WAJUMBE wa Bunge Maalumu, wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA), wamesema hawatarudi bungeni na badala yake kuanzia kesho
wataanza mikutano ya hadhara nchi nzima kuwaeleza wananchi juu ya hila
za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na washirika wake kutaka kuhodhi mchakato
wa uandikaji wa Katiba mpya.
UKAWA wamesema katika mikutano hiyo watazisambaza ‘CD’ zinazomuonesha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi, akiwa katika Kanisa la Methodist, mkoani Dodoma akiwaeleza
waumini wakatae muundo wa serikali tatu.
Walisema kwenye CD hizo, Lukuvi, anaonekana akiwaambia wananchi iwapo
wataridhia muundo wa serikali tatu, jeshi litachukua nchi na Zanzibar
itaingia katika utawala wa Kiislamu.
Juzi wajumbe wa UKAWA walisusia kikao cha Bunge Maalumu kwa madai ya
kuchoshwa kusikiliza matusi, ubaguzi na kauli za chuki zinazotolewa na
wajumbe kutoka CCM bila viongozi wakubwa kukemea.
Jana wakizungumza na waandishi wa habari, viongozi wa UKAWA walisema
hawatarejea bungeni mpaka watakapoketi kwenye vikao vya maridhiano
ambavyo pia watakwenda na masharti yao mojawapo ni rasimu ya Tume ya
Warioba ndiyo iwe msingi wa majadiliano.
Masharti mengine ni kukaa kwenye meza ya maridhiano na viongozi wa serikali na CCM, kusiwepo matusi, ubaguzi na kauli za chuki.
Mmoja wa viongozi wa UKAWA, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kuwa
watazunguka nchi nzima kuwaeleza wananchi kilichotokea bungeni na namna
CCM wanavyopenyeza rasimu yao kwa mlango wa nyuma.
“Sisi tupo tayari kwa mazungumzo kama tulivyoombwa na Mwenyekiti wa
Bunge Maalumu, Samuel Sitta, lakini hatutakubali kubeba matakwa ya CCM,
tunataka tujadili rasimu ya Tume ya Jaji Warioba ambayo ilikwenda
kuwahoji wananchi,” alisema.
Profesa Lipumba, alisema wameamua kususa vikao vya Bunge kwa sababu
hawako tayari kushiriki kupitisha masuala yenye masilahi ya CCM
yaliyopelekwa bungeni kwa mlango wa nyuma.
Alisema walitegemea wajumbe wangejikita kujadili rasimu
iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa hoja lakini badala
yake wameshuhudia matusi, ubaguzi, kauli za chuki ambazo zinachangia
zaidi kuligawa taifa.
Lipumba alisema rasimu iliyopo mezani inataja serikali tatu hivyo
kama wajumbe wa CCM wanataka kujadili serikali mbili, lazima Bunge
livunjwe na iundwe tume nyingine itakayotoa rasimu ya serikali mbili.
“Wenzetu wanatushangaza sana yaani walivyokuwa wakijadili rasimu ile
kama imetolewa na wapinzani, hii ni rasimu iliyotolewa na tume
iliyoundwa na rais, sasa kama wenzetu hawaamini sisi tunakwenda
kuwaeleza wananchi CCM isivyotaka kuandika Katiba yenye masilahi ya
wananchi,” alisema.
Lipumba pia alisema Chama cha Wananchi (CUF), kitaangalia hatua za
kisheria za kumchukulia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alivyokihusisha chama hicho na
taasisi ya kidini ya UAMSHO.
Alisema si kweli kwamba CUF imekuwa ikishirikiana na taasisi hiyo
ambayo mara kadhaa imekuwa ikihusishwa na mihadhara ya kidini yenye
vurugu visiwani Zanzibar.
Naye James Mbatia, alisema maridhiano ndiyo yatakayosaidia mchakato
wa Katiba kusonga mbele lakini kwa hali inavyoonekana CCM hawana dhamira
ya kuandika Katiba yenye kujali masilahi ya wananchi.
Alisema wiki iliyopita TCD iliitisha mkutano wenye lengo la kutafuta
maridhiano lakini CCM walituma wawakilishi wasio na nyadhifa za juu kama
zilivyofanya pande nyingine.
Naye Mwenyekiti wa UKAWA, Freeman Mbowe, alisema wameamua kususa
vikao vya Bunge kwakuwa wajumbe wengi kutoka CCM wameacha kujadili
rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Warioba ambayo ndiyo msingi wa
majadiliano yao.
Alisema Tume ya Warioba iliwekwa kisheria na ilifanya kazi ya
kuwahoji watu pamoja na kutumia nyaraka mbalimbali hadi kufikia kutoa
rasimu isiyotakiwa na wajumbe wa CCM walioanza kujadili rasimu
waliyopewa na chama chao.
“Kususia vikao vya Bunge ni miongoni mwa hatua za kutafuta haki,
kuendelea kushiriki vikao hivi ni kuhalalisha na kubariki udhalimu wa
CCM ambayo imeamua kukwamisha Katiba mpya.
