Kamishna Msaidizi wa Madini Mhandisi,Hamis Komba (wa pili kushoto) akiwa pamoja na Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma masomo ya Geomolojia katika Chuo cha ‘Asian Institute of Geological Science’ (AIGS) nchini Thailand. Wa kwanza kulia ni Agatha Mwinuka, anayefuata ni Emmanuel Minja na wa kwanza kushoto ni Doricas Moshi.
Wanafunzi wa Kitanzania nchini Thailand, wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wenzao kutoka mataifa mbalimbali , ambao wamelitembelea banda la Tanzania.
Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini katika picha ya pamoja na wanafunzi hao katika banda la Tanzania.
Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma masomo ya Geomolojia katika Chuo cha ‘Asian Institute of Geological Science’ (AIGS) nchini Thailand, wamewataka wadau wa tasnia ya madini ya vito na usonara nchini Tanzania kuichukua sekta hiyo kwa umakini mkubwa kutokana na mchango wake kiuchumi.
Aidha, wameeleza kuwa, nchi ya Thailand imepiga hatua kubwa katika sekta ya madini ukilinganisha na Tanzania lakini bado Tanzania inaweza kufaidika zaidi katika sekta hiyo ikiwa kila mdau atatimiza wajibu wake kikamilifu ili madini ya vito yaongeze mchango katika pato la taifa.
Wameongeza kuwa, Tanzania bado ina nafasi ya kujipanga upya kuhusu kuboresha zaidi sekta hiyo kama ilivyo kwa nchi nyingine endapo mipango mikakati ya maboresho itatekelezwa na kusimamiwa kikamilifu.
Wanafunzi hao wameyasema hayo, wakati walipolitembelea banda la Tanzania katika maonesho ya 53 ya Vito vya Usonara na Madini yanayoendelea katika jiji la Bangkok ambapo nchi zaidi ya 150 zinashiriki maonesho hayo.
“Thailand wamejipanga vizuri katika sekta ya madini. Wafanyabiashara wa madini wana umoja. Wadau wa madini wanatakiwa kuelewa kuwa madini yanawakilisha utajiri wetu tulionao”. Amesema Agatha Mwinuka.
Aidha, wameitaka serikali na wadau wa Tanzania wanaoshiriki maonesho hayo kujifunza kutokana na changamoto wanazozipata kutoka kwa nchi nyingine, jambo ambalo litasaidia kuboresha sekta ya madini na vito, ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara kuhakikisha kuwa wanafuata sheria na taratibu zilizopo.
“Tunaiomba serikali iendelee kuendeleza viwanda vya kukata madini. Ni jambo zuri kama shughuli hizi za kukata madini zitafanyika ndani ya nchi badala ya nje. Jambo hili linasaidia sana kuongeza thamani ya madini. Ameongeza, Emmanuel Minja.
Akiongelea kuhusu umuhimu wa kuendeleza na kuboresha kituo cha Tanzania Geomological Center, Doricas Moshi, ameeleza kuwa, kituo hicho kinaweza kutoa mchango mkubwa katika tasnia hii hasa katika nyanja ya ukataji madini na uthamini wa madini hivyo, ameitaka Serikali kukiongezea nguvu kituo hicho kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya Tanzania.
“Chuotunachosoma hapa kinatumia sana mifano ya madini ya Tanzania katika kufundisha. Mengi yametoka nyumbani, hii ni ishara nzuri. Serikali iliangalie hili. Ameongeza Doricas.
Aidha, wameeleza kuwa, soko la kimataifa kwa madini ya Tanzania lipo, hivyo, wamewataka wadau wote kuhakikisha wanashirikiana vizuri na serikali kuendeleza sekta hiyo kutokana na umuhimu na mchango wake kwa taifa.
Akizungumzia mipango iliyopo ya kuboresha sekta hiyo, Kamishna Msaidizi wa Madini, Mhandisi Hamis Komba, amesema kuwa, Serikali kupitia Shirika la Madini Tanzania (STAMICO), inatekeleza mikakati ya kuwasaidia wachimbaji wadogo na wa kati ili waweze kuendana na mahitaji ya soko la kimataifa kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali yakiwemo ya kukata madini, kuyaongezea thamani na kuwapatia mikopo kupitia Benki ya TIB.
“STAMICO imepewa jukumu la kuwaendeleza wachimbaji wadogo katika sekta ya madini hususani katika masuala ya uchimbaji, uongezaji thamani madini na biashara ya madini. Serikali imejipanga vizuri katika hilo”. Ameongeza Kamishana.
Ameongeza kuwa, Serikali inatambua kwamba wachimbaji wengi wapo katika sekta ya madini ya vito na usonara hivyo, jitihada za kuwaendeleza zitasaidia kufikia kiwango bora cha utendaji wao wa kazi.
Vilevile, ameongeza kuwa, kutokana na kuboreshwa kwa Sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inaiwezesha STAMICO kumiliki asilimia 50 ya hisa katika mgodi wa Tanzanite One, jambo ambalo linaifanya Serikali kuwa mmiliki katika mgodi huo.
0 comments:
Post a Comment