LATEST POSTS

Thursday, January 10, 2013

ZIARA YA MHESHIMIWA RAIS KATIKA WILAYA YA URAMBO NA KALIUA

 
 
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe: Jakaya Mrisho Kikwete alikua katika Ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Tabora na jana alizitembelea Wilaya za Urambo na Kaliua.
 
Katika ziara yake, Mhe. Rais alizindua ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Ndono - Urambo yenye urefu wa kilometa 42 ambapo fedha za ujenzi wa barabara hiyo zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika ziara yake, Mhe. Rais aliambatana na Waziri wa Maji Prof. Jumanne Magembe na Waziri wa Ujenzi Mhe.John Pombe Magufuli.
Mhe.Magufuli aliwaeleza Wananchi kuwa, ujenzi wa barabara una mikakati yake na sheria za manunuzi ni lazima zifuatwe, hivyo, kasi ya ujenzi inakwenda vizuri na hadi sasa, utekelezaji wa ujenzi unefikia asilimia 29 na anatarajia kazi ikamilike mwanzoni mwa mwaka 2014.
Kabla ya uzinduzi wa ujenzi wa barabara hiyo, Mhe. Rais alisema kuwa, barabara ni muhimu kwani ndio muhimili wa uchumi ndio sababu Serikali imeamua kuwekeza kwenye barabara shabaha kubwa ikiwa ni kuunganisha Mikoa yote kwa rami.
Mhe.Rais aliitaka Wizara ya Ujenzi kuisimamia TANROADS ili nao wawasimamie Wakandarasi wanaojenga barabara hizi ili kuhakikisha kwamba, barabara zinajengwa kwa viwango kiasi kwamba hazitahitaji matengenezo baada ya muda mfupi. Lengo ni kuona kwamba, barabara hazifanyiwi matengenezo hadi baada ya miaka kumi na tano au ishirini.
Akizungumzia tatizo la upatikanaji wa Maji Mkoani Tabora, Mhe. Rais alisema kuwa, tatizo liliopo katika Mkoa wa Tabora ni kwamba, Mkoa huu unapata mvua nzuri lakini shida ni kwamba hauna Makorongo na mabonde hivyo maji hupitiliza mbugani ambako huwezi kuchimba bwawa likawa na kina kikubwa. Hata hivyo, unaangaliwa uwezekano kuvuta maji toka Ziwa Victoria na kuyasambaza katika maeneo mbalimbali ukiwemo Mkoa wa Tabora. Lakini tatizo lingine ni ukosefu wa vyanzo vya maji vya kutosha. Alisema, kwa kuwa Wilaya ya Kaliua kuna mito, Wataalamu waangalie uwezekano wa kuyasambaza maji hayo ili kupunguza tatizo la ukosefu wa maji.
Kwa upande wa tatizo la upungufu wa dawa katika Hospitali na Zahanati, Mhe. Rais aliahidi kwamba atawasiliana na Bohari ya dawa(MSD) ili kujua tatizo ni nini ambalo lisababisha washindwe kutoa dawa kama ilivyokusudiwa. Vilevile aliahidi kushughulikia tatizo la upungufu wa Watumishi wa Idara ya Afya kwa kutoa kipaumbele kwa Mkoa wa Tabora kupangiwa Watumishi wa kutosha wakati wa kuwapangia watumishi vituo utakapofika.
Kwa upande wa bei ya tumbaku, Mheshimiwa Rais aliwataka Wakulima kuhakikisha Wanafunga Tumbaku yao kwa usafi na kuwataka Wateuzi kutoa bei nzuri kwa Wakulima ili waweze kunufaika na kilimo. Aidha, aliahidi kushughulikia suala la upatikanaji wa wateuzi katika Wizara ya Kilimo ili kutatua tatizo hilo.
Imeandikwa na Theresia Chacha
URAMBO

Habari ya Wilaya Ziara ya Mhe. Rais Wilayani Kaliua bado naiandaa nayo nitawaleteeni muda si mrefu.

NB
Wadau, nawaomba radhi sana kwa kuwaletea habari ambayo haina picha. Nimejitahidi sana ku upload picha ili nizitie katika habari hii lakini systeam ya kubrowse kwenye blog yangu inakataa sijui tatizo ni nini?Lakini  Naendelea kulifanyia kazi hili. Mambo yakiwa safi, nitaiupdate habari hii ili muifurahie zaidi ikiwa na picha. Nimeona si vyema siku ipite pasipo kuwajuza kilichojiri katika ziara ya Rais eti kwa sababu picha hazipo. Naomba radhi sana.
 
 

0 comments: