KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Mwanamke mmoja Mkazi wa
Mtaa wa Ilembo kata ya Iyela Jijini Mbeya amemjeruhi mume wake baada ya
kumwagia mafuta ya moto kichwani kwa kile kilichodaiwa kuwa ni mgogoro wa ndoa
baina yao.
Mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Beatrice Lusamba
(37) alitenda tukio hilo mwishoni mwa wiki majira ya saa saba mchana ambapo
alimwagia mafuta hayo Mume wake Lugano Mwambuja(50) ambaye ni mwalimu wa Shule
ya Sekondari Sange iliyopo Wilaya ya Ileje Mkoani Mbeya.
Akizungumzia tukio hilo Mhanga wa kisa hicho alisema yeye
makazi yake yako Wilayani Ileje lakini Mkewe pamoja na baadhi ya watoto wake
huishi Jijini Mbeya hivyo hufika nyumbani hapo mara chache kwa ajili ya
kutembelea familia na kupeleka huduma mbali mbali kama baba wa
familia.
alisema siku ya tukio alialikwa na Mkewe huyo kula
chakula cha mchana ambapo baada ya kukaribishwa ndani mwanamke huyo aliingia
jikoni akiwa na mayai matatu na galoni la mafuta ya kupikia, ambapo yeye alibaki
Sebureni akisubiri chakula alichokaribishwa apikiwe.
Alisema baada ya dakika kumi Mkewe huyo alirejea Sebuleni
akiwa ameshika kikombe chenye mafuta yaliyochemshwa ambayo alimwagia mwilini na
kisha kukimbilia nje akimwacha mumewe akiugulia maumivu makali yaliyotokana na
kuungua na mafuta ya moto mwilini mwake.
Mwalimu huyo aliongeza kuwa baada ya kupiga kelele ya
kuomba msaada ndipo alipojitokeza jirani yake aliyefahamika kwa jina la
Andamisye Kajange ambaye baada ya kumuona katika hali hiyo alimkimbiza katika
Hospitali ya Rufaa ya Mbeya alikopatiwa matibabu na
kuruhusiwa.
Mjumbe wa Mtaa Ilembo, Philly Mwakapimba alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa kabla ya kupeleka Hospitali Mhanga
waliripoti Kituo cha Polisi na kupewa fomu namba tatu (PF3) pamoja na kufungua
faili namba IR/2253/2014 na kuendelea kutibiwa.
Aliongeza kuwa mtuhumiwa hajakamatwa hadi leo baada ya
kutorokea kusikojulikana huku lawama likipewa Jeshi la Polisi kutokana na
kushindwa kumkamata mtuhumiwa kwa wakati hadi anapata mwanya wa kutoweka katika
eneo la tukio.
Akizungumzia mahusiano yake na mkewe Mwalimu huyo alisema
alioana na mkewe mwaka 2007 kwa ndoa ya kimila baada ya kufiwa na mkewe wa awali
mwaka 2006 alimyemwachia watoto wawili ambao ni Doris(20) na Happy Mwambuja(21)
ambapo aliamua kuoa mke huyo kwa ajili ya kusaidia malezi ya watoto
hao.
Alisema akiwa kazini mara nyingi alikuwa akipata taarifa
za mgogoro kati ya mkewe huyo na watoto jambo lililosababisha usuluhishi wa mara
kwa mara kufanyika ukiongozwa na Serikali ya Mtaa huku sababu ikibainika kuwa ni
tamaa ya mwanamke huyo kutaka kumiliki Nyumba ya Mwalimu huyo ili iwe mikononi
mwake na siyo Familia.
Alisema mara nyingi Mwanamke huyo amekuwa akijaribu kuiba
hati ya nyumba ili abadilishe majina na umiliki lakini anashindwa hali
iliyoml;azimu Mwalimu huyo kuamua kununua eneo lingine na kujenga ili
kumtengnisha mkewe pamoja na watoto lakini hali bado ilikuwa tete baada ya
mwanamke huyo kutaka amilikishwe yeye nyumba.
hadi sasa Mwalimu huyo anaendelea kupatiwa matibabu
Nyumbani kwake huku Jeshi la Polisi likiendelea kumsaka mtuhumiwa kwa ajili ya
kumfikisha katika vyombo vya sheria kujibu shtaka la kujeruhi kwa
makusudi.
|
0 comments:
Post a Comment