Mfanyakazi wa kike Eugenia John, anayefanya kazi katika duka linalouza vifaa vya simu Mtaa wa Aggrey, Kariakoo jijini Dar es Salaam anadaiwa kupigwa na kujeruhiwa hadi kuzimia na bosi wake aliyejulikana kwa jina moja la Chuwa.
Mfanyakazi wa kike Eugenia John, anayefanya kazi katika duka linalouza vifaa vya simu Mtaa wa Aggrey, Kariakoo jijini Dar es Salaam anayedaiwa kupigwa na kujeruhiwa hadi kuzimia na bosi wake Bw. Chuwa.
Chanzo chetu cha habari kinadai kwamba tukio hilo lilitokea hivi karibuni na wakati mfanyakazi huyo anapigwa imedaiwa alikuwa akilia kwa uchungu kitendo kilichowafanya majirani kufika katika eneo hilo.
Walipofika walimkuta binti huyo amezimia kutokana na kipigo jambo lililowafanya wananchi wenye hasira kali kutaka kumpiga Chuwa.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mmoja wa rafiki wa Chuwa alipoona wananchi hao wenye hasira wamemzingira mfanyabiashara huyo dukani kwake, aliamua kupiga simu polisi ambao walifika na gari aina ya ‘Land Rover Defender’ na kumuokoa kisha walimfikisha Kituo cha Msimbazi.
Habari zinadai kwamba Chuwa alipokuwa chini ya ulinzi wa polisi huku akipelekwa kituoni, mfanyakazi wake Eugenia alichukuliwa akiwa hajitambui na kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu.
Hata hivyo, kilichowashangaza wananchi ni kuwa Chuwa aliachiwa huru wakati binti huyo anapigania uhai wake hospitalini.
Majirani katika duka hilo waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa majina yao, walidai kwamba Chuwa ana kawaida ya kuwaadhibu na kuwatishia kwa bastola wafanyakazi wake pale wanapokosa au inapotokea upotevu wa fedha bila kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Kwa upande wa Eugenia inadaiwa kwamba alikuwa akiadhibiwa kwa kuchapwa na waya wa umeme ambao umeacha majeraha kibao na maumivu ya ndani kwa ndani mwilini na kwa sasa hajarejea kazini kwa madai kuwa bado hajapona.
Chuwa alipohojiwa ofisini kwake na mwandishi wetu alikiri kutokea kwa sakata hilo na kuokolewa na polisi kutokana na kutaka kushambuliwa na wananchi wenye hasira kali kwani usalama wake ulikuwa hatarini.
Hata hivyo, alikana kumpiga Eugenis na alipoulizwa kwa nini ana majeraha alisema aliumia mwenyewe akiwa dukani.
“Kwa nini unaniuliza maswali hayo wakati Eugenia ni ndugu yangu? Nisingependa mtu aingilie kati wala kuandikwa gazetini,” alisema.
Kamanda wa Kipolisi Mkoa wa Ilala, SACP Marietha Minangi alipoulizwa alisema kwamba taarifa hizo hazijamfikia mezani kwake.
“Lakini niahidi kwamba nitafuatilia ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Kamanda Minangi.
0 comments:
Post a Comment