“Matusi, ubaguzi, chuki haviwezi kutusaidia kupata Katiba mpya, UKAWA
hatuko tayari kuendelea kushiriki majadiliano yenye mambo
hayo….tunakwenda kwa wananchi kuwaeleza kile kinachofanywa na wajumbe
humu bungeni,” alisema.
Mbowe alisema si lazima Rais Jakaya Kikwete aondoke madarakani wakati
Katiba mpya imepatikana bali mchakato huo unaweza kuendelezwa na rais
mwingine lakini katika mazingira yanayokubalika na watu wote.
Posho
Hata hivyo wajumbe wa Katiba, walikuwa wakipigana vijembe kuwa UKAWA
wameamua kususa vikao vya Bunge baada ya kulipwa posho ya vikao mpaka
Aprili 22 mwaka huu.
Said Nkumba, alisema UKAWA ni wanafiki kwakuwa wamesusia vikao hivyo
baada ya kulipwa fedha hizo na kama wasingelipwa wasingethubu kulikimbia
Bunge.
Livingstone Lusinde, alisema UKAWA, hawana ujasiri wa kutetea
masilahi ya umma bali wapo kwa ajili ya kuangalia masilahi binafsi ndiyo
maana waliondoka bungeni baada ya kusikia wamelipwa fedha mpaka Aprili
22.
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu, Nchemba, alisema jana
waliwasiliana na benki kuona kama zilikuwa zimefanya malipo kwa wajumbe
hao wazuie fedha hizo ili kuwadhibiti wajumbe wa UKAWA ambao wanachukua
fedha bila kufanya kazi
Hata hivyo kauli hiyo ilionekana kupinga na Katibu wa Bunge, Yahya
Khamis, aliyesema fedha hizo tayari zimeshaingizwa kwenye akaunti za
wajumbe.
Khamis, alisema kuanzia Aprili 22, ndiyo watajua kama wajumbe wa
UKAWA, hawatahudhuria vikao vya Bunge hawataingiziwa fedha za kujikimu
na ile ya vikao.
Kwa siku moja wajumbe hao wanalilipwa sh 300,000 ambapo sh 230,000 ni posho za kujikimu, sh 70,000 posho ya vikao.
Makatibu Wakuu UKAWA watoa kauli
Makatibu wakuu wa UKAWA wamesema wabunge wao hawatarejea bungeni
badala yake watazunguka nchi nzima kuelezea namna serikali ya CCM
isivyotaka wananachi wapate katiba wanayoitaka.
Mbali ya msimamo huo, pia wameeleza mbele ya waandishi wa habari kuwa
kuwa Rais Jakaya Kikwete alipopata fursa ya kulihutubia Taifa wakati wa
kulizindua bunge, alianzisha vita ya kisiasa na kuigawa nchi vipande
kutokana na vitisho alivyovitoa kama mkuu wa nchi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Wilbroad Slaa, alisema wao kama makatibu wakuu wanaunga mkono wabunge
wao kutoka nje na kukiita kitendo hicho kuwa ni cha kishujaa na
uzalendo wa kukataa kuburuzwa.
Alisema hakuna chama kinachotaka Katiba Mpya kwa dhamira ya kuvunja
muungano kama wanavyodai CCM, badala yake wanataka katiba ya maridhiano
yanayoongozwa na uamuzi wa wananachi.
“Haya ni mapambano na vita inayohitaji kuunganisha nguvu zote kwa
kuwa hili ni jambo kubwa kwa mustakabali wa taifa na tunapoona watu
wanafanya masikhara kwa ajili ya masilahi na misimamo ya vyama vyao,
hatuwezi kukubali,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa kuna hatari ya mfumo uliozaa katiba inayotumika sasa
kurejeshwa katika mfumo mzima wa upatikanaji wa katiba mpya na kwamba
kama vyama vya siasa walionya hali hiyo mapema kwa ajili ya kulinda
umoja wa kitaifa.
“Tulikuwa tayari kuridhiana kuanzia mwanzo lakini wenzetu hawataki
maridhiano zaidi ya misimamo yao inayolindwa na wingi wao ndani ya
bunge, sasa sisi tuna watu nje ya bunge na kama wanasema kuwepo kwa
serikali tatu jeshi litapindua nchi huo ni uongo, kama mapinduzi
yangefanyika sasa kwa kuwa wamewadhulumu hao wanajeshi hata hela zao za
Operesheni Tokomeza,” aliongeza Dk. Slaa.
Dhana ya Vitisho
Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Shaweji Mketo, alisema ni jambo la
kusikitisha kuona serikali inatumia vitisho kwa wananchi wakati
walibariki mchakato mzima wa kukusanya na kuandika maoni ya wananchi ya
kupatikana katiba mpya
Mketo alisema kitendo cha wabunge wao kutoka nje kilitosha kulivunja bunge kwani rasimu haisemi mjadala wa serikali mbili.
UKAWA haitarudia makosa
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR Mageuzi, Mosena Nyambabe, alisema
kulikuwa na makosa mengi wakati vyama vya siasa viliporidhia kuingia
kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 bila kupata katiba mpya.
Alisema hoja zinazotolewa kuwa wapinzani hawataki katiba mpya
zinapotoshwa makusudi, kwa kuwa madai ya vyama vya upinzani kuhusu
katiba ya wananachi yalianza miaka ya 1960.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment