inapaswa kuelekeza fedha na nguvu zake kuwalinda wanafunzi waliopo shule za msingi na sekondari kwa kuwapa elimu ya ugonjwa huo kwani wao ndio viongozi wa kesho hivyo wakiangamia Taifa litakuwa limeangamia.
Bw. Makengwa aliyasema hayo mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Ukimwi iliyosomwa na Mwenyekiti wake, Bw. Bakari Honelo ambaye ni Diwani wa Kata ya Kilwa.
"Serikali isipoteze fedha zake kwahudumia watu wazima wenye Ukimwi, inatakiwa kuelekeza nguvu zake kwa vijana wa shule za msingi na sekondari, mtu mzima akipata virusi vya ugonjwa huu amejitakia mwenyewe," alisema Bw. Makengwa.
Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa vikali na baadhi ya madiwani na kuufanya ukumbi huo kulipuka kwa mayowe wakipinga kauli hiyo ambapo diwani wa Viti Maalumu, Sophia Mhina na Mwanaisha Nyange, walidai huo ni unyanyapaa ambao haukubaliki.
Akizungumza na Majira kutokana na kauli hiyo, Bw. Makengwa alisema; "watu ni wazembe, kila siku wanatangaziwa Ukimwi unaua na hauna tiba, lakini bado hawasikii, wengine wanafanya vitendo vya ngono zembe bila kutumia kondomu.
"Kwa nini Serikali ihangaike na mtu kama huyu, ndiyo maana nataka nguvu kubwa ipelekwe kwa watoto waliopo shule, tuachane na watu wazima...mimi mwenyewe nina wake wanane na watoto 32 lakini hakuna mwenye Ukimwi," alisema.
0 comments:
Post a Comment