Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete amesema ni utovu wa
nidhamu na ukosefu wa adabu unaoonyeshwa na baadhi ya Watanzania
kuwatukana, kuwadhihaki na kuwakejeli waanzilishi wa Taifa la Tanzania,
Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa
kwenye mahojiano maalumu na wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari (wa
Mwananchi hawakuwapo) ya kuadhimisha miaka 50 ya Muungano.
Kauli hiyo ilikuwa ni jibu la moja ya maswali
alilokuwa ameulizwa na wahariri hao kuhusu matusi, kejeli na dhihaka
ambazo zimekuwa zinaonyeshwa na wajumbe wachache wa Bunge Maalumu la
Katiba juu ya waasisi hao wa Tanzania na wabunifu wakuu wa Muungano wa
Tanzania.
“Ni kukosa adabu na ni utovu mkubwa wa nidhamu kwa
Mtanzania yeyote kuwatukana, kuwadhihaki au kuwakejeli waasisi wa Taifa
letu. Hawa ni watu ambao waliifanyia nchi yetu mambo makubwa,” alisema
Rais Kikwete na kuongeza:
“Mzee Karume yule aliongoza Mapinduzi yaliyoondoa
dhuluma na uonevu pale Visiwani. Waafrika walio wengi walikuwa wanaonewa
sana pale Tanzania Visiwani, pengine watu wamesahau, lakini hata pale
walipokuwa wanashinda uchaguzi, bado walikuwa hawapewi nafasi ya
kuongoza maisha yao wenyewe.”
Rais alisisitiza kuwa ni ukosefu wa adabu kwa
yeyote kumshutumu mtu aliyejitolea kiasi hicho ili kubadilisha mfumo
dhalimu na kujenga maisha na mazingira ya maisha bora kwa wengi.
“Mzee Nyerere yule ametuachia Taifa moja,
lililoungana, lenye umoja, lenye amani na mshikamano. Misingi ambayo
aliijenga yeye ndiyo imeendelea kuongoza Taifa letu kwa miaka yote hii,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment